Makala

TAHARIRI: Sonko awajibikie uozo uliopo jijini

September 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MHARIRI

UONGOZI wa Jiji la Nairobi unafaa kulaumiwa kufuatia ongezeko la mikasa ya majengo kuporomoka.

Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko juzi alijitokeza na kukiri kwamba ufisadi uliosheheni katika idara ya uhakiki wa majengo jijini ndio umechangia katika kutokea kwa mikasa hiyo mara kwa mara.

Kulingana na Bw Sonko, maafisa katika serikali ya kaunti wamekuwa wakikiuka Sheria ya Ujenzi na Mpangilio wa Jiji kwa kuchukua hongo na kuidhinisha ujenzi wa majumba mabovu.

Alidai maafisa hao fisadi wamekuwa na mazoea ya kuzima mitambo ya kidijitali na kuidhinisha ujenzi wa majumba bila kufuata utaratibu ufaao.

Gavana alitoa malalamishi hayo kufuatia kifo cha wanafunzi saba walioangamia kufuatia kuporomoka kwa jengo la shule ya Precious Talents, Ngando, Nairobi.

Je, Gavana Sonko alichukua hatua ipi baada ya kubaini kwamba maafisa wake waliotwikwa jukumu la kuidhinisha majumba wanajihusisha na ufisadi huku wakihatarisha maisha ya watu? Gavana anataka wakazi wa Nairobi wamsaidie vipi kukabiliana na maafisa hao wafisadi?

Hiyo si mara ya kwanza kwa Bw Sonko kushutumu maafisa wa kuidhinisha majengo katika serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Alipokuwa akifariji waathiriwa wa mkasa wa moto katika eneo la Kabiro mtaani Kawangware, eneobunge la Dagoretti Kaskazini, miezi minne iliyopita, Bw Sonko pia alitoa malalamishi sawa na hayo.

Alionya kwamba serikali yake imeanza operesheni ya kukagua majengo yote kwa lengo la kuwanasa wamiliki wa majumba ambayo hayajaidhinishwa. Huo umekuwa wimbo wa Bw Sonko kila majumba yanapoporomoka na kusababisha maafa jijini Nairobi.

Hulka ya viongozi kujitokeza na kulalamika kila mara mikasa inapotokea ni ishara ya kushindwa na majukumu waliyopewa na wapigakura.

Ikiwa viongozi ambao wamepewa mamlaka na wananchi kupitisha maamuzi na kuchukua hatua kwa niaba yao, kazi yao ni kushutumu na kuwalimbikizia wengine lawama, wananchi wa kawaida wasio na mamlaka watafanya nini?

Wakati umewadia kwa viongozi kuwajibika na kukoma kuwanyooshea watu wengine kidole cha lawama.