UBUNIFU WA KIUCHUMI: Anaendeleza kilimo cha kitunguu maji kwa mfumo wa mabonde
Na GRACE KARANJA
USHINDANI mkubwa wa kibiashara kutoka nchi jirani ya Tanzania unaendelea kuwapa tumbojoto wakulima wa humu nchini.
“Mapendekezo yetu kama wakulima ni kuomba serikali kama kweli inamjali Mkenya, itupunguzie gharama ya uzalishaji ya mazao humu nchini ili tuweze kupambana na hali ya biashara sokoni ambayo huingia kutoka mataifa jirani,” anasema mkulima Sarah Ngwiri kutoka eneo la Nebu, Gatundu Kusini.
Mkulima huyu amekuwa akifanya kazi katika kampuni mbalimbali kwa muda mrefu hadi pale alipochoshwa na sheria na masharti kutoka kwa waliomwajiri.
“Nilipata hasara sana msimu baada ya msimu. Nilikuwa tu nikipiga simu ili kujua hali ya mazao shambani kwani sikupata nafasi ya kwenda. Jambo hili liliniudhi sana hadi pale nilitafakari hatua ambayo ningechukua ili kujiendeleza katika kilimo cha kila siku. Japo haikuwa rahisi, niliamua kuacha kazi na kujiunga na kilimo masaa ishirini na manne,” anasema Sarah.
Jambo lingine lililomtia wasiwasi ni jinsi angepata fedha za kuanza tena kwa sababu alikuwa tayari amepata hasara na kubaki hoi kutokana na kilimo cha awali. Ni katika mtandao wa Facebook alipokutana na mtaalamu ambaye alimshauri kulima wakati wa msimu wa mvua na kutumia mfumo wa bonde yaani Basin irrigation ambao hauna gharama kubwa ya kuanza.
Mfumo huu wa mabonde hupunguza kiwango cha maji kinachotumika shambani, ni rahisi kunyunyizia madawa wakati mazao yameshambuliwa na pia ni rahisi kupalilia hata ukiwa peke yako.
Ushauri wa mtaalam
Julius Nduati, mwazilishi na mshauri wa mimea wa kampuni ya Afrikan Soil and crops Care Limited. Anasema mkulima anaweza kulima ikiwa ana chanzo cha maji zao hili hufanya vizuri maeneo yaliyo na joto la wastani.
Katika mfumo huu wa mabonde, bonde la futi moja kwa moja mraba hupandwa kati ya vitunguu 35 na 45.
Kama washauri wa kilimo wanavyosema kabla ya kufanya kilimo chochote kile mkulima anatakiwa kupima kiwango cha asidi kilichoko katika mchanga wake.
Kupanda
Kuna njia mbili za kupanda kitunguu nazo ni njia ya moja kwa moja ambapo shamba huandaliwa vizuri. Kisha mbolea ya samadi kwa kutawanya kisha kuchanganywa vizuri na udongo. Tengeneza mistari ya kina cha sentimita 2.5 na yenye umbali wa sentimita 30 kutoka mstari hadi mstari. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10.
Njia ya pili ni kupandikiza miche kutoka kitaluni baada ya wiki 6 au 8 tangu kusia mbegu. Ndiyo njia inayotumia zaidi na wakulima wengi wa vitunguu.
Nafasi ya upandaji iwe umbali wa Sm30 kati ya mstari hadi mstari na Sm 8 kati ya mche hadi mche. Muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu na hali ya hewa. Kuthibiti magugu kwa njia ya kung’olewa kwa mkono au kutifuliwa kwa jembe bila kuharibu mizizi ya kitunguu.
Aidha, Sarah anawahimiza wakulima kupanda kitunguu katika ardhi ambayo haina mazao mengine kwa kufanya hivyo utawezesha mwanga kupenya ndani ya vitunguu kwa urahisi, ambao husaindia kitunguu kukua upesi.
Mtaalam anaonya kuwa baadhi ya magonjwa kama vile Baka zambarau (Puple Blotch), ni ugonjwa ambao husababishwa na fangasi.