• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Tanzania yapiga hatua ndege zikitengenezewa nchini humo

Tanzania yapiga hatua ndege zikitengenezewa nchini humo

THE CITIZEN Na WANDERI KAMAU

TANZANIA imepiga hatua mpya katika sekta ya uchukuzi wa ndege, kufuatia kutengenezwa kwa ndege tatu mpya katika kituo cha kiufundi cha Uwanja wa Kikanda wa Ndege wa Morogoro.

Kituo hicho, kilichozinduliwa mnamo 2021 na kampuni ya Airplane Africa Limited (AAL) kutoka Jamhuri ya Czech, ndicho cha kwanza kutengeneza ndege barani Afrika.

Ndege hizo aina ya Skyleader zina uwezo wa kuwabeba abiria wawili.

“Kutengenezwa kwa ndege hizo kunaashiria mafanikio makubwa,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege nchini Tanzania (TAA), Moussa Mbura, kwenye kikao na wanahabari mnamo Jumatatu.

“Uwekezaji huu wa AAL unabuni nafasi za ajira zaidi kwa raia wa Tanzania,” akaongeza.

Mafanikio hayo makubwa yanajiri wiki chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan wa taifa hilo kutoa maagizo kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuanza majaribio ya treni ya umeme inayotumia Reli ya Kisasa (SGR).

Tanzania ilijenga reli hiyo ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

Rais Suluhu alisema kuwa kufikia Julai 2024, Tanzania inafaa kuwa imeanza huduma za uchukuzi kutumia treni ya umeme.

Taifa hilo limekuwa likiahirisha uzinduzi wa huduma za uchukuzi wa aina hiyo ya kisasa kabisa katika kanda hii tangu Aprili 2017.

Wadau wanasema majaribio hayo yanaashiria hatua kubwa sana katika ukuaji wa sekta ya uchukuzi nchini Tanzania.

Treni itakayokuwa ikitumika imetajwa kuwa ya kipekee, kwani itakuwa ikisafiri kwa mwendo wa hadi kilomita 160 kwa saa moja.

Huku Tanzania ikiendelea kupata mafanikio makubwa katika sekta ya uchukuzi, hali ni tofauti nchini Kenya, kwani watu wengi wamekuwa wakilalamikia miundomsingi duni, hasa katika viwanja vya ndege.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), abiria wengi wamekuwa wakilalamikia kunyeshewa, licha ya serikali kutangaza kufanya ukarabati.

Uwanja huo pia umekuwa ukikumbwa na matatizo ya umeme kupotea mara kwa mara.

Mwezi Februari, mwanahabari Larry Madowo alisema kuwa ni kinaya uwanja huo unakumbwa na matatizo chungu nzima ya kimiundomsingi licha ya hatua zilizowekwa na serikali kuboresha hali yake.

“Inashangaza kuwa huu ni miongoni mwa viwanja vikubwa zaidi vya ndege katika ukanda huu,” akasema Bw Madowo.

Katika uchukuzi wa reli, reli ya kisasa nchini Kenya baina ya Nairobi ya Mombasa imetajwa ya kiwango cha chini, ikilinganishwa na reli za kisasa zilizotengenezwa nchini Tanzania na Ethiopia mtawalia.

“Maana halisi ya reli ya kisasa ni kuwa treni inafaa kutumia umeme badala ya dizeli. Reli hizo ndizo zilizo katika mataifa kama China, Amerika, Korea Kusini kati ya mengine. Hivyo, ukweli ni kuwa, Tanzania na Ethiopia zimepiga hatua kubwa sana ikilinganishwa na Kenya,” asema Bw Gerrison Muthama, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchukuzi.

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki wa Shabana FC wamlilia Mungu asaidie isishushwe...

Mwanahabari Rita Tinina aliaga dunia kutokana na nimonia...

T L