TAHARIRI: Serikali yafaa iwe na uwazi kwenye bajeti
Na MHARIRI
HISIA tofauti zimetolewa tangu Alhamisi Waziri wa Fedha aliposoma taarifa ya makadirio ya matumizi ya pesa za serikali kwa mwaka 2019/2020.
Kwa kawaida, kuna waliofurahia bajeti hiyo na wale wanaoendelea kulalamika, hasa masikini ambao kulingana na wachanganuzi itawaathiri pakubwa na kufanya maisha yao kuwa magumu zaidi. Hii ni kawaida ya bajeti ya serikali; kuna wanaonufaika na wanaopoteza.
Hata hivyo, kinachosikitisha wanaharakati na wataalamu wa kisheria ni hatua ya bajeti kusomwa kabla ya mahitaji muhimu ya kisheria kuzingatiwa.
Kulingana na wanaharakati, bajeti haikufaa kusomwa kabla ya sheria ya ugavi wa mapato ya serikali kupitishwa na bunge.
Kwao, na ni kweli, hatua ya serikali ilikaidi agizo la mahakama kwamba bajeti haifai kutangulia sheria hiyo.
Huu bila shaka ni mtindo mbaya ambao wabunge wanaendeleza kwa kudharau mahakama.
Ni dharau kwa sababu serikali ilikuwa na muda wa kutosha wa kuwasilisha mswada huo ili wabunge wawe na muda wa kuujadili na kuupitisha kabla ya bajeti kusomwa.
Kuna sababu ya wanaharakati kuamini kwamba kuna kitu ambacho serikali inataka kuficha na ambacho kitawaathiri Wakenya wa kawaida.
Ikizingatiwa kuwa katika mswada huo serikali hueleza mbinu za kukusanya pesa za kufadhili miradi yake, Wakenya wana sababu ya kuhofia ongezeko la kodi.
Ni nini kingine kinachoweza kufanya serikali na bunge kukiuka agizo la mahakama ikijua bayana kwamba hatua hiyo itaweka mfano mbaya?
Kwa nini serikali ikakosa kuweka wazi mikakati yake ya kukusanya ushuru na kutangaza kwamba itafanya hivyo kwenye miswada ambayo imechelewesha kuwasilisha au imekwama bungeni?
Kuongezea Wakenya ushuru wa aina yoyote ile ni kuwadhulumu zaidi na yamkini, hawana budi kujiandaa kwa hali hiyo.
Mwanya
Kuna mwanya mkubwa katika bajeti na ni lazima serikali itafute pesa kwa vyovyote vile.
Hili ni jukumu la serikali na kwa maoni yetu hakuna shida iwapo pesa watakazotozwa zitatumiwa vyema kuimarisha maisha yao. Wasiwasi wetu ni kwamba, kuendelea kudharau maagizo ya mahakama kunaweka nchi pabaya.
Hata tunapojiandaa kwa hali ngumu ya maisha, tunataka kuona serikali ikijitendea haki ili tuamini kwamba itaweza kututendea haki kwa kutumia ushuru wetu kujenga nchi.