TUNAWEZA: Mtindio wa ubongo haukuzima ndoto yake
Na PAULINE ONGAJI
HAJAACHA ulemavu umzuie kutimiza ndoto yake kama mwimbaji, mwandishi, mwanamitindo, mshawishi wa mauzo kwenye mitandao ya kijamii na mhisani.
Huo muhtasari wa maisha yake Bw Rahul Bhavan, 34, msanii ambaye licha ya kukumbwa na mtindio wa ubongo – cerebral palsy- hali ambayo inamlazimu kutumia kiti cha magurudumu na kupooza kwa mikono yake – hajaacha hali hii izime ari yake ya kung’aa katika nyanja tofauti anazohusika nazo.
Kama mwanamitindo, Bw Rahul anajivunia kufanyia kazi mojawapo ya wasanifu mavazi watajika wa mavazi ya kihindi nchini. “Nimefanyia kazi msanifu mavazi Shenu Hoonda,” asema.
Kama mwanamuziki, Bw Rahul tayari ana nyimbo mbili. “Wimbo wangu wa kwanza ni Sai meri jaan, wimbo unaomshukuru Mungu kwa hatua ambazo amenisaidia kupiga maishani. Kibao changu cha pili Tanha Hoon main yaara, ni cha mapenzi ambapo nimeimba kwa ushirikiano na mwanamuziki Faisal kutoka nchini Pakistan,” aongeza.
Kama mwandishi, Bw Rahul ameandika na kuzindua kitabu chake cha kwanza ‘Romantic Thoughts’, kinachojumuisha nukuu 80 za mapenzi, zilizochanganywa na picha za wanamitindo tofauti wa fashoni.
Aidha, Bw Rahul amejiundia jina katika ulimwengu wa kutumia mtandao kufanya mauzo, ambapo anajivunia kutoa huduma zake kwa filamu, nyimbo na hata mashindano ya urembo.
“Nimemfanyia mauzo produsa na mwanafilamu Nameeta Jamal kupitia filamu yake ‘Unprotected’. Aidha, nimehusika katika shindano la urembo la Miss India, makala ya Kenya, tangu mwaka wa 2016,” aeleza.
Lakini mbali na sifa hizo, anasema hakuna jambo linalompa raha kama kuhusika katika kazi ya uhisani.
Kila mwezi, amekuwa akikusanya rasilimali ili kuwalisha zaidi ya watoto 150.
“Nilianza shughuli hii Machi 2016, lakini kwa sababu ya janga la maradhi ya Covid 19, nililazimika kuhairisha kazi hii hadi angaa mwezi Januari mwaka ujao,” aongeza.
Kulingana na Bw Rahul, licha ya changamoto ya kimaumbile, wazazi wake walimlea sawa na watoto wengine wa kawaida.
“Pindi nilipotimu umri wa ujana, walianza kunifunza kuhusu maisha na hasa jinsi ya kuwa huru. Kila mara waliniambia kwamba hawatakuwa nami na hivyo nilihitaji kujisimamia na kukabiliana na changamoto za maisha kivyangu,” aeleza.
Lakini mambo hayajakuwa rahisi kwani amekumbana na changamoto mbalimbali, huku tatizo kuu likiwa kudhihirisha uwezo wake licha ya ulemavu unaomkabili.
“Wakati mwingine, licha ya bidii yangu, kuna baadhi ya watu ambao bado wanatumia ulemavu wangu kama mizani ya kupima uwezo wangu,” asema.
Ombi lake ni kwa jamii kuelewa kwamba walemavu pia wana uwezo wa kujiimarisha kimaisha, hisia, ndoto na moyo unaopenda.
Ndoto yake ni kuendelea na kazi yake kama mwanamitindo ambapo anataka kudhihirisha kwamba kutumia kiti cha magurudumu sio mwisho wa maisha.