• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
UCHAMBUZI WA VITABU VYA FASIHI: Maudhui ya Malezi katika Riwaya ya Chozi la Heri

UCHAMBUZI WA VITABU VYA FASIHI: Maudhui ya Malezi katika Riwaya ya Chozi la Heri

Na ENOCK NYARIKI

TUSINGETAMATISHA sehemu ya maudhui katika riwaya ya Chozi la Heri kabla ya kuyaangazia maudhui ya ulezi. Upo ulezi wa kupanga ambao mwandishi anauonyesha kama unaofaa katika mazingira fulani hasa mazingira ya vita ambayo husababishia familia utengano wa aina nyingi.

Ulezi huu pia unaonyeshwa kama unaowezekana katika mazingira ambapo wanandoa wamejaribu kupata mtoto lakini kwa sababu ya ugonjwa au hali nyingine za kimaumbile jambo hilo haliwezekani.

Katika Msitu wa Mamba zinakohamia familia nyingi baada ya machafuko ya uchaguzi mkuu unaanza kuvyaza kizazi kipya cha matajiri kama vile Lunga na wenzake ambao wanamiliki mashamba makubwa yanayotoa mazao mengi. Jambo hili linaibua tatizo jipya la uhasama kutokana na kutanuka kwa pengo baina ya walionacho na wasionacho.

Awamu ya kwanza ya vita vya wenyewe kwa wenyewe inapoanza, serikali inaamua kuwahamisha watu hawa kutoka kwenye Msitu wa Mamba walikokaa kiharamu na kuwapeleka katika Msitu wa Simba. Lunga anajikuta akiogelea kwenye lindi la umaskini. Fidia anayopewa na serikali haitoshi kutekeleza mahitaji yake yote ya kimsingi. Naomi, mkewe Lunga, hawayakubali mabadiliko yanayoikumba aila na hayuko radhi kuishi tena na Lunga.

Kwenye barua anayomwandikia Lunga(uk,81), Naomi anamwambia anataka kutamba na ulimwengu kwa sababu kwa njia hiyo angeambulia chochote ambacho angetumia kumsaidia Lunga kukimu aila. Lunga anapoaga dunia kutokana na kihoro cha kutengwa na mkewe na kutokana na kuporomoka ngazi ya maisha wanawe Umu, Dick na Mwaliko wanaachwa mikononi mwa kijakazi.

Sauna, kijakazi wa akina Umu anapoamua kutoroka na Dick na Mwaliko ambao baadaye anawatumia kama vyambo vya kujipatia riziki yake, Umu anajikuta kwenye njia panda. Baadaye Umu anajikuta jijini anakojiunga na shule ya Tangamano. Kwa msaada wa Mwalimu Dhahabu, Umu anapata wazazi wapya ambao wanayakidhi mahitaji yake ya malazi, chakula na elimu. Wazazi hawa wapya ni Mwangeka na Apondi. Mwaliko, nduguye Umu, naye anajikuta mikononi mwa walezi wapya ambao ni Mwangemi na mkewe Neema ambao hawana mtoto kwa sababu ya ugonjwa wa Sickle-cell. Baadaye sadfa inawakutanisha Dick na Umu katika uwanja wa ndege. Wazazi wa kupanga wa Umu wanaamua kumtilia Dick upondo.

Alhasili, upangaji wa watoto ni ulezi mbadala hasa pale ambapo ulezi wa kawaida umekumbwa na changamoto za kila aina. Mwandishi anaonyesha ufanisi wa ulezi wa kupanga kwa kutuonyesha ufanisi kimaisha kwa watoto waliopitia ulezi wa aina hiyo. Kwa mfano, Umu anaishia kuwa injinia, Dick anafanikiwa katika biashara na Mwaliko ni mhariri katika kampuni ya magazeti ya Tabora.

Uwajibikaji

Mwandishi aidha anakashfu kutowajibika kwa wazazi katika malezi ya watoto wao. Naomi, mkewe Lunga anasawiriwa kama mwanamke asiyeyajali malezi ya watoto wake. Badala ya kumtia moyo mumewe na kumsaidia alaa kulihali katika kuwalea watoto, anaamua kujitenga naye wakati ambapo Lunga anakabiliana na mawimbi yanayosababishwa na kuteremka kwa vidato vya maisha. Lunga anapoaga dunia, watoto wanajikuta hawana mtu wa kuwaelekeza.

Kunayo pia malezi ya Chandachema ambayo yanatekelezwa na bibi yake Chandachema. Fumba, baba yake Chandachema anampeleka mwanawe huyo kijijini kwa wazee wake na kumtelekezea kule. Chandachema anazaliwa baada ya Fumba kumringa mwanafunzi wake Rehema. Si fumba wala Rehema wanawajibikia malezi ya mtoto wao. Bibi anapoaga dunia, Chandachema anajikuta mikononi mwa jirani ambaye naye hamsetiri kwa muda mrefu.

Wazazi wa Zohali pia hawauwajibiki ulezi wa Zohali hasa pale Zohali anapoambulia ujauzito akiwa katika kidato cha pili. Jambo hili linamfanya Zohali kutorokea jijini anamokumbana na matatizo ya kila aina. Pete anasema kuwa ana wazazi wawili ila ni wazazi tu. Hajadiriki kuonja utamu wa malezi ya baba wala mama baada ya mama yake kumpeleka kwa bibi na kumtelekeza kule. Jambo hilo lilitokea baada ya kuzuka kwa mzozo baina ya baba na mama kuhusu babaye Zohali(uk, 146- 147).

Vituo vya kuwalea watoto yatima vinajitokeza kuwa makazi mbadala kwa watoto wanaojikuta katika hali tata za ulezi. Miongoni mwa vituo vinavyoelezewa humu ni pamoja na Wakfu wa Mama Paulina, shirika la Kidini la Hakikisho la Haki na Utulivu, Jeshi la Wajane wa Kristu miongoni mwa vituo vingine.

Maudhui mengine yanayojitokeza riwayani ni pamoja na uchafuzi wa mazingira, ukosefu wa ajira, ufisadi, usihiri miongoni mwa mengine madogo. Katika makala yajayo tutashughulikia nafasi ya vijana riwayani.

You can share this post!

UCHAMBUZI WA VITABU VYA FASIHI: Maudhui zaidi katika...

SHANGAZI AKUJIBU: Nitaishi vipi na mke na mie hujikojolea...

adminleo