Makala

TAHARIRI: Tutumie fursa hii kulainisha spoti

March 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MHARIRI

MASHIRIKISHO mbalimbali ya michezo yatumie fursa hii kujisaili na kutafakari upya kuhusu njia bora za kuboresha ukuaji wa spoti nchini.

Kutokana na virusi vya corona ambavyo vimeathiri takribani ulimwengu mzima, mashindano na hafla mbalimbali zimeahirishwa au kufutiliwa mbali kama mojawapo ya njia za kuzuia kuenea zaidi kwa janga hilo la kimataifa.

Kenya, kwa mantiki iyo hiyo, imeahirisha hafla zake pamoja na mashindano mbalimbali yakiwemo Ligi Kuu ya soka ya Kenya (KPL).

Kwa sasa hamna mchezo unaoendelea na hivyo pana wasaa mwingi wa viongozi na wadau wakuu wa fani mbalimbali za michezo kubaini penye udhaifu katika maendelezo ya michezo husika na hivyo kuutafutia suluhu.

Katika kandanda, kwa mfano, pamekuwapo na udhaifu mwingi unaohusiana hasa na fedha, udhamini na hata ufisadi miongoni mwa matatizo mengineyo.

Mashirikisho yanayohusika, kwa hivyo yanafaa kuanza kufikiria kuhusu jinsi ya kusuluhisha tatizo la kifedha ambalo linatishia kulemaza baadhi ya mashindano kama vile ligi kuu ya KPL na hata Super League. Hata baadhi ya timu zimeshajiondoa katika ligi hizi kutokana na uchochole.

Huu ni wakati mwafaka kwa FKF na timu zinazotatizika kuanza kuzungumza na mashirika ya kibiashara ili kuwezesha ufadhili.

Sharti wadau watafakari kuhusu kwa nini baadhi ya wadhamini wanajiondoa katika ufadhili wa michezo mbalimbali.

Tathmini ya haraka inatambua kuwa wadhamini wengi hujiondoa katika ufadhili wa klabu za Kenya kutokana na ubadhirifu au ufisadi.

Pesa zinazofaa kuzifaa klabu zimekuwa zikifyonzwa hasa na viongozi wa michezo mbalimbali.

Sharti wadau wakuu wajisaili, ni kwa njia ipi taifa hili linavyoweza kuangamiza uovu huu ili kuvutia mashirika fadhili.

Naam, twafahamu kwamba uchumi ni mbaya na hivyo basi mashirika mengi hayana hela ya kuzifadhili timu, ila hii haimaanishi kuwa hatuna mashirika nchini humu ambayo yanapata faida na ambayo yanaweza kudhamini michezo yetu.

Kimsingi, itakuwa bora kufikiria kwa kina pale tulipokosea ndipo mambo yetu yakaanza kutuendea mrama, ili tujirekebishe.