Makala

TAHARIRI: EACC na DCI zina meno ya kung'ata wafisadi

May 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

Wakenya wamechoshwa na wizi wa kila mara wa pesa za umma unaoripotiwa katika magazeti na vyombo vingine vya habari. Ufichuzi wa hivi majuzi wa Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu nchini Bw Ouko kuhusu bajeti tata ya Kaunti ya Kiambu ni jambo la kuhuzunisha hata zaidi.

Magavana na maafisa wengine wa serikali wamebuni mbinu mpya za kufuja mali ya umma wakidhani kwamba hawatagunduliwa.

Hata ingawa Katibu katika Hazina ya Kitaifa Dkt Kamau Thugge amemwondolea lawama gavana Waititu, bado kuna maswali mengi ambayo Wakenya wanajiuliza kuhusu kupotea kwa mabilioni ya pesa za umma.

La kustaajabisha zaidi ni kuwa Naibu Rais William Ruto alimtetea Waititu kwa kinywa kipana kuhusiana na jambo hilo.

Tume ya Kupambana na Ufisadi na DCI zapaswa kuchunguza madai haya kwa haraka sana na kuwashtaki watakaopatikana na makosa ya uporaji.

Huu ndio wakati wa kuwafunga jela mafisadi wote waliogeuza ofisi zao kuwa mifereji ya kurinia ushuru wa raia wachapa kazi.

Bila kukoleza chochote, Wakenya ni watu wenye bidii za mchwa, lakini bidii zao hugeuzwa sufi na kupeperushwa angani pasi na kuona matunda yake. Viongozi wachache waovu wanawaumiza kwa kweli.

Tusilojua ni kuwa mbegu hii ya ufisadi inapandikizwa kwenye akili za wadogo wetu na wataishi kujua kwamba ufisadi ndio damu na ubongo wa nchi yetu.

EACC na DCI zijifunge kibwebwe kuwakamata wahuni hawa. Tuungane sote kuuangamiza ufisadi, si ofisini, majumbani, shuleni, maabadini na hata maeneo ya umma.

Tulikabili donda ndugu hili kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Ni wakati mwafaka wa Wakenya kuona faida ya ushuru wao. Pesa zinazokopwa kila uchao kutoka China nazo zitumiwe kwa njia ya kumfaidi raia wa kawaida.

Ufisadi katika taifa la Kenya umetajwa kama janga la kitaifa, huku baadhi ya wizara mbalimbali zikipatikana kuhusika kwenye kesi za ufisadi, lakini uovu unaweza kuzimwa, sote tukijitolea kabisa.

Rais naye anafaa kukaza kamba dhidi ya mafisadi, bila kujali nafasi ya fisadi huyo serikalini. Anapaswa vilevile kutekeleza ahadi alizotoa kwamba afisa yeyote was serikali atakayetajwa katika kesi ya ufisadi na kupelekwa mahakamani utalazimika kuondoka serikalini. Anafaa kuzipa nguvu DCI na EACC katika shughuli hii.