UCHAGUZI WA 2027: Vyama vipya 25 vyasajiliwa 30 vikiwasilisha maombi ya kusajiliwa
TAKRIBAN vyama vipya 25 vya kisiasa vimepata usajili wa muda katika kipindi cha miezi michache iliyopita, huku vingine zaidi ya 30 vikiwasilisha maombi ya kusajiliwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Mbio hizi za kusajili vyama vipya zinaashiria wasiwasi unaoongezeka katika ulingo wa siasa, hasa kutokana na mchakato wa kura za mchujo katika miungano mikubwa ambapo wanasiasa mara kwa mara wamekuwa wakipokonywa haki na kunyimwa tikiti za kuwania nyadhifa mbalimbali.
Fedha za Hazina ya Kitaifa ya Vyama vya Kisiasa ya mabilioni ya shilingi pamoja na hamu ya kuingia katika miungano kama wadau wakuu, pia ni kichocheo kikubwa cha mbio hizi za kusajili vyama vipya.
Vyama ambavyo havikuwa vikifaidika na mabilioni ya pesa za Hazina ya Vyama vya Kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2022, kwa mara ya kwanza vimeanza kupokea fedha za kufadhili shughuli zao kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2022.
Sheria hiyo inaelekeza kuwa ili chama cha kisiasa kifaidike na Hazina ya Vyama vya Kisiasa, lazima kiwe na angalau mwakilishi aliyechaguliwa, uwiano wa kijinsia wa thuluthi mbili miongoni mwa viongozi wa chama, na uwakilishi wa makundi maalum katika uongozi.
Sheria hiyo pia inaeleza kuwa asilimia 70 ya fedha hizo hugawanywa kwa kuzingatia uwiano wa jumla ya kura ambazo chama kilipata katika uchaguzi uliotangulia.
Stakabadhi kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) inaonyesha kuwa Achievement Party of Kenya (ACPOK), Accountability and Transparency Party (ATP), Kenya Liberation Movement (KELMO), Economic Patriotic Alliance (EPA), The Economic Pillars Alliance (TEPA) na Reformed Patriotic Democrats (REPA) vilipata usajili wa muda mwezi Septemba.
Mwezi Julai, ORPP ilitoa usajili wa muda kwa Vision for Development Alliance (VIDA), Hekima Alliance Party (HAPA) na Kenya Ahadi Party (KAP).
Vilivyosajiliwa pia ni Forty-Seven Voices of Kenya Congress Party (VOICES), African Development Congress (ADC), Msingi wa Utaifa Party (MUP), Conservation of Democracy in Kenya (COD-K), National Transformation Party (NTP) na United Patriotic Movement (UPM).
Vyama vingine vipya vilivyosajiliwa ni The Inclusive Party (TIPTIP), Alliance for Democratic Association (ADA), People’s Forum for Rebuilding Democracy (PFRD), Imarisha Uchumi Party (IUP), The Future Party (TFP), Economic Liberation Alliance Party (ELAP), Kenya Democracy for Change (KDC), Kenya United Generation Party (KUG), Forum for Economic Development Agenda (FEDA) na National Economic Development Party (NEDP).
Centrists for Economic and Social Reforms Party (CESRP), National Harmony Party of Kenya (NHPK) na Social Democratic Party of Kenya (SDP) ni miongoni mwa zaidi ya vyama 30 ambavyo majina yao yamehifadhiwa na kuidhinishwa kwa usajili.
Vyama hivyo vipya vinaongeza orodha ndefu ya jumla ya vyama 91 vilivyosajiliwa kikamilifu. Democracy for the Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na The Alliance Party (TWAP) ni miongoni mwa vyama vilivyopata usajili kamili mapema mwaka huu.
Bw Gachagua alisajili chama kipya kufuatia kutimuliwa kwake madarakani Oktoba 2024.
Hatua hiyo ilitokana na mzozo mkali kati yake na Rais William Ruto. Tangu wakati huo, chama chake kimekuwa mstari wa mbele kupinga United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto, hasa katika eneo la Mlima Kenya.