Makala

Tuongee Kiume: Kelele huyeyusha gundi inayounganisha wapenzi

Na BENSON MATHEKA September 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

EPUKA kumpigia kelele mwanadada  mpenzi wako. Naam, kumpigia kelele demu anayekupenda ni kumdhulumu.

Hii haimaanishi kuwa hamfai kutofautiana. Kutofautiana ni kawaida katika uhusiano wa kimapenzi lakini kupigiana kelele ni sumu. Ukimpigia kelele demu wako, unaharibu gundi inayowaunganisha. Wapenzi hawafai kupigiana kelele, wanazungumza kama marafiki.

Demu anapopenda mwanamume kwa dhati, huwa anajitoa kikamilifu kwa mtu wake. Huwa anatoa moyo na roho yake kwa mwanamume wa ndoto yake. Hata hivyo, wengi huwa wanajuta kwa kupata wanaume wanaowapenda huwa wanachukulia kujitolea kwao kwa mzaha.

Kwa hivyo kaka, epushia mwanadada anayekupenda kwa dhati masononeko. Baadhi ya wanaume huwa wanawakosea mademu wanaowapenda kwa dhati kwa kutojua na wengine huwa wanafanya hivyo makusudi.

Kuvunja moyo mwanadada anayejitoa kwako kunamuumiza zaidi ya unavyoweza kufikiria. Kunamuathiri kihisia, kunamfanya achukie mapenzi na kunaweza kuathiri mahusiano yake ya baadaye.

“Kumbuka mapenzi hayafai kuwa ya kuumizana. Mapenzi yanapaswa kuponya moyo, kuwa kimbilio la mtu kwa kuwa na mwenzi wa kumsaidia kubeba mazito ya maisha na kufanya maisha kuwa na maana.

Hata hivyo, wanaume wengi huwa wanafanya maisha ya mademu wanaowapenda kuwa jehanamu,” asema Mercy Masibo, mwanasaikolojia na mtaalamu wa mahusiano ya mapenzi.

Anasema hali hii ya kuvunjwa moyo inatokana na wanaume kujifanya wanapenda vipusa.

“Iwapo haumpendi kwa dhati, mwambie tu na uache kumharibia wakati, ni heri ajue haumpendi kuliko kujifanya unampenda,” aongeza Masibo.

Mbaya zaidi, aeleza, ni mwanamume kumwambia mwanamke aliyetoa moyo wake kwake kwamba hana sura nzuri.

Mary Kimani, mtaalamu wa mahusiano anakubaliana na hili akisema kitu kichungu zaidi ambacho mwanamume anaweza kuambia  mwanamke yeyote anayempa moyo wake kwake ni kwamba ana sura mbaya.

“Kila  mwanamke ana urembo wake wa kipekee. Kumwambia mwanadada aliyechagua kukupenda kuwa hana sura au umbo la kuvutia ni kumdunga mkuki moyoni,” asema Kimani na kuongeza kuwa wanaume katili huwa wanatumia maneno haya kudhalilisha vipusa wakichoka nao au kuwafanya wajichukie.

Wanaume huwa wanawaumiza vipusa wapenzi wao kwa kuwafananisha na vimwana wao wa zamani.

Kimani anasema mwanaume akifanya hivyo huwa anaalika janga.

“Kamwe usimfanye mpenzi wake ahisi kuwa hafikii kiwango cha mtu wako wa zamani. Unapaswa kumpenda alivyo na bila masharti na ni jukumu lako kumfanya kuwa bora. Usiwahi kufananisha demu wako na mpenzi wako wa zamani,” asema Kimani.