Makala

Tulioshwa maelfu ya pesa kwa ahadi ya kuanzishiwa biashara

February 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MERCY KOSKEI

NOVEMBA mwaka jana, Cynthia* alipatana na ujumbe kwa WhatsApp (status) ya rafikiye uliokua ukitangaza biashara ya kuuza virutubisho vya afya.

Cynthia alivutiwa na ujumbe huo na baada ya kuzungumza na rafikiye alimshauri atembelee afisi ya kampuni hiyo jijini Nakuru.

Kwenye afisi hiyo alitambulishwa kwa mshauri aliyedai kuwa kampuni hiyo imeipa kipaumbele afya, utajiri na mtindo wa maisha huku akitaja manufaa ya virutubisho hivyo.

Mshauri huyo alisisitiza kuwa virubitisho hivyo vilikua na nguvu ya kuzuia magonjwa na kumfahamisha kuwa angepata faida ya kifedha kati ya Sh4,800 hadi Sh,6,000 iwapo angeleta wateja wapya.

Habari hiyo ilimpa Cynthia furaha, kwani alijua kuwa angeboresha afya na vilevile kupata pesa na kuishia kujiunga na mradi huo, akichagua kifurushi cha bei ya Sh42,000.

“Katika ofisi, mshauri alichora piramidi ya jinsi mpango huo ulivyofanya kazi na umuhimu wa virutubisho hivyo, walinieleza kuwa vinazuia maradhi kama saratani, arthritis na mengine ambayo ni ghali kutibu. Nilielezwa kuwa kampuni hiyo ilikua geni mjini Nakuru na kuwa wakazi wengi walikuwa wakijiunga. Nilijua kuwa ingenufaisha jamii yangu,” Cynthia alieleza Taifa Leo.

Hata hivyo, Cynthia alitakiwa kulipa pesa hizo kabla ya kupokea virutubisho vyake ndani ya wiki moja. Alikumbwa na changamoto ya kifedha.

Baada ya wiki moja, alifanikiwa kukusanya pesa kupitia akiba na michango kutoka kwa marafiki, na kukamilisha malipo.

Matarajio yake yaligeuka kuwa ya kukatishwa tamaa kwani ‘kampuni’ hiyo iliendelea kumnyima virutubisho alivyoahidiwa, likitaja umuhimu wa kuongeza wateja zaidi.

Cynthia alijaribu kuwasiliana na kampuni hiyo, lakini maswali yake hayakujibiwa, na mwishowe akapoteza pesa zake.

 “Nilipewa risiti baada ya kulipa, nambari yangu ilikua inakaribia 750, maana waliokuwa mbele yangu pia walipitia hali hiyo hiyo. Kwa miezi mitatu sasa nimejaribu kuwafikia ili walipe pesa zangu lakini sijafaulu. Natumai pamoja na waathiriwa wengine tutazipata,” alisema.

Mwathiriwa mwingine, Sharon, alijipata katika hali hiyo baada ya kushawishiwa na jirani yake, ambaye alimuahidi mapato makubwa baada ya kuwaelekeza wateja wapya.

Kwa tamaa ya kupokea faida kubwa, Sharon alichagua kifurushi cha bei ya juu zaidi, na kupelekea kuchukua mkopo ili kuagiza virutubisho vingi.

Hata hivyo, alipoteza zaidi ya Sh100,000 baada ya kampuni hiyo kumkwepa.

“Nilichagua kiwango cha juu zaidi, nilitamani sana virutubisho ili viwafaidi wazazi wangu kule kijijini, sikujua kuwa walitaka pesa zangu, walinufaika na pesa zetu. Walipokea mamilioni,” alisimulia.

Kennedy Mugo alilengwa na mpango huo wa udanganyifu alipopokea mwaliko kwa kile alichoamini kuwa ni mkutano uliopangwa kujadili masuala ya afya na uwezeshaji wa kifedha.

Mwaliko huo ulionekana kuwa rasmi kutoka kwa maafisa wa Kaunti ya Nakuru.

“Tunafuraha kukujulisha kuwa umechaguliwa kuhudhuria warsha ya uwezeshaji wa kifedha na afya tarehe 10 Februari. Manufaa ikiwa pesa za kuanzisha biashara, kujiandikisha katika mpango wa makazi na huduma za afya ya Serikali ya Kitaifa, elimu bora ikiwa ni pamoja na kusafiri nje ya nchi kwa masomo zaidi na safari na likizo ulimwenguni kote,” ulisoma ujumbe huo.

Hata hivyo, alipohudhuria mkutano huo, alipigwa na butwa baada ya kukosa maafisa kutoka serikali ya Kaunti na ile Kitaifa.

Badala ya majadiliano kuhusu afya na uwezeshaji wa kifedha, kampuni hiyo ilianza kuuza sera ya vifurushi.

“Nilitulia tu na kuketi. Wawakilishi wa kampuni hiyo walitufunza kinyume na mada ilivyoratibiwa. Walianza kuuza vifurushi vyao. Tulijaribu kuuliza maswali lakini tulinyimwa nafasi badala yake walitutaka tuchague wawakilishi ambao wangetuletea majibu baadaye,” alisema.

“Wanatumia ukosefu wa ajira nchini kulaghai watu. Wengine hata walilipa pesa ili kujumuishwa kwenye orodha. Watu wanapaswa kuwa waangalifu na wajue hakuna cha bure,” aliongeza.

Kamanda wa Polisi wa Nakuru, Samuel Ndanyi amewataka wale ambao wamenaswa na matapeli hao kupiga ripoti ili uchunguzi kuanzishwa.

“Tutaweza kuanzisha upelelezi mara tu watakapopiga ripoti suala hilo. Watu wawe makini na wasitoe pesa pale wanapoahidiwa biashara,” alisema.