• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Tabia uchwara zinazoshusha maana halisi ya heshima mazishini

Tabia uchwara zinazoshusha maana halisi ya heshima mazishini

Na MWANGI MUIRURI

WAKATI mpendwa amepoteza uhai wake kwa mkuki wa mauti, walioachwa nyuma katika uhai husononeka si haba na kilio cha majonzi hutanda.

Hata hivyo, kuna waombolezaji ambao huzidisha majonzi hayo kupitia tabia zao mbovu kipindi hicho kigumu na hadi mazishi.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mkuu wa Kanisa Katoliki katika Kaunti ya Nyeri, Askofu (mstaafu) Peter Kairu, kupoteza mpendwa kwa mauti ingawa ni uamuzi wa Mungu aliye mmiliki wa uhai, ni kawaida ya binadamu na moyo wake dhaifu kuona kana kwamba ameonewa.

Anasema kuwa dhana hiyo ndiyo husababisha kilio cha mahangaiko walioachwa wakijiuliza maswali mengi bila jibu, lakini machozi hayo hatimaye yakichangia kupata nafuu na kukubali kwa hali na kuendelea mbele na maisha.

“Ni jukumu la wale ambao ni wapenda wema kutwaa jukumu la kutuliza nyoyo za hao walioachwa na kujiepusha na hali yoyote ya kuwazidishia walioachwa mahangaiko ya majonzi. Kuna wengine katika jamii walio na tabia mbovu ya kuanza kusambaza udaku usiofaa kuhusu mwendazake, wale ambao watajaribu juu chini kuzua kashfa katika hali ya mauti hata iwe hayo mauti yalitokea katika hali inayoelezeka kwa urahisi. Wengine si madaktari lakini utawapata wakikueleza alikougua, kilichoenda mrama katika matibabu na mbona mauti yakazuka,” asema Kairu.

Anasema kuwa wengine hujitokeza katika matanga sio katika ile nia njema ya kusaidiana na wanaoomboleza kustahimili makali ya mkuki wa mauti, bali kama watafiti wa udaku wa kusambazwa, wakitaka kujua kumeachwa mke au mume mwenye umri wa miaka mingapi na umbo gani, watoto wangapi na hali ya kimaisha katika boma hilo.

Anasema kuwa huo ni sawa na ushetani kwa sababu ni Ibilisi ndiye tu atajitokeza katika familia inayoomboleza kwa nia nyingine isipokuwa ile ya kutaka kushirkiana na kutulizana.

“Mwovu hutafuta ushahidi wa kuandaa karamu katika majukwaa ya udaku na fitina,” asema.

Askofu huyo anasema kuwa hali hii haijaanza leo wala jana, kwani kulikuwa na wale ambao walichangia pakubwa kifo cha Yesu Kristo bila ya kufuata utaratibu wa haki bali waliongozwa na udhalimu.

Anasema kuwa hata leo hii, hao makuhani wa udhalimu wangali wapo na wanaendeleza sera za “watumwa wa dhambi na ambao katika majonzi, wao hupata sababu ya kuangua kicheko.”

Kuna hali zingine ambazo hujitokeza katika hafla za maombolezi ambazo huishia kuangazia jamii kama iliyooza kimaadili hasa wale ambao huchukua fursa ya kuanda amazishi kujitajirisha.

Familia moja yapanda maua katika kaburi la mpendwa wao. Picha/ Mwangi Muiruri

Kwa mujibu wa Mshirikishi wa Masuala ya Usalama katika eneo la Rift Valley, George Natembeya, kuna visa vingi amekumbana navyo akitekeleza wajibu wake serikalini na ambavyo “vimeniacha nikiwa na maswali tele kuhusu utu katika jamii.”

Anasema amekumbana na matanga bandia kuandaliwa kwa msingi wa kukusanya hela, walio hai wakitangazwa kama maiti ili njama hiyo ifaulu.

“Kuna baadhi huwa na ukatili uliopitiliza ambapo wao huandaa harambee kuchangia mgonjwa aliye hospitalini akihitaji msaada wa dharura ili atibiwe na maisha yake yanusurike, lakini wanapopewa hizo pesa, wanatelekeza yule mgonjwa na wanaishia kugawana hizo pesa na yule mgonjwa anaishia kuaga dunia,” asema Natembeya.

Anasema kuwa pia kuna wale ambao hupanga njama ya kuua aliye hai kwa msingi duni wa ulafi wa mali ili wabaki na mali ya mwendazake.

“Yaani, mtu anapanga mauaji ya binadamu mwenzake ili mali itwaliwe; mali ambayo hata aliyeitwaa hataenda nayo kaburini bali ataaga dunia na aiache nyuma ikiendelea kuwafaa wengine na akijua vyema kuwa Mungu hatampa amani ya kuponda mali hiyo ya kupatikana kwa njia hiyo ya ukatili,” asema.

Kulingana na Natembeya, hali hii imesambaa katika jamii ambapo hata wajane na watoto hutimuliwa baada ya mauti ya baba mzazi ili mali iondoke kutoka mikononi mwa familia hiyo na ibakie mikononi mwa walafi wachache.

Katika hali hizo, Natembeya ambaye ni mwokovu katika imani ya Kikristo anasema kuwa kunahitajika kuwe na ustaarabu katika hali ya majonzi ya mauti na wote wajipe utaratibu ulio na utu wa kushiriiki hafla hizo.

“Kunao hufurahia mauti ili wanyakue hata wajane ambao wameachwa nyuma…wengine wanafurahia kwa kuwa watapata biashara ya kuuza majeneza, ya kuuza huduma za uchukuzi, biashara za kuhifadhi maiti…biashara ndani ya mauti sio utu,” ateta.

Bw James Njuguna ambaye ni kiongozi wa kundi la vijana wabunifu katika sanaa ndani ya Kaunti ya Nyeri anasema ameshuhudia visa ambapo wengine hushiriki matanga wakitekeleza ujasusi wa jinsi uwizi na ambapo familia zinazoomboleza hupoteza ama mifugo au bidhaa za nyumbani.

“Kuna wanaoiba magari na pikipiki katika hafla za maombolezi na mazishi huku wengine wakipora mikoba ya wenyewe. Ushauri wangu wa dhati ni kwa wale ambao husafiri kutoka mijini kuhudhuria mazishi. Mazishi ya heshima ni pale utashiriki katika kila awamu ya hafla hiyo ya kumsafirisha mwendazake hadi kaburini akaanze maisha yake mapya ya kuzimu,” asema Bw Njuguna.

Anaongeza kuwa ameshuhudia visa ambapo kuna waombolezaji wa mijini ambao wakifika katika hafla ya mazishi huanza kusaka mahaba vijijini huku wengine wakiuliza ni wapi wanaweza wakajinunulia ulevi au hata bangi. Anaongeza kuwa wengine huanza kutangatanga hadi mashambani ya majirani vijijini wakisaka maparachichi, mboga na matunda mengineo, wengine wakianza kujinunulia kuku wa kurejea nao jijini.

“Utapata kuwa hao watu wanapiga kelele ibada ikiendelea na hata hawashiriki maombi na nyimbo na la kuchukiza zaidi, katika kando mwa kaburi, hutawaona wakisaidiana kurudisha mchanga. Kazi yao huonekana wakivamia chakula, chai na soda na maji ya chupa huku wanakijiji wakitwikwa mzigo wa kuchapa kazi ya kuchimba na kujaza kaburi katika mazishi,” asema.

Anasema kuwa hao wengi wa mijini kazi yao mazishini huwa ni kuonyesha wanavijiji nguo zao za bei ghali, mavazi ya kuchochea hisia za kimahaba, kelele na vurugu wakipiga picha mitindo ya selfie, kuweka nyimbo kwa simu kwa sauti ya juu na kupigapiga picha kila kitu katika hapo mazishini na pia kuchukua mikanda ya video.

Amalizia: “Kuna tofauti ya kuhudhuiria mazishi na kuhudhuria hafla ya michezo ya kuigiza.”

You can share this post!

AK yatafuta suluhu ya mbio za mita 10,000

SHANGAZI AKUJIBU: Niliacha mume wangu, nikashikana na...

adminleo