Akili MaliMakala

Uchakataji viazi kupunguza hasara

January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SIRI kwenye kilimo ipo kwenye uchakataji wa mazao, ndio kauli anayoamini Teresiah Wanjiku, mkulima wa viazi kutoka Nyandarua. 

Nyandarua ikiwa mojawapo ya kaunti nguzo kuu katika uzalishaji nchini na inayoongoza, Wanjiku amekuwa kwenye kilimo cha zao hilo kwa kipindi cha miaka 10.

Hata hivyo, mwaka 2020 – katikati mwa janga la kimataifa la Covid-19 nusra mama huyu akatize ndoto yake ya kusaidia kuziba gapu ya uzalishaji viazi nchini.

Hilo, anasema linatokana na amri ya kutoka ama kuingia Nairobi na viunga vyake, ambayo ni mnunuzi mkuu wa viazimbatata.

Teresiah Wanjiku, mkulima wa viazi kutoka Nyandarua na mwanachama wa Kiwafa Self-Help Women Group akielezea kuhusu uchakataji viazi chini ya muungano wao. Picha|Sammy Waweru

“Mazao ya wakulima yaliharibika na kuozea shambani kwa sababu ya kukosa wanunuzi,” anaelezea.

Wanjiku anakumbuka kupoteza zaidi ya magunia 500 ya viazi ambayo endapo angeuza kwa kipakio cha kilo 50 – kila gunia lingemuingizia Sh3, 000.

Virusi vya corona navyo vikamtoa nyama mdomoni.

Chini ya kundi la kina mama la Kiwafa, Nyandarua, Wanjiku na wakulima wenza walifunguka macho.

Anasema, hasara waliyokadiria ikawa mwanzo wa kuchakata viazi lengo likiwa kurefusha muda wa mazao yao kudumu ili kuwahi soko lenye ushindani mkuu.

Kiwafa Self-Help Women Group iliasisiwa 2008, kulingana na Wanjiku kwa minajili ya kuboresha maisha ya wakulima wa viazi eneo la Ol Jororok, Nyandarua.

Teresiah Wanjiku, mkulima wa viazi kutoka Nyandarua akionyesha vitafunwa vya viazi. Picha|Sammy Waweru

Uongezaji thamani, ni safari iliyong’oa nanga 2023, baada ya wanachama wake kupata mafunzo kupitia taasisi mbalimbali kama vile Shirika la Utafiti wa Masuala ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo (Kalro) chini ya Wizara ya Kilimo, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta  (JKUAT) na kile cha Nairobi (UoN).

“Kalro ilitufunza jinsi ya kuzalisha mbegu bora na ya hadhi ya viazimbatata, JKUAT nayo ikatufadhili mashine na mitambo ya uchakataji na UoN  – ikatufunza jinsi ya uongezaji bidhaa thamani,” Wanjiku anaelezea.

Miaka miwili baadaye, kutoka uchakataji wa tani 1 moja ya viazi sasa kundi hilo la kina mama linasindika kilo 20 kila wiki.

Wanjiku anakadiria kukua ambapo muungano kiwango cha wanachama kimepanda hadi 15 kutoka 10 waliouanzisha.

Potato sticks ni aina ya kripsi za viazi ambazo Teresiah Wanjiku huunda kwa kutumia viazimbatata. Picha|Sammy Waweru

“Mwenyewe, sasa ninakuza viazi kwenye ekari tatu kutoka kwa robo ekari niliyoanza nayo,” anakiri, akifichua kuwa ilimgharimu mtaji wa Sh20, 000 kuingilia kilimo cha viazimbatata.

Wanjiku alikuwa akifanya kazi kwenye maabara ya masuala ya afya, kabla kuingilia zaraa.

Chini ya KIWAFA, huchakata unga – unaoundwa kwa kutumia viazi, vitafunwa kama vile kripsi na vipande vyembamba vya viazi vilivyokaushwa vyenye muundo wa vijiti.

Kwa wiki, kundi hilo Wanjiku anadokeza kwamba huunda kilo 750 za unga wa viazi kilo moja ikiuzwa Sh500, na kipimo sawa na hicho cha vipande vya viazi vilivyokaushwa (starch), bei pia ikiwiana.

Kripsi na vitafunwa, gramu 100 huchezea Sh100.

Teresiah Wanjiku, mkulima wa viazi kutoka Nyandarua, wakati wa maonyesho ya Kibiashara Afrika Mashariki (EAC-MSMEs), Nairobi akionyesha mseto wa bidhaa za viazi zilizochakatwa. Picha|Sammy Waweru

Kundi hilo likikadiria kuhudumia zaidi ya wakulima 1,000 Ol Jororok, Wanjiku anakiri kupunguza kiwango cha uharibifu wa mazao kutoka asilimia 30 hadi chini ya asilimia 15.

“Faida tunayopata kama wakulima wa viazi kupitia uongezaji mazao thamani ni ishara kuwa siri ya kilimo ipo kwenye uchakataji.”

Wanjiku ambaye pia ni karani, anasema kwa msimu chini ya mafunzo faafu kitaalamu wanayoendesha ekari moja humpa karibu magunia 120.

Bei nayo, aghalabu kwa muda sasa imekuwa ikichezea kati ya Sh3, 000 hadi Sh3, 500.

Teresiah Wanjiku, ambaye ni mkulima Nyandarua na mwanachama wa Kiwafa Self-Help Women Group wakati wa Maonyesho ya EAC-MSMEs, Nairobi 2025. Picha|Sammy Waweru

Licha ya ufanisi waliopata, anasema ukosefu wa mashine na mitambo ya kisasa na ya kiotomatiki inalemaza utendakazi wao.

Tunaomba serikali na wahisani wajitokeze kupiga jeki huduma zetu kuboresha sekta ya viazi nchini, Wanjiku anarai.

Anasema, hilo likiafikika upotevu wa viazi ambao wakulima wanalalamikia kila uchao, kikundi chao kitasaidia kwa kiwango kikubwa kushusha gapu hiyo.

Kulingana na Serikali ya Gatuzi la Nyandarua, kaunti hiyo tajika katika uzalishaji viazimbatata hupoteza kati ya asilimia 30 na 40 ya viazi msimu wa mavuno kwa sababu ya wakulima kukosa miundomsingi bora na soko la mazao.