Makala

Tabasamu tele wakazi wakifaulu kupiga simu kwa mara ya kwanza bila kupanda juu ya mti

April 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA OSCAR KAKAI

AKIWA ameketi kwenye shina ya mti pamoja na marafiki zake wengine ndani kwenye msitu katika kijiji cha Akiriamet, wadi ya Masol, Lakapi Depamuk akiwa na simu yake ya rununu aina ya ‘Mulika Mwizi’, kwa sauti ya juu akitabasamu anaongea na mwandani wake mwenye yuko katika mji wa Kapenguria.

Bw Depamuk, 37, ni mwenye furaha sababu ni mwanzo mpya kwake pamoja na wakazi wengine.

Hii ni kwa sababu, tangu anunue simu yake mwaka wa 2019, Depamuk amekuwa akisumbuka. Amekuwa akipanda kwenye miti akitafuta mawimbi ya kupiga ama kupokea simu.

Hata hivyo, mambo ni shwari katika eneo hilo. Kijiji chake kwa sasa kina mawimbi ya simu.

“Sasa ninaweza kupiga simu hata nikiwa chini ya kitanda, ndani ya shimo, bonde ama mto bila shida yeyote.  Sipandi miti ama milima tena,” anasema.

Anaongeza kusema kuwa hatua hiyo imemsaidia kusaka mifugo walioibiwa kwenye mashambulizi na majangili kutoka jamii jirani.

“Tulikuwa tukituma watu kupeana ujumbe lakini sasa mambo ni rahisi sababu tunapiga simu kwa watu katika maeneo ya Kainuk na Sigor ili hatua ichukuliwe kwa wakati. Majangili walikuwa wakitoroka bila sisi kujua,” anasema Bw Depamuk.

Mkazi wa Masol, Pokot Magharibi akipiga simu. Picha|Oscar Kakai

Agnes Cherapuo mwenye umri wa miaka 34 kutoka eneo la Masol ni mama mwenye furaha bila msongo wa mawazo.

“Ninafuraha sababu ninaweza kumpigia mhudumu wa afya wakati mtu ni mgonjwa ama mama mja mzito anataka kujifungua. Vituo vya afya viko mbali. Tulikuwa tukibeba wagonjwa mikononi kufikia wahudumu wa fya lakini sasa niko na namba ya simu ya mhudumu wa afya ambaye mimi humpigia simu wakati wa suala la dharura,” anasema Bi Cheparuo.

Maeneo mengi ya mashinani katika kaunti ya Pokot Magharibi yalitengwa na hayana mawimbi ya mawasiliano kutokana na idadi ndogo ya watu na umaskini.

Hata hivyo, ni mwanzo mpya kwa wakazi katika maeneo hayo baada ya mamlaka ya mawasiliano kupitia kwa Universal Service Fund (USF) kuleta huduma hizo.

Vilevile, vijiji vya mashinani vimepigwa jeki na mtandao wa kidijitali wa mawasiliano.

Wakazi ambao hawakusoma sasa hupeana habari kwa maafisa wa serikali ikiwa kuna shambulizi ama wizi wa mifugo. Hii imechangia visa vya ujangili na wizi wa mifugo kupungua.

Kwa sasa wakazi wa eneo kama Akiriamet hawatembei mwendo mrefu kupiga simu. Wanaenda kwenye kituo cha kidigitali cha mawasiliano kupiga simu bila malipo zaidi.

Wakazi wameelewa maisha ya kidijitali na kufurahia mtandao ya bure na hata kujaza simu moto.

Naomi Chepsurum kutoka eneo la Masol anasema kuwa mpango huo unanufaisha jamii kwa ujumla na watoto wa shule ambao wazazi wao hawawezi kupata huduma za mtandao kwa wanao.

Mawasiliano ya kidijitali yameimarika katika maeneo hayo kutokana na vizingiti vya umbali, gharama na ugumu wa kupata huduma hizo.

Kati ya kata ambazo zimenufaika na mpango huo ni Chepserum na Apuke ambapo mawimbi ya mawasiliano tayari yamewekwa. Kata zingine ambazo zimenufaika na huduma hizo ni Kiwawa, Kola, Lotukum, Kaputulomwo, Ombolion, Kachawa, Amala, Meshau, Emboasis, Kopsori, Akiriamet, Marush na Popoo.

Uwezo wa kupiga simu bila kupanda milima au miti umeleta mwamko mpya eneo la Masol. Picha|Oscar Kakai

Mpango huo umegharimu Sh42.4 milioni kupitia kwa mamlaka ya mawasiliano ambayo imeunganisha kata 14 katika kaunti ya Pokot Magharibi kwa awamu ya kwanza na ya pili.

Mamlaka hiyo pia inapanga kuweka huduma hizo kwa awamu ya tatu kwa kata zingine 68 katika kaunti hiyo. Hiyo itagharimu Sh148.6 milioni katika kata za Chepkoriong, Parua, Kale, Kokwopsis, Nyarkulian, Kamelei na Tapach ambapo mawimbi ya mawasiliano yataimarishwa.

Katibu katika Wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano Eric Kiraithe ambaye alikutana na maafisa wa serikali, maafisa wa wadi na machifu kutoka maeneo ambayo yatanufaika, Jumanne mjini Kapenguria na kujadili kuhusu masuala ya kidijitali pia walizuru maeneo ya mpango huo na kuongea na walionufaika.

Bw Kiraithe anasema kuwa mamlaka ya mawasiliano itahakikisha kuwa kuna usawa kwa mawasiliano kwa kila mtu nchini.

Naibu wa kamishna katika kaunti ndogo ya Pokot Kusini Pokot David Boen alisema kuwa mpango huo utakuwa wa manufaa kwa wakazi.

“Awali ilikuwa vigumu wakati wa mashambulizi. Ripoti kutoka kwa machifu sasa zinatufikia kwa urahisi,”alisema.