Tuambizane: Ukipuuza matatizo katika ndoa na uhusiano, mambo yataharibika
KATIKA mahusiano ya mapenzi na ndoa, matatizo huwa yanaibuka na kama haujawahi kuyapata, subiri, yatakuja. Wanachofanya watu wengi ni kupuuza matatizo badala ya kuchukua hatua za kuyasuhuhisha kwa haraka.
Unapoyapuuza masuala yakizuka katika uhusiano wako wa kimapenzi, huwa unayaongezea mbolea yapate nguvu na kunawiri na hatimaye kuharibu ndoa yako na kwa kiwango kikumbwa maisha yako ya kimapenzi.
“Kupuuza masuala yanapozuka katika uhusiano wako wa kimapenzi ni hatari sana. Ni sawa na kufunika mbegu ya mumea wenye sumu mchangani na kuongezea mbolea. Inamea na kuwa na nguvu, kuchanua maua, kutoa mbegu zaidi na hatimaye kuharibu mazingira unayoishi,” asema mwanasaikolojia Kenan Kamau, mtaalamu wa masuala ya mahusiano.
Anasema watu wanaopuuza matatizo yakianza kutokea katika uhusiano wa kimapenzi huwa wanaalika balaa. “ Kupuuza kunayafanya kuzaa matatizo au hatari mpya pia,” asema.
Kulingana na Kamau, watu wanafaa kuwa chonjo kwa matatizo ya wapenzi wao na kuwasaidia kukabiliana nayo. “ Hapa sizungumzii matatizo ya kifedha ambayo watu wengi hupatia kipaumbele.
Nazungumzia matatizo ya kimaisha, kikazi, kihisia, kiakili na yanayohusiana na maslahi ya mtu binafsi.
Ukiwa katika uhusiano wa dhati wa kimapenzi, utatambua mwenzako akipitia hali ngumu kimawazo hata kama hatakufahamisha,” alisema. Palipo na penzi la dhati, huwa kuna mawasiliano mazuri yanayoweza kufanikisha utatuzi wa matatizo kabla hayajakomaa na kuwa balaa.
Usipowasiliana na mwenzi wako, asema Grace Mawia, mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya mahusiano ya kimapenzi, utajenga chuki kwa mwenzi wako.
Mawia anasema chanzo kikubwa cha balaa katika mahusiano ya kimapenzi ni wahusika kutokuwa na nia moja. “Watu wasipokuwa na nia moja katika uhusiano, hawawezi kutambua matatizo yakizuka na hakuna anayejali yanayompata mwenzake.
Hali ikiwa hii, kila suala huwa linapuuzwa na kwa kufanya hivi linabadilika kuwa balaa kwa wahusika wote,” asema Mawia.
Wataalamu wanasema kwamba makosa makubwa zaidi ni mtu kujitetea binafsi, badala ya kushughulikia tatizo likizuka. “ Kwa kufanya hivi, hakuna suala linaweza kutatuliwa na huwa unamtenga mwenzi wako. Jifunze kutenganisha tatizo, na mwenzi wako.
Kwa mfano, ikiwa suala ni mwenzi wako kuchelewa kufika nyumbani au anatumia simu sana na kukunyima muda unaohitaji, hilo ni suala, lakini mwenzi anafaa kubaki kuwa maalum kwako,” asema.
Mawia anaongeza kuwa njia nzuri ya kusuluhisha masuala ya mahusiano ya kimapenzi ni kila mmoja kusikiliza mtazamo wa mwenzi wake.
“Acha mwenzi wako amwage yaliyo katika moyo wake. Mwaga yaliyo katika moyo wako. Kuweni wangwana. Kumbuka, lengo ni kutafuta suluhu si kuthibitisha ni nani aliye sahihi au mbaya,” asema.