• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
SWAGG: Sofia Vergara

SWAGG: Sofia Vergara

Na THOMAS MATIKO

SOFIA Vergara ni miongoni mwa waigizaji wa kike wanaotajwa kuwa matajiri kupindukia hapa duniani.

Anaweza akawa sio maarufu sana kwa mashabiki wengi wa filamu hapa nchini Kenya na barani Afrika kwa ujumla, pengine kutokana na aina ya filamu anazoigiza, lakini kule Hollywood wanamtambua sababu mchango wake umeweza kuingiza hela kinoma.

Akiwa na umri wa miaka 46 kwa sasa, Sofia kaendelea kuvuruga tasnia ya uigizaji kwa kuwapa wakati mgumu waigizaji chipukizi.

Alivyoanza uigizaji

Unaweza kusema ilikuwa ni bahati mbaya hadi yeye kuishia kuwa mwigizaji sababu sio kitu alichokuwa amekipangia katika maisha yake ya awali.

Akiwa kwao Colombia kabla ya kuhamia Marekani na kuchukua uraia wa taifa hilo vilevile, alisomea udaktari wa meno akahitimu na kupata ajira.

Hata hivyo akiwa na umri wa miaka 23, aliachana na kazi hiyo ya kuwa mtaalamu wa meno na kuingilia uanamitindo.

Uanamitindo nao ulimkuta kwa bahati mbaya.

Wakati mmoja akiwa anajivinjari kwenye ufuo wa baharini kule kwao, mwonekano wake ulimvutia mpiga picha mmoja aliyemtokea na kumshawishi ajaribu kwani alikuwa na sifa zote.

Kupitia koneksheni za mpiga picha huyo, Sofia akaishia kujiingiza kwenye uanamitindo akihusika sana kwenye biashara matangazo.

Taratibu akaanza kujisogeza katika masuala ya kuigiza hasa alipopata kazi ya kuwa mwenyeji wa kipindi cha usafiri ‘Fuera de serie’ kilichomtambulisha kwenye hadhira ya Amerika.

Mama wa watu akazidi kukaza buti na kuishia kupata kazi zingine kibao za uigizaji zilizozidi kumsukuma hadi alipoangukia ile iliyomtoa vyema na kumtangaza hata zaidi, kipindi cha televisheni cha Modern Family 2009.

Kutokana na ustadi wake, Sofia aliishia kuteuliwa mara nne kwenye tuzo za Emmy. Kabla kutokea hapo, alikuwa tayari ameshapata shavu kwenye filamu ya Four Brothers (2005) na kazi zingine mbili za produsa mtajika Tyler Perry, Meet the Browns (2008) na Madea Goes to Jail (2009).

Wasifu wa kazi zake ulipanda na Sofia akazidi kupokea michongo kibao akitokea kwenye filamu nyingi zaidi zilizofanya vyema kama vile Hot Pursuit (2015), Machete Kills (2013), The Smurfs (2011) kati ya nyinginezo. Kadri alivyojihusisha na filamu nyingi ndivyo thamani na brandi yake ilivyopanda.

Thamani

Utajiri wake ulikadiriwa kufikia dola 160 milioni kufikia mwaka jana ambapo aliuaga kwa kuingiza dola 42.5 milioni kwa mujibu wa Forbes.

Kwa miaka saba toka mwaka jana kurudi nyuma, Sofia ndiye aliyekuwa mwigizaji wa vipindi vya televisheni aliyeongoza kwa kulipwa mshahara mkubwa zaidi ya wote duniani.

Sofia anapiga mkwanja zaidi kupitia dili za kimatangazo alizosaini na kampuni mbalimbali kama vile Pepsi, Kmart, Synthroid kati ya nyinginezo.

Mahusiano

Alifunga ndoa akiwa na umri wa miaka 18 pekee na mpenzi wake Jo Gonzalez ambaye pamoja walijaliwa kupata mtoto wa kium,  Manolo aliyezaliwa Septemba 1991.

Hata hivyo, ndoa yao ilivunjika 1993 walipotalikiana.

Miaka kadhaa baadaye aliingia kwenye uhusiano mwingine na Nicholas Loeb ambaye alimchumbia 2012 baada ya kuwa pamoja kwa miaka miwili. Hata hivyo Mei 2014 walivunja uchumba huo na kuachana.

Sofia alikutana na mwigizajji mwenza Joe Manganiello Disemba 2014 na baada ya uhusiano wa miezi sita, walioana Novemba 2015.

Mpaka sasa ndoa hiyo bado ipo imara. Wikendi hii walisherehekea kutimiza miaka minne ya ndoa yao kwa kuenda kula bata Italia.

Mjengo

Aprili 2014, Sofia alinunua jumba la kistaa katika mtaa wa kifahari wa Beverly Hills kwa thamani ya dola 10.6 milioni.

Mjengo huu una vyumba saba vya kulala na bafu 11. Pia unao ‘spa’ na kidimbwi cha kuogelea na sifa zinginezo kama hizo.

Usafiri

Anazo mashine za kutosha kuanzia Range Rover, Mercedes Benz, Bentley na Audi.

You can share this post!

Soko la Pamoja la Afrika: Makubaliano yaafikiwa

Pogba, Lingard waonekana wakizozana

adminleo