Makala

TAHARIRI: Polisi wazembe wasihamishwe

August 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

HATUA ya wasimamizi wa Idara ya Polisi kuwapa uhamisho maafisa wazembe na wale waliohusishwa na uhalifu haifai na inafaa kukomeshwa.

Kwenye tukio la hivi punde zaidi, maafisa wote wa ngazi za juu eneo la Pwani walihamishwa kutokana na kile kinachoaminika kushindwa kwao kukabiliana na uuzaji wa mihadarati katika eneo hilo.

Mara kwa mara, kumeripotiwa visa vya polisi wa ngazi za chini kunaswa mchana peupe wakishiriki katika uhalifu.

Wengine wamefumaniwa wakikodisha silaha zao kwa wahalifu, kisha baadaye, wakagawana mapato ya uhalifu huo.

Mojawapo ya mapendekezo muhimu kwenye Katiba ya 2010 ni mageuzi katika idara ya polisi. Tume Huru ya Huduma za Polisi ilibuniwa na ilitarajiwa kuongoza mchakato mzima wa mabadiliko katika kikosi hicho.

Hatuelewi iwapo ni hujuma kutoka kwa wasimamizi wa kikosi hicho au uzembe. Lakini kilicho wazi ni kwamba, kikosi hicho kimetekwa na maafisa walaghai, wazembe na katili ambao hawana ufahamu hata kidogo kuhusu haki msingi za raia.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i amedhihirisha uwezo wake wa kufanikisha mabadiliko katika sekta tofauti alikohudumu. Huu ndio wakati wa kufanyia kikosi cha polisi mabadiliko makubwa.

Inashangaza kwamba, afisa wa polisi aliyepatikana na makosa ya aina moja au nyingine, ama hupewa uhamisho hadi maeneo kame au kwa wale wa ngazi za juu, uhamishwa hadi stesheni nyingine.

Kimsingi, kile kinachoendelea hapa ni kuhamisha shida kutoka eneo moja hadi jingine. Polisi wahuni hawawezi kubadilika eti kwa sababu wamepewa uhamisho.

Tunachosema hapa ni kwamba, sawa na watumishi wengine wa umma, maafisa wa polisi ambao wameonyesha utepetevu kazini au wameonekana kushirikiana na wahalifu kuvunja sheria wanapasa kufutwa kazi na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Isitoshe, idara ya polisi wa trafiki ambayo kwa miaka mingi imeongoza kwa ulaji rushwa bado haijafanyiwa mageuzi hata kidogo.

Jaribio la Inspekta Mkuu mpya wa polisi Hillary Mutyambai kuondoa vizuizi vingi vya polisi barabarani yamkini lilihujumiwa na polisi wa ngazi za kadri. Vizuizi hivyo vimeongezeka katika maeneo mengi nchini katika siku za hivi majuzi.

Imekuwa ni biashara ya kuokota hongo kama kawaida. Wakati wa kufanyia kikosi hicho marekebisho makubwa, kama ilivyopendekeza katiba ni sasa.