• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
TAHARIRI: Serikali inasinzia klabu zikitatizika

TAHARIRI: Serikali inasinzia klabu zikitatizika

Na MHARIRI

NI wakati mzuri kwa klabu zinazoshiriki kandanda ya kimataifa, sawia na Harambee Stars, ziwe zinatunzwa ifaavyo.

Mnamo Jumatano, Gor Mahia iliandaa harambee kwa dhamira ya kuchangisha pesa za kuiwezesha kushiriki mechi ya ufunguzi ya raundi ya pili ya soka ya Klabu Bingwa Afrika (CAF) hapo Jumapili ugenini Algeria.

Lakini matokeo ya mchango huo yalishangaza wengi pale Sh3,00,000 pekee zilipochangishwa.

Inapozingatiwa kuwa timu hiyo inafaa icheze mechi hiyo ya ugenini nchini Algeria dhidi ya USM Algiers, basi kuna hatari kubwa. Klabu hiyo inasema ililenga kuchangisha Sh3 milioni ambazo ndizo zinaitosha kwa mechi hiyo.

Kwa kawaida mchezo kama huu unapofanyika, klabu inayocheza ugenini huhitajika kuondoka nyumbani angaa siku tatu kabla ya mechi ndipo pakitokea mushkeli katika usafiri, timu iwe na nafasi ya kurekebisha mambo maadamu ni nadra sana CAF kupangua mechi yake timu inapopata matatizo madogomadogo kama ya usafiri.

Ikumbukwe kuwa Gor Mahia ilijipata katika matatizo kama hayo mwaka jana ilipocheza na RSB Berkane, Morocco ugenini; karibu wachezaji wakose kufika uwanjani kutokana na matatizo ya usafiri uliosababishwa na ukosefu wa pesa.

Hapa ndipo Serikali ya Kenya kupitia kwa Wizara ya Michezo, pamoja na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), walipofaa kupata funzo na kuanza kuyajali maslahi ya klabu zinazowakilisha taifa hili katika mashindano ya kimataifa.

Gor inapong’aa, ni taifa hili ndilo litakaloona fahari wala si Gor pekee.

Kwa wakati huu ni wazi kuwa klabu nyingi za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) hasa zinazotegemea ufadhili wa mashirika ya bahati-nasibu, zinatatizika sana kifedha kutokana na hali kwamba mdhamini mkuu wa michezo nchini, SportPesa, alisitisha udhamini wake mwezi jana kutokana na vuta nikuvute baina ya serikali na mashirika ya kamari.

Hiyo inamaanisha kuwa timu hizo sharti zitafute udhamini kutoka kwingineko.

Lakini kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayoikumba nchi hii, inakuwa vigumu sana timu kupata mdhamini mbadala.

Hapa jukumu linasalia mikononi mwa serikali. Huu ndio wakati mwafaka kwa Wizara ya Michezo kujitokeza na kufadhili timu kama Gor Mahia ili iweze kusafiri hadi Algeria kwa mechi hiyo muhimu ya bara. Vinginevyo itakuwa aibu kuu ikiwa timu hiyo itakosa usafiri au itatizike njiani.

  • Tags

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Kama kuzalisha ni raha, basi malezi yawe...

Mwili wa Cohen wapatikana shimoni nyumbani kwake Kitisuru

adminleo