• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
TAHARIRI: Ndoto ya Saba Saba iendelezwe nchini

TAHARIRI: Ndoto ya Saba Saba iendelezwe nchini

NA MHARIRI

KENYA Jumapili iliadhimisha miaka 29 ya Saba Saba ambayo huwa ni kila mwaka, Julai 7. Kwa miaka kadhaa sasa, siku hii haijakuwa ikivutia shamrashamra kutoka kwa viongozi wa upinzani na mashirika ya kijamii jinsi ilivyokuwa awali.

Tunatambua kwamba Kenya imepiga hatua kubwa kidemokrasia tangu enzi za utawala wa chama kimoja ambapo Saba Saba ilianza kuadhimishwa, lakini hii haimaanishi viongozi wa upinzani na wanaharakati wanastahili kulegeza kamba katika utetezi wa wanyonge.

Kimya kilichoshuhudiwa jana kilikuwa cha kutia hofu kwani ilionekana kama kwamba hakuna viongozi waliojitolea kwa ukakamavu kuendeleza ajenda ya upinzani inavyofaa.

Katika enzi za utawala wa chama kimoja cha Kanu, viongozi wa upinzani walikuwa na ari ya kupigania demokrasia ya vyama vingi.

Kwa msingi huu, walikuwa na ujasiri wa kukosoa kila aina ya maovu ya serikali iliyokuwa mamlakani licha ya vitisho, mauaji, kukamatwa na kufungwa bila hatia na hata kuteswa kizuizini.

Baada ya uongozi wa vyama vingi kupatikana, Saba Saba ilikuwa ingali ni siku muhimu iliyotumiwa kushinikiza mabadiliko ya mfumo wa uongozi ili kuwezesha uwazi, usawa na uadilifu kitaifa.

Ari ya mapambano haya ilianza kupungua wakati utawala wa Chama cha Kanu chini ya aliyekuwa rais Daniel arap Moi ulipoangushwa katika mwaka wa 2002, kisha baadaye Kenya ilipopata katiba mpya mwaka wa 2010.

Tangu hapo, kuna matukio mengi ambayo yameshuhudiwa yaliyofanya nguvu za upinzani na mashirika ya kijamii kufifia.

Kwanza, serikali ilifanikiwa kupitisha sheria kali ambazo zilitatiza shughuli za mashirika ya kijamii kwa kisingizio cha kudhibiti mashirika hayo yasitumiwe vibaya na maadui wa taifa.

Jambo jingine lililotokea ni kwamba viongozi wa upinzani katika enzi hizi wamekosa mwelekeo.

Wengi wao hawana uadilifu wa kisiasa kwani vitendo vyao vinadhihirisha ni watu wanaojali zaidi maslahi yao ya kibinafsi kuliko kutetea haki za umma ipasavyo.

Makundi haya mawili yanastahili kujihoji na kutafuta jinsi ya kuwapa Wakenya matumaini kwamba bado kuna viongozi wanaoweza kutegemewa kutetea haki za mnyonge.

You can share this post!

Adhani kapata mke kumbe kicheche

Uhuru aendelea kutua katika ngome kuu za Raila

adminleo