KAMAU: Wakati umefika kwa asasi husika kudhibiti wanablogu
Na WANDERI KAMAU
MOJA ya athari kuu za teknolojia mpya duniani ni kumwezesha kila mtu kutoa hisia zake kuhusu masuala mbalimbali yanayofanyika katika jamii bila kizingiti chochote.
Hili ni kupitia majukwaa yenye ufuasi mkubwa wa watu kama Facebook, Whatsapp na Twitter, ambapo watumizi wake huelezea hisia zao kwa njia huru bila mwingilio wa aina yoyote.
Hali hii ni kinyume na ilivyokuwa miaka ya awali, ambapo Kenya, kama sehemu nyinginezo duniani, ilikuwa na vyombo vichache sana vya habari ambavyo vilitoa nafasi kwa umma kueleza maoni kuhusu mwelekeo wa jamii.
Katika jamii nyingi, mamia ya watu waling’ang’ania nafasi chache zilizotolewa na vyombo hivyo.
Kizingiti kingine ni kwamba, vyombo vingi vilikuwa vinamilikiwa na serikali, hivyo raia hawakuwa na uhuru wowote wa kimawazo kujieleza.
Kutokana na ukuaji mkubwa wa teknolojia, kumeibuka kundi la watu maalum ambao si wanahabari wa kawaida waitwao “wanablogu.”
Majukumu yao yanafanana na yale ya wanahabari, kwani wengi wao huandika na kutangaza masuala mbalimbali yanayoendelea katika jamii kwenye nyanja za kisiasa na kiuchumi.
Wengi wameibukia kuwa maarufu sana, kiasi kwamba, wamekuwa wakitumiwa na viongozi wa kisiasa kama “watetezi” dhidi ya wakosoaji wao, hasa mitandaoni.
Ikizingatiwa wengi ni vijana wenye weledi mkubwa wa masuala ya teknolojia, wao hutumia njia zote kuhakikisha wameeleza ajenda na mikakati ya utendakazi wa viongozi hao.
Hata hivyo, mkasa mkuu kwenye “utendakazi” wao ni kwamba, huwa hawajali kanuni zozote za uandishi wa habari wala ukweli na athari za baadhi ya masuala wanayoyaandika.
Wengi huandika tu bora ziwe ni habari za “kuwasisimua” wafuasi ama waajiri wao.
Ni kwenye harakati hizi ambapo wengi wamewaharibia sifa watu maarufu kwa kuandika kila aina ya tuhuma dhidi yao bila kubaini ukweli wake.
Watu maarufu wamehusishwa na sakata za ufisadi, mahusiano ya kimapenzi, ulanguzi wa mihadarati kati ya maovu mengine.
Cha kushangaza ni kuwa, katika nyanja kama siasa, wengi hutumiwa na wanasiasa kuwaharibia sifa washindani wao.
Ni mtindo unaozidi kushika kasi nchini, kwani Kenya ni miongoni mwa mataifa yenye mpenyo mkubwa wa intaneti Afrika.
Mtindo huo ndio umezifanya nchi kama Tanzania, Uganda, Eritrea kati ya zingine kuweka sheria kali kuwadhibiti na kuwaadhibu ikiwa watapatikana wakizikiuka.
Huu ndio wakati mwafaka wa kudhibiti baadhi ya wanablogu hawa.