Makala

Uchaguzi 2027: Ruto akimbizana na miradi ya ‘hustler’ aliyoahidi raia

Na MOSES NYAMORI May 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameanza upya juhudi za kufufua utekelezaji wa miradi yake aliyoahidi kuboresha maisha ya wananchi mashinani, huku akilaumiwa kwa kushindwa kutimiza ahadi nyingi za kampeni alizotoa kabla ya uchaguzi wa 2022.

Katika ziara zake mbalimbali nchini, Rais Ruto amekuwa akisisitiza utekelezaji wa miradi kama ujenzi wa masoko ya kisasa kwa kina mama mboga, mpango wa nyumba za bei nafuu, na upanuzi wa huduma za umeme vijijini.

Miradi hii imeanza kuchukua nafasi ya kipekee kwenye ajenda ya maendeleo ya Rais, ikifasiriwa kama mbinu mpya ya kujipanga upya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika kampeni za 2022, Rais Ruto alijijenga kupitia sera ya kuinua uchumi kuanzia mashinani aliyoiuza kwa watu wa kipato cha chini, kama vile wahudumu wa boda boda, vijana wasio na ajira na mama mboga.

Lakini zaidi ya miaka miwili akiwa mamlakani, ahadi zake nyingi hazijatekelezwa kikamilifu, hali iliyopelekea rais mwenyewe kuanza kufuatilia kwa karibu miradi hiyo kupitia ziara zake za kikazi.

Katika ziara yake ya hivi karibuni Kaunti ya Migori, Rais alikagua maendeleo ya ujenzi wa masoko kadhaa ikiwemo soko la Riosir huko Rongo litakalowahudumia wafanyabiashara zaidi ya 300, soko la matunda la Oria linalogharimu Sh47 milioni katika eneo la Uriri, na soko la Ntimaru katika Kuria Mashariki.

Katika ziara yake Narok, Rais alizindua soko la kisasa la Suswa ambalo limekamilika na liko tayari kutumika, pamoja na soko la Ntulele ambalo pia limekamilika.

“Nchi yetu inaweza kubadilishwa na viongozi jasiri na wenye maono, walio tayari kufanya maamuzi sahihi. Tumejitolea kuunganisha taifa letu ili kuunda mazingira bora kwa mafanikio ya kiuchumi, bila kujali tofauti zetu za kisiasa,” alisema akiwa Uriri.

Mradi wa nyumba za bei nafuu umekuwa sababu kuu ya ziara za Rais.

Ingawa ushuru wa nyumba unaofadhili mradi huu umekumbwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wafanyakazi wa mshahara wa kila mwezi, Rais Ruto anaonekana kushikilia msimamo wa kuutekeleza kikamilifu.

Kulingana na serikali, zaidi ya nyumba 130,988 ziko kwenye hatua mbalimbali za ujenzi, huku zingine 127,476 zikiendelea kuuzwa.

Licha ya maendeleo hayo, serikali imeshindwa kutimiza lengo la kujenga nyumba 200,000 kwa mwaka.

Akiwa Migori, Rais alizindua ujenzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu wa Kehancha wenye vyumba 298 katika Kuria Magharibi, na pia ujenzi wa nyumba 183 katika mradi wa Ntimaru.

Katika Mji wa Kilgoris, Kaunti ya Narok, alizindua mradi mwingine wa nyumba.

“Miradi yetu ya mabadiliko imeleta utulivu kwa uchumi wetu. Tuko kwenye njia ya kuharakisha ukuaji kupitia miradi yetu mingi ya maendeleo inayochochea uchumi na kuzalisha utajiri kwa wote,” alisema akiwa Kilgoris.

Serikali inadai kuwa mpango huo umechangia ukuaji wa uchumi kwa kuzalisha nafasi 244,232 mpya za ajira katika sekta ya ujenzi, huku ajira katika sekta hiyo zikifikia 261,976 mwaka 2025.

Hata hivyo, ripoti ya Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) mwaka 2024, imeonyesha kuwa sekta ya ujenzi ilidorora kwa asilimia 0.7 mwaka huo, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3 mwaka 2023.

“Sekta ya ujenzi ilidorora kwa asilimia 0.7 mwaka 2024 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3 mwaka 2023, hali iliyoashiria kipindi cha mabadiliko kwa sekta hiyo,” ilisema KNBS.