TEKNOHAMA: WiFi inachujisha mbegu za kiume
Na LEONARD ONYANGO
ONGEZEKO la wanaume walio na mbegu hafifu za kiume limezua wasiwasi miongoni mwa watafiti wa masuala ya afya ya uzazi huku baadhi ya wanasayansi wakihofia kuwa huenda dunia ikakosa watu katika karne chache zijazo.
Wanasayansi wanasema kuwa idadi ya wanaume walio na mbegu dhaifu imeongezeka kwa asilimia 40 sasa ikilinganishwa na miaka 50 iliyopita.
Wanaume walio na mbegu hafifu wanashindwa kutungisha mimba.
Unene kupita kiasi, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, shinikizo la damu na kuketi chini kwa muda mrefu ni miongoni mwa mambo ambayo yanasababisha wanaume kuwa na mbegu dhaifu.
Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Bispebjerg Frederiksberg nchini Denmark, ulibaini kuwa watoto ambao baba zao wanavuta sigara pia huwa na mbegu duni za kiume wanapokuwa watu wazima.
Watafiti hao walichunguza vijana 778 wa umri wa miaka 19 kwa kuwauliza ikiwa mmoja wa wazazi wao alikuwa akivuta sigara.
Waligundua kuwa vijana ambao wazazi wao walikuwa wakivuta sigara kila siku walikuwa na mbegu za kiume chache kwa asilimia 10.
Mbali na sigara, matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Western, Australia, yaliyotolewa Mei, mwaka huu, yalionyesha kuwa hisia za mama mjamizito zinaweza kuathiri mtoto aliye tumboni.
Kulingana na watafiti hao, mwanamke anayekuwa na mzongo wa mawazo mara kwa mara wakati wa ujauzito, atajifungua mtoto mwenye mbegu za kiume hafifu atakapokuwa mtu mzima.
Watafiti wanasema wiki za kwanza 18, mama mjamzito hafai kuwa na mzongo wa mawazo.
Watafiti hao walichunguza vijana 623 wa umri wa miaka 20 wakati wa utafiti huo.
Wengi wa wanawake hao wajawazito ni wale walikuwa wakikumbwa na masaibu kama vile kumpoteza mtu wa familia, matatizo ya ndoa na ukosefu wa hela.
Vijana ambao mama zao walipatwa na masaibu zaidi ya mara tatu walikuwa na upungufu wa mbegu za kiume kwa asilimia 36.
Wanaume ambao mama zao walikuwa na mzongo wa mawazo chini ya mara tatu walikuwa na upungufu wa mbegu za kiume kwa asilimia 11.
Tafiti mbalimbali pia zinaonyesha kuwa kuweka simu kwenye mfuko karibu na sehemu za siri kwa muda mrefu pia ni hatari kwa mbegu za kiume.
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Technion cha nchini Israeli, walibaini kuwa simu huharibu mbegu za kiume kwa zaidi ya asilimia 47.
Mtafiti aliyeongoza utafiti huo Profesa Martha Dirnfeld, alisema kuwa simu inatoa joto ambalo huathiri mbegu za kiume.
Watafiti hao walichunguza wanaume 100 waliokuwa wakisaka matibabu ili kusaidiwa kuwa na mbegu za kutosha kutungisha mimba.
Watafiti hao walibaini kwamba wanaume waliokuwa wakitembea na simu zao mfukoni au kulala karibu na simu zao usiku bila kuzima, walikuwa na mbegu hafifu.
Utafiti wabainisha
Utafiti wa hivi karibuni ambao huenda ukawatia hofu wanaume ni ule uliofanywa na wanasayansi nchini Japan uliosema kuwa mtandao wa WiFi unaharibu kwa kiasi kikubwa mbegu za kiume.
Utafiti huo uliofanywa kati ya Agosti na Novemba 2018 ulihusisha wanaume 51.
Wanaume hao walitolewa mbegu za kiume kwa njia ya kiteknolojia na kuzigawa katika sampuli tatu.
Sampuli moja iliwekwa karibu na kifaa cha kutoa intaneti ya WiFi, sampuli nyingine iliwekwa mbali kidogo na kifaa hicho na nyingine iliwekwa katika eneo lisilokuwa na WiFi. Baada ya masaa 24, mbegu hizo zilipimwa.
Watafiti walibaini kuwa asilimia 23 ya mbegu zilizowekwa karibu na chanzo cha intaneti ya WiFi zilikufa ikilinganishwa na asilimia nane ya mbegu zilizowekwa eneo lisiokuwa na WiFi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linatabiri kwamba tatizo la wanaume kuwa na mbegu hafifu ndilo huenda likawa kubwa zaidi baada ya ugonjwa wa kansa na maradhi ya moyo katika kipindi cha miaka michache ijayo.
Wataalamu wanapendekeza ndizi na kitunguu saumu kama vyakula muhimu vinavyosaidia kuimarisha mbegu za kiume.