UCHAFUZI WA HEWA: Athari za hewa chafu kwa mapafu ni sawa na kuvuta pakiti moja ya sigara kila siku
Na LEONARD ONYANGO
MAMILIONI ya Wakenya wanaoishi mijini wamekuwa wakivuta zaidi ya sigara 20 kwa siku bila kujua.
Wataalamu wanasema kuwa ukiishi au kufanya kazi kwenye mazingira yaliyo na hewa chafu kama vile maeneo ya viwandani, steji ya mabasi au maeneo yaliyo na vumbi nyingi kwa muda mrefu ni sawa na mtu ambaye anavuta pakiti, moja ya sigara kila siku kwa kipindi cha miaka 29.
Wataalamu wa afya pia wanasema kuwa mtu anayevuta hewa chafu yuko katika hatari kubwa ya kuugua maradhi ya mapafu sawa na mvutaji sigara.
Watafiti nchini Amerika walihusisha watu 7,071 wa kati ya umri wa miaka 45 na 84 ambao ni wakazi wa miji iliyoathiriwa na hewa chafu.
Walipima hewa katika makazi yao kubainisha kiwango cha chembechembe za kemikali.
Baadaye watu hao walipimwa hali yao ya afya ya mapafu.
Watafiti waliwafuatilia kwa kipindi cha miaka 10 na kisha kuwapima tena.
Katika maeneo yaliyokuwa na hewa chafu zaidi, walibaini kuwa idadi kubwa ya watu walikuwa na ugonjwa wa mapafu sawa na mtu ambaye amevuta sigara kwa kipindi cha miaka 29.
“Tulishangaa kubaini kuwa hewa chafu ina madhara sawa na sigara ambayo imekuwa ikiaminika kuwa chanzo kikuu cha magonjwa ya mapafu,” akasema Dkt Joel Kaufman, mmoja wa watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Washington.
Hewa chafu pia husababisha ugonjwa wa pumu (asthma).
Aidha inapunguza maisha ya watu na hata kutatiza uwezo wa wanawake kuzaa.
Kufanya vibaya shuleni
Mbali na kusababisha maradhi ya mapafu, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha California, Amerika pia umebaini kuwa watoto wanaoishi karibu na barabara ambapo magari hupita kwa wingi, hufanya vibaya shuleni.
Watafiti hao walisema watoto hao huwa na matatizo ya kukua na hata kuzungumza.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Environmental Research, unasema kuwa hewa chafu inayotolewa na magari ni hatari kwa watoto wadogo na hata akina mama wajawazito.
“Matokeo ya utafiti wetu yanaonyesha kuwa kuna haja ya akina mama wajawazito na watoto wadogo kuepushwa na na mazingira yenye hewa chafu,” akasema Dkt Pauline Mendola, mtafiti wa Kitivo cha Afya ya Umma chuoni hapo.
Tafiti za hapo awali zimeonyesha kuwa hewa chafu husababisha mama mjamzito kujifungua mtoto wa uzani wa chini. Wanasayansi pia wanaamini kwamba hewa chafu husababisha kujifungua mtoto kabla ya kufikisha wakati wake au kuharibika kwa mimba.