• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
SWAGG: Samuel L. Jackson

SWAGG: Samuel L. Jackson

Na THOMAS MATIKO

HUWEZI ukawa mpenzi ashiki wa sinema na ikawa humfahamu Samuel L. Jackson.

Na kama itokee hivyo, basi itakuwa wewe ni mbaguzi wa rangi au tu mmoja kati ya mashabiki ovyo.

Miongoni mwa waigizaji maarufu na tajiri wenye asili nyeusi waliosumbua sana kule Hollywood yupo huyu jomba mwenye umri wa miaka 71.

Alizaliwa mwaka 1948, enzi ya utawala wa kikoloni uliokuwa umeshamiri barani Afrika.

Jinsi Waafrika walivyokuwa wakiteswa na kubaguliwa na mbepari kwao Afrika, ndivyo nao watu wenye asili nyeusi kama Samuel waliozaliwa Amerika nao walikuwa wakinyanyaswa na kubaguliwa.

Lakini leo hii, hawa wazungu wanampa heshima zake zote. Tena sio tafadhali. Yaani ile ‘fulu respecti’ kama ukiamua kumuuliza pasta mtatanishi Ng’anga wa kanisa la Neno ambaye hivi majuzi kawatolea mapovu maaskofu wake.

Samuel leo wanampa zile ‘shikamoo baba!’ lakini ndio afikie upeo huu, alipambana sana.

Utajiri

Kufikia Aprili 2018 utajiri wake ulikuwa unakadiriwa kufikia dola 220 milioni. Unaweza kuwa na uhakika kwamba thamani yake itakuwa imepanda kufikia sasa hasa baada ya filamu ya Avengers: Endgame kuendelea kufanya vizuri. Ni mojawapo ya filamu kubwa ambazo amehusika siku za hivi karibuni zinazofanya vizuri sokoni.

Miaka minane iliyopita, 2011, aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu Guiness Book of World Records baada ya kutajwa kuwa mwigizaji wa pekee ambaye uhusika wake ulipelekea filamu alizotokea kuingiza jumla ya dola 7.4 bilioni kimauzo kwenye Box Office. Pia hilo lilimfanya kuwa kati ya waigizaji wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi duniani.

Filamu zilizomtajirisha

Alianza taaluma yake ya uigizaji 1973 lakini licha ya kuhusika kwenye filamu kibao na vipindi vya televisheni toka kipindi hicho, ilimchukua miaka 21 kutoka vizuri kwenye gemu.

Hii ni baada yake kuigiza kwenye filamu ya Pulp Fiction (1994).

Jina lake lilianza kupata umaarufu na kuwa kubwa hata nje ya Amerika.

Ufunuo huo ukamfungulia milango. Aliendelea kuigiza akitokea kwenye filamu zaidi ya 100.

Lakini katika filamu zote zile zilizofanya vizuri sokoni na kuweza kumtajirisha ni Avengers: Endgame (2019) iliyoingiza zaidi ya dola 800 milioni mpaka sasa, Avengers: Infinity War (2018) dola 679 milioni, The Avengers (2012) dola 624 milioni, Incredibles 2 (2018) dola 609 milioni na Captain Marvel (2019) dola 426 milioni.

Jinsi anavyokafunga

Kwenye suala la senti, ndio hatanii kabisa. Anakafunga kukafunga asikudanganye mtu. Ukiachana na mshahara wake mrefu usiopungua dola 10 milioni kila mwaka, pia anaingiza senti zaidi kupitia uprodusa. Sio tu mwigizaji. Malipo ya uprodusa wa vipindi na filamu anavyohusika navyo pia unamwongezea hesabu.

Tatu, anaingiza mkwanja kutokana na mikataba ya matangazo ya kibiashara aliyosaini na kampuni mbalimbali. Zipo dili kibao kama viole Apper, Capital One na kadhalika ambazo humtumia kujiuza huku akivuta mamilioni ya dola kila kukicha.

Nne, analipisha mpunga mzuri kwa kuingiza sauti yake kwenye filamu za vibonzo (animations) na pia ‘video games’. Kwa mfano sauti yake imetumika kwenye The Incredibles na ‘video game’ ya Grand Theft Auto: San Andreas (2004).

Boma la uhakika

Anaishi kule Los Angeles anakomiliki jumba la kifahari lenye vyumba sita vya kulala vyote vikiwa vinajitegemea. Yaani kila chumba kina choo, bafu, na hata sebule ya kipekee.

Alilinunua Juni 2000 kwa thamani ya dola 8.35 milioni. Hii ina maana kuwa miaka 19 baadaye, thamani ya mjengo huo kwa sasa itakuwa ni zaidi ya dola 20 milioni kama akiamua kuliuza.

Kule New York, anao mjengo mwingine wa vyumba vinne alioununua 2005 kwa dola 4.8 milioni lakini kufikia Novemba mwaka jana aliuweka mnadani kwa ada ya dola 13 milioni.

Ndoa

Amedumu kwenye ndoa yake ya mke mmoja LaTanya Richardson kwa kipindi cha miaka 39 sasa toka walipooana 1980. Ndoa hiyo imewajalia mtoto mmoja pekee binti mwenye miaka 37, Zoe Jackson.

Samuel anasema siri kubwa ya mafanikio ya ndoa yao licha ya panda shuka nyingi ni kiapo walichopeana cha kuhakikisha ndoa yao kama watu wa asili nyeusi haivunjiki.

Usafiri wa kiwango

Kwa mkwanja wake halafu na umri huo kwa nini ajinyime! Licha ya kuwa mzee, ni mpenzi mkubwa wa mikebe ya nguvu.

Anamiliki kadhaa kuanzia Maybach 57 S iliyomgharimu Sh40 milioni, Jaguar XF (Sh5 milioni), Rolls Royce (Sh33 milioni), Range Rover (Sh8 milioni) na Toyota Camry (Sh3.5 milioni).

SWAGG

Huyu ni jamaa wa masuti kwa sana tu. Lakini pia anapenda zile kofia ziitwazo kitaani ‘Godfather’ na miwani za kawaida ila za kidesaina.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Naona aibu kutembea na mke wangu...

Rais ‘matatani’ kuhusu kura ya maamuzi

adminleo