TAHARIRI: Raia apunguziwe mzigo wa maisha
Na MHARIRI
RIPOTI kuwa gharama ya maisha imezidi kupanda humu nchini, inazidisha wasiwasi miongoni mwa wananchi kuwa huenda maisha yakawa magumu zaidi tunapoanza mwaka huu mpya.
Shirika la takwimu nchini (KNBS) zinaonyesha kuwa gharama ya maisha iliongezeka na kufika asilimia 5.82 mwezi uliokamilika Jumanne.
Ongezeko hili lilifanya maisha kuwa ghali zaidi ikilinganishwa na yalivyokuwa mwezi Novemba.
Takwimu hizo zinaonyesha kwama bei za mboga kwa mfano, zilizidi kupanda japokuwa mvua imekuwa ikiendelea kunyesha kote nchini. Katika masoko mengi, nyanya tatu ziliuzwa kwa Sh25 huku waliotaka nyanya moja wakilazimika kuinunua kwa Sh10.
Hali ilikuwa sawa na hivyo kwa wanunuzi wa Sukumawiki, vitunguu na hata unga wa mahindi.
Kupanda huku kwa gharama ya maisha kunajiri wakati ambapo Wakenya wengi wametumia pesa kwa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.
Tunapoanza mwaka huu wa 2020, yapo mambo ya lazima ambayo yatamlazimu kila mmoja wetu kuyatekeleza. La kwanza ni kodi ya nyumba kwa waliopangisha, ikifuatwa na karo katika shule za msingi za kibinafsi, shule za upili, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.
Hali hii ambapo kila mtu anakuwa na mzigo mzito wa gharama ya maisha, yafaa kuangaliwa upya na serikali. Kila mara kwenye hotuba zao, Rais na Naibu wake wamekuwa wakisisitiza kuwa uchumi wa nchi utakua kwa tarakimu mbili, kwa maana ya kuanzia asilimia kumi. Hali mashinani ni tofauti kabisa.
Sasa hivi kuna familia nyingi ambazo zililazimika kusalia mijini kwa kukosa nauli za kuzifikisha kwao mashambani, hata baada ya kufanya kazi kwa mwaka mzima.
Kuimarika kwa uchumi na kuwapunguzia wananchi gharama ya maisha ni jambo linalowezekana. Serikali inachohitaji kufanya, ni kuweka mikakati na miundomsingi ya kuwawezesha wakulima kukuza vyakula kwa bei nafuu.
Tayari wakazi wa maeneo ya Kaskazini Mashariki wanalia kuwa wamevamiwa na nzige. Japokuwa maeneo hayo hayajulikani kukuza vyakula kwa wingi, iwapo nzige hao watamaliza nyasi chache zilizoko, ng’ombe wa wafugaji watadhoofika na kutoa maziwa machache.
Badala ya kusherehekea Mwaka Mpya, maafisa wa wizara ya Kilimo wanapaswa kuwa mashinani wakikabiliana na wadudu hao hatari.