UBUNIFU: Mwanafunzi abadilishaye taka kuwa bidhaa za thamani
Na PETER CHANGTOEK
BAADHI ya watu aghalabu hawaoni thamani yoyote iliyopo katika taka kama vile chupa za plastiki zilizotupwa na zile za glasi.
Lakini kwa mwanafunzi mmoja wa chuo cha anuwai, takataka hizo ambazo huwa hazina thamani kwa waja wengi, huweza kugeuzwa kuwa hela ambazo zitamsaidia.
Teresa Kibiri, 22, ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha kitaifa cha anuwai cha Nyeri – Nyeri National Polytecnic – kilichoko katika Kaunti ya Nyeri.
Yeye husomea stashahada katika taaluma ya utengenezaji wa fasheni.
Nia yake katika shughuli hii ni kujipa riziki kwa kukusanya chupa za plastiki na za glasi zilizotupwa na kutapakaa kila mahali, na kuzitumia kuziunda hela kwa kuzitumia kuzitengeneza bidhaa kadha wa kadha, ambazo zina thamani katika maskani ya binadamu.
Aidha, Teresa anasema kwamba hii ni mojawapo ya mbinu za kuyahifadhi au kuyasafisha mazingira ili yawe safi na ya kufaa kwa watu.
“Mimi hutengeneza maua ya kurembesha nyumba na afisi kwa kutumia chupa za plastiki,” adokeza, akiongeza kuwa pia, huzitengeneza bidhaa za kurembesha maeneo ambayo sherehe mbalimbali huandaliwa.
Pia, yeye huzitumia nyuzi tofauti tofauti kuzitengeneza bidhaa zinazofanana na zulia.
Hutumia sindano maalumu na nyuzi kuzitengeneza baadhi ya bidhaa hizo.
Teresa alianza kushughulika na shughuli hiyo mnamo mwezi Machi mwaka uliopita, kwa kuutumia mtaji usiokuwa mwingi.
“Nilianza kwa kuutumia mtaji wa Sh3,500 nilizopewa na mamangu, Mary Kahaya. Mwalimu wetu wa miradi, Nicholas Mathendu, alinishauri nije na mradi na kuuwasilisha katika maonyesho ya bidhaa katika maonyesho ya tatu ya KATTI na TVET, yaliyoandaliwa katika uwanja wa Tononoka, Mombasa,” aeleza Teresa, akiongeza kuwa hushirikiana na Peris Mwangi, ambaye ni mwanafunzi mwenza katika chuo hicho.
Anafichua kuwa wao hushughulika na shughuli ya kuzitengeneza bidhaa zizo hizo katika siku za wikiendi, wakati ambapo hawamo darasani.
Hata hivyo, anasikitika kwa sababu kuna baadhi ya changamoto ambazo huwakabili.
“Mojawapo ya changamoto ni kuwa baadhi ya wateja hukosa kulipia baada ya kupelekewa bidhaa. Mimi huziuza bidhaa hizo mitandaoni, kote nchini,” afichua Teresa.
Mbali na kuziuza bidhaa zake mitandaoni, yeye huziuza bidhaa zenyewe katika duka la shangazi yake lililoko mjini Nyeri.
Anasema kuwa yeye huliuza ua moja kwa bei ya Sh1,200 na kigoda kimoja ambacho hukunjwa, huuzwa kwa bei ya Sh4,000. Pia yeye huzitengeneza sindano za kufumia ambazo huziuza kwa bei ya Sh500 kila moja. Hata hivyo, anadokeza kuwa bei inaweza kupunguzwa ikitegemea uwezo wa kifedha wa mnunuzi.
Teresa anafichua kuwa yeye hukusanya chupa za plastiki za maji, na za vinywaji vinginevyo kama vileo katika hafla mbalimbali. Aidha, hupata malighafi nyingine katika karakana ambazo hutengenezewa samani au fanicha.
“Mimi huzinunua nyuzi kwa Sh50 tu kila mmoja,” asema.
Teresa ana ushauri kwa vijana: “Ninawashauri vijana wenzangu kujitosa katika biashara hii kwa sababu huhitaji mtaji kidogo na ina faida.”
Anfichua kuwa katika siku za usoni, anaazimia kuisajili kampuni yake, na kushirikiana na washirika wengine ambao hutengeneza bidhaa na kupakia katika chupa, na ambao wana shida ya kukusanya chupa zizo hizo baada ya kutumiwa.
Hilo, asema Teresa, litasaidia kubuni ajira kwa watoto wanaorandaranda mitaani, kwa kuwapa kazi ya kukusanya chupa hizo na kuwauzia, na hivyo kupata riziki ya kila siku.