Taratibu za kupanda uyoga
KUANZIA maandalizi hadi mavuno, uyoga huchukua karibu siku 42.
Dennis Macharia amekumbatia teknolojia ya Synthetic, anayoipigia upatu akisema imepunguza siku za maandalizi ya mbegu kutoka 30 hadi 15.
Aidha, hutumia matawi ya ngano, anayotoa Narok, yanachanganywa na mbolea ya kuku, mbegu za pamba, na gypsum, shughuli inayochukua siku tisa.
“Nina vyumba viwili maalum vya kuunda substrate ya uyoga,” Macharia anasema.
Vilevile, vipandio hivyo huwekwa udongo anaotoa msitu wa Kijabe.
Kinachofuata, ni mchanganyiko huo kuwekwa kwenye chumba cha kiwango cha juu cha joto (pasteurization unit), muda wa siku saba.
“Husaidia kuangamiza viini, vimelea na Pathojeni zozote zilizomo,” anaelezea Eric Makhuyi, Meneja wa Mikakati Garden Mushrooms.
Mchanganyiko wa vipandio hivyo unawekwa kwenye mifuko maalum kisha inatiwa mbegu (spawns), na kupelekwa katika vyumba vya kukuzia uyoga, na Makhuyi anasema siku 21 daadaye huanza kuvuna.
Vyumba vya upanzi, vina mitambo ya kisasa kufuatilia utendakazi, kusawazisha hewa na joto.
Macharia hukuza aina ya white button Mushroom, na kutambua iwapo zao ni tayari kuvunwa kofia ya uyoga inapaswa kuwa ngumu – isiyovunjika upesi inapofinywa kiasi.
Isitoshe, kofia iwe na kipenyo (diameter) cha karibu sentimita tatu au nne.