Makala

Sura mpya ya Uhuru Park

April 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

MWONEKANO mpya wa bustani la Uhuru Park umezua msisimko wa aina yake miongoni mwa wakazi wa jiji la Nairobi na Wakenya kwa jumla.

Mnamo Jumapili, Machi 31, 2024 Wakenya waliofika katika bustani hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili walisifia mwonekano wake mpya, wakisema ni dhahiri sasa hicho ni kivutio kipya kwa watalii na wageni tofauti jijini.

Bustani hilo lilifunguliwa upya na Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi mnamo Jumamosi, aliyesema kuwa serikali yake ilikuwa ishapata kibali cha usimamizi wake kutoka kwa Wizara ya Ulinzi, kwani ndiyo ilkuwa ikiendesha urembeshaji na ukarabati huo mpya.

“Muundo mpya wa bustani hili utatoa nafasi kwa Wakenya wa tabaka mbalimbali kufika na kufurahia mandhari ya kipekee jijni,” akaema Bw Sakaja.

Sura mpya ya bustani la Uhuru Park. PICHA|WANDERI KAMAU

Bustani hilo lilifunguliwa kwa mara ya kwanza na Mzee Jomo Kenyatta, mnamo Mei 23, 1969.

Kufuatia urembeshaji huo mpya, baadhi ya masuala ya kipekee ambayo hayakuwepo hapo awali ni ujenzi wa sanamu za kuwakumbuka wapiganaji wa Mau Mau.

Pia, kuna nembo za kuashiria jumbe za amani, upendo na umoja.

Vile vile, eneo la Freedom Corner limejengwa upya kama kumbukizi kwa marehemu Profesa Wangari Mathai, anayekumbukwa kwa juhudi za kupigania na kutetea utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Wakenya waliozungumza na Taifa Dijitali walimpongeza Rais Mstaafu Uhuru Kenytta kwa kuanzisha juhudi za kukarabati bustani hilo upya, wakisema kuwa kibarua kipya kwa serikali ya Rais William Ruto ni kuhakikisha bustani hilo limetunzwa ifaavyo.

“Nimefurahia sana mwonenako wa bustani hili. Hapo awali, baadhi ya sehemu zake zilkuwa zikijulikana kwa uhalifu. Wahalifu walikuwa wakijificha na kupora raia, hasa nyakati za usiku. Hata hivyo, mpangilio huu mpya unahakikisha hata kuna uwepo wa usalama wa kutosha. Tunairai serikali kudumisha hadhi hii mpya ya bustani hili,” akasema Bi Beatrice Mwangi, ambaye ni mkazi wa Doonhold, Nairobi.