• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Mambo haya ni lazima kwa Stars

TAHARIRI: Mambo haya ni lazima kwa Stars

Na MHARIRI

HARAMBEE Stars inapojiandaa kushiriki kandanda ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kuanzia Juni pana mambo kadhaa ambayo kikosi hicho kinahitajika kuzingatia.

Kikosi hiki chafaa kufahamu kwamba mara hii mashabiki hawatarajii kushuhudia Kenya ikishiriki fainali hizi tu bali wanatazamia ushindi katika mechi nyingi iwezekanavyo ndipo kipige hatua ya maana kwenye fainali hizo za bara.

Inapokumbukwa kwamba Harambee Stars haijawahi kupiga hatua yoyote zaidi ya makundi katika fainali hizi ambazo imeshiriki mara tano, huu ni wakati muafaka kwa Kenya kuonyesha Afrika kuwa nayo imeinuka katika masuala ya soka.

Harambee yafaa ijue kuwa kandanda ya leo huwa haiwatambui miamba au wanyonge. Siku hizi wanyonge ndio wanaowika katika mengi ya mashindano ya kandanda huku wale waliojulikana kama majabari wakijiangukia ovyo.

Japo imepangwa pamoja na timu ngumu sana kama vile Senegal na Algeria, Kenya haifai kuogopa na badala yake icheze kwa ghera na ari kwa sababu hiyo pekee ndiyo njia tu ya kupata ufanisi.

Wala timu hiyo isiwadharau wanyonge Tanzania maana nao wako tayari kupigana kwa udi na uvumba hadi wafuzu kwa hatua za ziada.

Mbali na kujiamini, sharti timu iwe imejiandaa vyema inapoelekea katika kabumbu hii inayoanza Juni 21 na kushirikisha timu 24.

Kenya iliahidiwa kuandaliwa nchini Ufaransa kwa majuma kadhaa kabla ya fainali hizo kung’oa nanga nchini Misri. Ushauri wetu ni kwa serikali na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), kuhakikisha kuwa rasilmali zote zinazohitajika kwa maandalizi haya zimepewa timu hii ili isichelewe kuanza kujiandaa.

Punde ligi mbalimbali zinapoisha, kocha Sebastien Migne anahitajika kuwaleta pamoja wachezaji aliowateua ili waanze maandalizi ya mara moja. Ingekuwa bora zaidi iwapo timu hiyo pia ingepewa timu za hadhi kucheza nazo mechi za kujipima nguvu.

Naam hata timu zisizokuwa na majina makubwa ni muhimu katika matayarisho hayo, lakini timu kubwa zitaweza kuwaweka Harambee katika hadhi nzuri zaidi.

Mbali na hayo, ni jambo muhimu wanasoka wa kikosi hicho cha taifa wapewe marupurupu mazuri tena kwa wakati ufaao kama njia ya kuwatia motisha wanapoelekea nchini Misri kupeperusha bendera ya Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Magoha aonya Knut vikali kwa kupinga mtaala mpya

MWANAMKE MWELEDI: Ukoloni uliwasha moto wa uandishi

adminleo