• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
TEKNOHAMA: Facebook kuondoa ‘like’ kupunguza msongo akilini

TEKNOHAMA: Facebook kuondoa ‘like’ kupunguza msongo akilini

Na LEONARD ONYANGO

HIVI majuzi jamaa fulani aliacha kutumia Facebook kutokana na kigezo kwamba hakuna mtu anayependa (Like) picha zake licha ya akaunti yake kuwa na wafuasi 3,000.

Jamaa huyo ni miongoni mwa maelfu ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wamejipata wapweke na msongo wa mawazo kwa kukosa ‘Like’.

Sasa mtandao wa Facebook umetangaza kuficha alama ya ‘Like’ ili kunusuru watu dhidi ya kupatwa na msongo wa mawazo ambao husababisha wengi kujitoa uhai.

Baadhi ya watumiaji wa Facebook sasa hawataweza kujua idadi ya watu wanaopenda picha zao au kutazama video zao walizopakia katika mtandao huo.

Jaribio la kuondoa ‘Like’ limeanzia nchini Australia. Mtandao wa Instagram ambao hutumiwa kwa wingi kupakia picha, pia umeanza majaribio ya kuondoa ‘Like’.

Mkurugenzi wa Facebook nchini Australia, Mia Garlick alisema mtandao huo unafanya majaribio baada ya kubaini kwamba ukosefu wa ‘Likes’ umewafanya watumiaji wengi kuhisi wapweke na hata kufikiria kujitoa uhai.

“Hatua hiyo imepongezwa sana na makundi ya kulinda afya ya ubongo,” akasema Garlick.

“Mtumiaji wa Facebook hatajua ni watu wangapi wamependa alichokiandika au picha. Hiyo itasaidia kupunguza msongo wa mawazo,” akaongezea.

Alisema watu wanafaa kuzungumzia masuala muhimu badala ya kushindana kupata ‘likes’.

Kulingana na Garlick, majaribio hayo yatafanyika katika nchi nyingine kama vile Australia, Canada, Brazil, New Zealand, Japan, Italia na Ireland.

Tafiti ambazo zimewahi kufanywa zimehusisha matumizi ya mitandao ya kijamii na matatizo ya kiafya kama vile msongo wa mawazo, kuhisi upweke, kuonekana mtu asiye na hadhi na mwenye wivu.

Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa katika jarida la Journal of Social and Clinical Psychology ulisema kuwa idadi ya ‘likes’ husababisha mtu kujilinganisha na mwenzake hivyo kuleta matatizo yanayoathiri afya ya ubongo.

“Mtandao wa Facebook hausababishi msongo wa mawazo. Kinacholeta matatizo ya akili ni watumiaji kuanza kujilinganisha na wenzao kwa kutumia ‘likes’,” wakasema watafiti hao wa Chuo Kikuu cha Houston, Amerika.

Mbali na watu wazima, watafiti pia wanasema kuwa mitandao ya kijamii inaathiri afya ya watoto; hasa wa kike.

Utafiti

Utafiti uliochapishwa katika jarida la The Lancet Child & Adolescent Health miezi miwili iliyopita, ulihusisha wasichana 10,000 wa kati ya umri wa miaka 13 na 16 nchini Uingereza.

Watafiti walibaini kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuathiri afya ya wasichana kutokana na matusi na kuzomewa mitandaoni.

Walisema mitandao ya kijamii inaweza kusababisha watoto kutopata usingizi na kukosa muda wa kufanya mazoezi ya viungo.

“Mitandao ya kijamii haina madhara, lakini inasababisha watoto kupoteza muda mwingi badala ya kufanya shughuli zinazoboresha afya ya ubongo kama vile mazoezi na michezo,” wakasema watafiti hao.

Wataalamu wanashauri watu kutumia muda mfupi mno katika mitandao ya kijamii ili kuepuka kuwa na msongo wa mawazo.

Tumia muda mwingi kuzungumza na watu walio karibu nawe badala ya kuzama kwenye mitandao ya kijamii. Fanya mazoezi ya viungo na shughuli nyinginezo zinazoimarisha afya ya ubongo.

You can share this post!

MAZINGIRA NA SAYANSI: Umuhimu wa nyuki kwa chakula na...

KUMLINDA MTOTO: Watoto kujiua, suala la malezi au mtindo wa...

adminleo