SWAGG: Missy Elliott
Na THOMAS MATIKO
KAMA wewe ulianza kusikiza muziki wa Hip hop katika miaka ya themanini na tisini, basi sharti unamfahamu rapa wa kike Missy Elliott.
Anaweza akawa ametuliza kasi ya muziki wake katika miaka ya hivi karibuni, ila mwanamama huyu alitisha sana miaka hiyo na kuishia kuwa mmoja kati ya marapa maarufu wa kike duniani.
Sifa zake zilizotokana na muziki pia zilimfungulia milango ya utajiri kwa sababu wadau wengi walimkubali hivyo walimsapoti kwa njia tofauti kwa kile alichokuwa akikifanya.
Wasifu wa kikazi wa Missy Elliott kwenye muziki wa Hip hop ni mkubwa sana, huyu sio rapa tu, pia ni produsa makini, dansa hatari na mtunzi mashairi stadi.
Jitihada zake kwenye gemu zimempelekea kutwaa tuzo tano za Grammy, hizi zikiwa ni tuzo za hadhi kubwa duniani katika ulimwengu wa muziki.
Missy Elliott kafanya kazi na manguli wote wa muziki ambao ni malejendari kwa sasa. Hapa unawazungumzia watu kama Jay Z, Dr Dre, Madonna, Janet Jackson, Katty Perry, Beyonce, Timbaland na wengine kibao.
Maisha ya utotoni
Missy Elliott alizaliwa Julai 1971 na kupewa jina Melissa Arnette Elliott kule Portsmouth, Virginia.
Babake Ronnie alikuwa ni mwanajeshi huku mamake Patricia akiwa mfanyakazi katika kampuni ya umeme.
Baada ya kuacha kazi ya kijeshi, maisha yalikuwa magumu sana kwa Ronnie na familia yake na mara nyingi angemdhalilisha Patricia kwa kumpiga mbele ya binti yao.
Haya maisha yalimfanya kuogopa sana kwa namna alivyokuwa akiona mamake akiteswa na babake. Lakini Missy Elliott alikuja kutishika zaidi yalipomkuta mabaya zaidi.
Hii ni baada yake kunajisiwa na binamu yake wa karibu, alipokuwa na umri wa miaka minane tu.
Tukio hilo lilimfanya awaandikie barua marehemu Michael Jackson aliyekuwa akivuma wakati huo na dadake Janet Jackson wamwokoe kwa kumtambulisha kwenye muziki ili aweze kuepukana na mateso aliyokuwa akipitia.
Kwa bayati mbaya Janet na Michael hawakuwahi kuijibu barua yake. Kukosa kupata majibu kulimuumiza sana na aliishi kulia kila kukicha.
Japo kwa sasa ni marafiki na Janet baada yake kuja kuwa staa, wakati mwingine huwa anashindwa kuelewa kwa nini hakujibu barua yake.
Muziki
Maisha yalipozidi kuwa mabaya hasa ya mamake kuteswa na Ronnie, alimwomba atoroke sababu angeishia kumuua siku moja.
Kipindi hiki Missy Elliott alikuwa na umri wa miaka 14.
Kusoma ikawa taabu ila alipambana.
Ni kwenye harakati hizo akiwa shule ya upili, ndipo alianzisha kundi lake la Sista lililoishia kusainiwa na lebo ya Swing Mob Records.
Wakati akidhani nyota yake inaanza kung’aa, pigo lingine lilimkuta pale Swing ilipoamua kufunga biashara huku ikizika albamu ya kwanza aliyokuwa karibu kuiachia.
Msanii solo
Baada ya kufa kwa Swing, kundi lake la Sista pia likasambaratika. Hapo Missy Elliott akaamua kujiweka karibu zaidi na rafiki yake wa utotoni ambaye ni produsa, Timbaland.
Kwa pamoja waliwatengeneza biti na traki za wasanii mastaa kama vile Aaliyah, AWV, Puff Daddy, Raven Symone.
Nyota ilipong’aa
Akiwa kwenye pilkapilka hizo za kuwafanyia mastaa wengine kazi, mwaka 1996 alikutana na Sylvia Rhone, Afisa Mkuu Mtendaji wa Elektra Entertainment Group iliyojihusisha zaidi na usambazaji wa muziki.
Rhone alimshauri Missy Eliott afungue lebo yake ya Goldmind ambapo alirekodia albamu yake ya kwanza Supa Dupa Fly iliyotoka mwaka 1997.
Elektra ilihusika pakubwa katika usambazaji wa albamu hiyo iliyoishia kumfungulia milango baada ya kuuza Platinum (zaidi ya nakala milioni saba).
Huu ukawa ndio mwanzo wa mafanikio yake. Alifuatisha na albamu zingine tano zaidi na zote zikaishia kugonga Platinum.
Albamu yake ya tano ilitoka 2005 na toka kipindi hicho, Missy Elliott alipotea kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 10 hadi 2016 aliporejea tena.
Utajiri
Thamani ya mali yake na fedha zilizo benki, inakadiriwa kuwa haipungui dola 50 milioni.
Majumba
Kawekeza sana kwenye masuala ya ujenzi akiwa anamiliki majumba manne ya nguvu katika mitaa mbalimbali ya kifahari kule Marekani.
Nyumba mbili zipo Virginia, Miami huku Atlanta na New Jersey akiwa na moja moja.
Usafiri
Analo rundo la magari ya nguvu mzee. Unaambiwa anamiliki mchuma wowote mzuri na wenye bei mbaya. Missy Elliott anamiliki zaidi ya magari 10 ya nguvu.
Utaanza na Rolls Royce Phantom (Sh42 milioni), Lamborghini Aventador (Sh45 millioni), Bentley Continental, Ferrari Enzo, Lamborghini Diablo (Sh9 Millioni), umalizie na Lamborghini Gallardo ambazo anamiliki mbili kila moja ikimgharimu Sh20 milioni.