UBUNIFU WA KIUCHUMI: Mjasiriamali anayetengeneza bidhaa kupitia malighafi asilia
Na SAMMY WAWERU
UTENGENEZAJI na uimarishaji wa viwanda ni mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Serikali na ambazo Rais Uhuru Kenyatta ameahidi kutekeleza.
Mgao wa mabilioni ya pesa umetengewa hilo na utaendelea kutengwa, mradi kuona viwanda vilivyoko vinaimarishwa na vinavyopaniwa kufunguliwa.
Hata hivyo, kwa Roger Wekhomba, ufunguzi wa viwanda hauhitaji mamilioni au mabilioni ya pesa. Mtafiti na mjasirimali huyo, ambaye ana Shahada ya Masuala ya Sayansi, anahoji kwamba ikiwa una vifaa vinavyotumika jikoni kama vile sufuria, mwiko au kijiti cha mapishi, kisu, kijiko, kichujio na moto, basi una kiwanda na tayari kuunda bidhaa.
Aghalabu, nyingi ya bidhaa tunazotumia kila siku zinatokana na mimea na mazao ya kilimo. Kwa mfano, juisi au sharubati, kinywaji kipenzi cha wengi, inaundwa kwa matunda.
Mji wa Ruaka, ulioko Kaunti ya Kiambu, shughuli mbalimbali kuanzia zile za biashara hadi uchukuzi, zimenoga. Katika mji huo huo, Roger amewekeza katika kiwanda cha uongezaji thamani mimea na mazao ya kilimo.
Kwenye jengo la shughuli hiyo, chini ni duka ambalo limesheheni sabuni na mafuta aina tofauti.
“Bidhaa hizi zote zimeundwa kwa mazao ya kilimo na mimea, hazijatiwa kemikali yoyote, ni bidhaa hai (organic) na ambazo ni salama,” akaambia Akilimali.
Juu ya duka hilo, ni karakana iliyosheheni malighafi yatokanayo na mazao ya kilimo na mimea. Ni kiwanda cha kutengeneza sabuni, mafuta (lotion na cream), vipodozi na mishumaa inayonukia. Chini ya kampuni yake inayofahamika kama Soap Masters, Roger pia hutengeneza viungo kama vile tomato sauce, tomato paste, chillie sauce, jemu, peanut, miongoni mwa vinginevyo.
Aidha, bidhaa hizo ni kati ya Sh100-800.
Malighafi anayotumia yanajumuisha matunda kama vile maparachichi, machungwa, mafuta ya nazi na ya mapera.
Katika orodha hiyo pia kuna nyanya, matunda ya kahawa, mbegu za cheer, moringa, hawaji ndiyo turmeric, tamarind, makaa, mafuta ya mbarika, mdalasini (cinnamon) na maua aina ya hibiscus.
Roger anasema utengenezaji wa bidhaa hizo, ni shughuli inayochukua muda mfupi. Anakusanya malighafi kadhaa na kwa pamoja anayatia kwenye jegi.
Kwa kifaa anachotambua kama stick blender, anayachanganya sawa na inavyosongwa sima kisha kwa kutumia chombo maalum aina ya cake mixer kilichounganishwa kwa nguvu za umeme, anakoroga kwa kasi. Vifaa hivyo, anadokeza kuwa kimoja kinauzwa kati ya Sh2, 400 – 3, 000.
Ni shughuli inayochukua chini ya dakika kumi pekee.
“Muda huo, nimetengeneza mikebe minne ya mafuta, mmoja ukiwa na uzani wa gramu 200 nitakaouza Sh800. Nikikokotoa gharama ya kuunda mmoja haizidi Sh150, hii ikiwa na maana kuwa nitaunda faida ya Sh650,” afafanua.
Mjasirimali huyo anasema changamoto kuu katika jitihada zake ilikuwa ukosefu wa fedha, na kupitia mfadhili mmoja alipigwa jeki kima cha Sh3.3 milioni pamoja na akiba yake iliyofikia Sh500, 000.
Kulingana na Roger, ambaye pia ameandika kitabu ‘Neglected Value’ kinachofafanua jinsi rasilimali zimepuuzwa, viwanda na maendeleo yatajiri ikiwa serikali italipa kipaumbele suala la uongezaji thamani mazao ya kilimo.
Wakati wa mahojiano aliiambia Akilimali kuwa kwa siku hufanya mauzo kati ya bidhaa 15-20.