• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
TAARIFA YA KIPEKEE: Mimi sitoki jamii ya Abagusii, msanii Getumbe aweka wazi

TAARIFA YA KIPEKEE: Mimi sitoki jamii ya Abagusii, msanii Getumbe aweka wazi

NA FRIDAH OKACHI

MSANII wa Injili William Getumbe Mutua almarufu ‘Yesu Ninyandue’, amekanusha kutoka jamii ya Abagusii.

Bw Getumbe aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba kuhusishwa kwake na jamii hiyo kunatokana na kufanya kazi ya muziki na Christopher Nyangwara Mosioma, almaarufu Embarambamba.

Mwanamuziki William Getumbe akizumgumza na mmoja wa mashabiki kwenye bustani ya Jevanjee | PICHA| FRIDAH OKACHI

“Vituko kwenye sanaa ndio vilifanya kuhusishwa na jamii hiyo. Mimi ni mzaliwa Machakos, baba anatoka ukambani naye mama anatoka Kaunti ya Embu,” anasimulia Bw Getumbe.

Mwanasaikolojia huyo ambaye ni mkazi wa Kaunti ya Uasin Gishu alisema wazazi wake walihamia katika eneo hilo.

“Wakati mwingine huwa nasoma taarifa kuwa eti mimi ni msanii kutoka eneo la Nyanza…. Wazazi wanatafuta riziki yao Uasin Gishu, nasi watoto tukafuata nyayo hizo,” asema akitabasamu msanii huyo.

Kuhusu uimbaji wake wa kutumia maneno yanayotisha na kuogopesha kwenye masikio ya mashabiki wake, alisema huenda akabadilisha baada ya kupokea maoni mbali mbali.

‘Teknolojia ya kisasa ya maneno’

Bw Getumbe akifanyiwa mahojiano na Taifa Leo| PICHA| FRIDAH OKACHI

Alisisitiza kuwa teknolojia ya kisasa ilichangia kutumia maneno hayo kupata umaarufu kwenye sanaa yake.

“Mimi ni mwanasaikolojia, na wakati nyimbo zangu haswa ule wa ‘Yesu Ni nyandue’ ulikashifiwa na mashabiki, nimekusanya maoni hayo na hivi karibuni nitatumia lugha ambayo inavutia na kupendeza,” alikiri baada ya kuulizwa hatima yake.

Aliwataka wanamitandao na mashabiki kukumbatia teknolojia ambayo ina athari zake ambazo zinatajwa kuwa mbovu kwa jamii.

“Sasa hivi wanasema lugha ambayo natumia ni mbovu kwenye mitandao ya kijamii. Leo wanakataa, kisha kesho wataanza kukubaliana na matamshi hayo,” alisema Bw Getumbe.

Mwanaharakati huyo alisema lugha aliyokuwa akitumia kwenye nyimbo zake huenda ilikuwa ni ndimi (speaking in tongues) ambayo watu wengu walimnukuu visivyo kwa kuhusisha na lugha ya Kiswahili bila kufuata Biblia.

“Mbinguni hakuna lugha ya Kiswahili ambayo tutaongea, ninapoimba wakati mwingine natumia ndimi, hili ndio jambo ambalo serikali haifahamu,” alisema mwanaharakati huyo.

Safari ya kushtakiwa

Bw Getumbe akijieleza kwenye mahojiano| PICHA| FRIDAH OKACHI

Baada ya kukamatwa na maafisa wa polisi na kisha kuachiliwa kwa bondi ya Sh10,000, mwanamuziki huyu bado anasubiri Bodi ya Uainishaji Filamu Nchini (KFCB) kumfikisha mahakamani na kushtakiwa kwa matumizi ya lugha mbaya kwenye filamu zake, mtindo wa mavazi na kulipa leseni ya Sh250,000 kama ilivyodai awali.

“Bado sijafikishwa, tarehe waliyofaa kunipeleka kortini, nilifika kwenye kituo cha polisi kuwasubiri lakini nikapata ujumbe hawatapatikana. Wamefanya hivo mara tatu sasa,” aliongeza msanii huyo.

Japo, mwanaharakati huyo na pia msanii alienda mahakamani kupinga kiasi cha pesa alichohitajika kulipa, alisema kesi hiyo itasikizwa hivi karibuni.

“Wakili wangu alienda mahakamani kupinga faini ile kwa kuwa nafahamu leseni ya msanii inafaa kulipwa mara moja kwa mwaka. Lakini kulingana na wao faini ile nilistahili kulipia kila video ambazo nimesambaza kwenye mtandao ambayo ni kinyume na sheria,” alidokeza.

  • Tags

You can share this post!

Mahangaiko: Wakazi wanavyong’ang’ania maji...

Tafuteni barakoa mvalie sababu kuna wimbi la mafua, Wakenya...

T L