• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
TAHARIRI: Harambee Stars iongezwe ufadhili

TAHARIRI: Harambee Stars iongezwe ufadhili

Na MHARIRI

MAFANIKIO ya kikosi cha kandanda cha Wazito yanatupa changamoto sisi Wakenya na hasa wenye nafasi zao katika jamii kuongeza hisani yetu katika makuzi ya mchezo huo humu nchini.

Klabu hiyo inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Nairobi kwa sasa inaongoza katika jedwali la timu zinazoshiriki ligi ya pili kwa hadhi nchini, almaarufu Super League, kwa jumla ya alama 72.

Ni dhahiri shahiri kuwa lau klabu hiyo haingekuwa imenunuliwa na bilionea mmoja kutoka Uswizi, Ricard Badoer, yakini haingekuwa katika nafasi hiyo nzuri inayoiweka katika upeo bora wa kukwezwa ngazi hadi katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu ujao.

Mafanikio ya Wazito ambayo iliteremshwa daraja msimu uliopita kutokana na matokeo mabovu na kuendelea kutatizika hata baada ya kushuka daraja kabla ya kununuliwa na mwinyi huyo, yanaashiria pengo lililopo katika maendeleo ya mchezo wa kandanda na pia michezo mingineyo humu nchini.

Pengo hilo ni ukosefu wa ufadhili.

Je, kwa nini pana ukosefu wa ufadhili Kenya?

Hatuna matajiri nchini ama ni kwa kukosa moyo wa kusaidiana wenyewe kwa wenyewe?

Ukweli ni kwamba Kenya imejaaliwa mashirika na watu binafsi wenye pesa tumbi nzima. Hivyo basi ni kutokana na kukosa moyo wa kusaidia ndiyo maana hamna ufadhili wa kutosha.

Sharti tubadili mwenendo huu kwani tuna jukumu la kuwasaidia wenzetu wasiobahatika katika jamii, hasa ikizingatiwa kuwa michezo ni sekta inayohusisha zaidi vijana. Kwa kuwekeza katika michezo, hivyo basi, tunawasaidia vijana kujikimu kimaisha.

Maadamu mafanikio ya michezo yamedhihirika kufikiwa hasa panapokuwa na ufadhili na udhamini wa kutosha, inakuwa bora kuiangalia kwa makini timu yetu ya taifa ya soka, Harambee Stars ambayo inajiandaa kushiriki fainali za Kombe la Afrika kuanzia Juni.

Harambee kwa sasa imetengewa Sh250 milioni pekee.

Pesa hizi hakika ni chache sana kwa timu inayotarajiwa kufanya makuu katika ngazi ya kimataifa.

Inapozingatiwa kwamba timu hii inaenda kukita kambi katika mataifa ng’ambo; Ufaransa hasa, maandalizi hayo yataigharimu kiasi kikubwa cha pesa, kulizo hizo ilizopewa.

Hivyo basi, pana uwezekano itakapoelekea kwenye fainali zenyewe nchini Misri, itakuwa imepungukiwa kwa kiasi kikubwa. Njia pekee ya kuzuia matokeo mabaya yanayotokana hasa na ukosefu wa pesa, basi ni wadhamini waanze kujitokeza kufadhili zaidi timu hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa mtaa wa Karagita walalama ‘nguvu za...

Shujaa yafufua matumaini ya kusalia Raga ya Dunia kwa...

adminleo