• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
SWAGG: Lance Reddick

SWAGG: Lance Reddick

Na THOMAS MATIKO

LANCE Reddick ni mmoja kati ya waigizaji walioweza kuonyesha uwezo mkubwa katika fani hiyo.

Akiwa na umri wa miaka 56, Lance ni miongoni mwa waigizaji wenye asili ya watu weusi waliofanikiwa kupambana na ushindani uliopo Hollywood.

Sanaa

Japo jina lake ni maarufu sana katika ulingo wa burudani, Lance pia ni mwanamuziki makini wa Jazz akiwa tayari ameachia albamu yake.

Albamu hiyo Contemplations & Remembrances ilitoka 2007.

Baada ya kuzaliwa miaka 56 iliyopita kule Baltimore, Marekani, akiwa kijana mdogo alijiunga na taasisi ya Peabody Preparatory kusomea masuala ya muziki.

Kisha alijiunga na Chuo cha Rochester kuzidisha ufahamu wake katika muziki.

Baada ya hapo alihamia jijini Boston, katika miaka ya 80 na kujiunga na Chuo maarufu cha Uigizaji cha Yale School of Drama 1991 alikosomea uigizaji.

Alianza uigizaji miaka minane baadaye akitokea kwenye filamu kadhaa kama Great Expectations (1998), Godzilla (1998), The Siege (1998), I Dream of Africa (2000), zikiwa miongoni za kazi zake za mwanzoni.

Filamu hizo zilimfungulia milango hata zaidi na kuweza kumlambisha dili kwenye ‘series’ kadhaa zilizoishia kuwa kubwa mno kama vile The Wire, Lost, Fringe kati ya nyinginezo.

Toka alipoanza sanaa ya uigizaji, Lance kahusika sana katika filamu kibao kubwa kubwa zikiwemo za hivi karibuni White House Down, John Wick 1,2,3, Avengers: Endgame kati ya nyingi nyinginezo.

Hata hivyo asilimia kubwa ya filamu alizoigiza ametumika kama mwigizaji msaidizi licha yake kuonyesha uwezo anaweza kuvalia nafasi ya mhusika mkuu.

Hata hivyo hana tatizo na nafasi anazopata kuonyesha kipaji chake.

Mkwanja

Licha ya kuigiza katika zaidi ya filamu 50 na nyingi zikishia kufanya vizuri, utajiri wake bado ni mdogo sana.

Makadirio ya utajiri wake kufikia mwaka huu yaonyesha kuwa anafikisha dola 3 milioni tu.

Mkwanja wake umetokana na malipo ya uigizaji pamoja na sauti yake kutumika kwenye ‘video games’ kadhaa za aksheni.

Uhusiano

Amekuwa kwenye ndoa kwa miaka minane sasa kwa mkewe Stephanie Day. Walifunga ndoa Juni 2011 hata hivyo uhusiano wao ulianza toka walipokuwa matineja.

Mjengo

Anamiliki mjengo wa kifahari mjini Los Angeles anakoishi na mke wake Stephanie.

Hata hivyo, kayaweka maisha yake kuwa siri sana. Haifahamiki ikiwa wana watoto, ila kuliwahi kuwepo na tetesi kuwa mkewe aliwahi kunasa ujauzito na kujifungua binti wakiwa bado ni wapenzi katika maisha yao ya ujana.

Hata hivyo, mpaka sasa taarifa kuhusu mtoto au watoto wao zimeendelea kuwa siri kubwa.

Usafiri

Lance anamiliki magari kadhaa ya nguvu yanayomrahisishia usafiri wake mjini yakiwemo Range Rover, Mercedes Benz, Bentley na Lamborghini.

You can share this post!

VIDUBWASHA: Kwa mashabiki wa Barca (Oppo Reno 10X Zoom FC...

Wafuasi wa Tshisekedi na Kabila wazua taharuki DRC

adminleo