Uchanganuzi: Bila Kalonzo itakuwa mlima kwa Raila kukwamua Ruto 2027
RAIS William Ruto ambaye anaonekana kupoteza ushawishi eneo la Mlima Kenya lililo na kura nyingi anahitaji kiongozi wa ODM Raila Odinga ili kufanikisha azma yake ya kuchaguliwa tena 2027.
Na hii ni iwapo Bw Odinga atahifadhi ngome zake, ambazo hazitoshi endapo kiongozi huyo wa upinzani, hataungwa mkono na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.
Katika uchaguzi wa urais wa 2022, ambao Dkt Ruto alimshinda Bw Odinga, rais alipata asilimia 87 ya kura za Mlima Kenya, ambazo ni asilimia 42 ya jumla ya kura alizopata kitaifa.
Isipokuwa mwaka wa 2007, Bw Musyoka alipowania urais, amekuwa mgombea mwenza wa kiongozi huyo ODM mara mbili. – 2013 na 2017. Bw Musyoka pia alimuunga mkono Bw Odinga 2022 alipokuwa na Bi Martha Karua kama mgombea mwenza wake.
Ni kutokana na hali hiyo ambapo wachambuzi wanahoji kuwa Rais Ruto anahitaji kuungwa mkono na Bw Odinga ili kuepuka aibu ya kuondolewa madarakani baada ya muhula mmoja, na hata hivyo, muungano wao bado utakuwa dhaifu bila uungwaji mkono wa Bw Musyoka na Mlima Kenya.
Sio sasa
Hata hivyo, Bw Munyori Buku, mkuu wa Mawasiliano wa Rais Ruto, alisema majadiliano kuhusu azma ya Rais Ruto kuwania muhula wa pili si suala la kuzungumziwa kwa wakati huu.
“Muhula wa pili? Rais Ruto hajawahi kuzungumzia muhula wa pili! Kwa hakika, amesema kwenye mikutano ya hadhara kwamba hauwezi kutumia muhula wa kwanza kufikiria wa pili,” Bw Buku aliambia Taifa Leo.
“Kwa hivyo, mwelekeo huo haufai kabisa. Mabadiliko katika makazi, huduma za afya kwa wote, kilimo, ujumuishaji wa kidijitali na ushirikishwaji wa kifedha, miongoni mwa mengine, zinatekelezwa sasa,” Bw Buku aliongeza.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri wa chuo kikuu Prof Peter Kagwanja anahoji kuwa ‘Rais Ruto bila kuungwa mkono na Mlima Kenya lakini akiwa na Bw Odinga, atashinda muhula wa pili’.
Lakini mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) Bw Charles Mwangi anasema Odinga bila Bw Musyoka hawezi kuwa msaada kwa Rais Ruto.
Bw Mwangi anahoji kuwa 2007 Dkt Ruto alikuwa katika kambi moja na Bw Odinga lakini wakashindwa na Mwai Kibaki.
Anasema ‘inasikitisha kusikia watu wakifikia uamuzi kwamba Bw Odinga atamsaidia Rais Ruto uchaguzini kushinda muhula wa pili’.
Bw Mwangi anahoji kuwa Bw Odinga huwa anasaidiwa na watu wengine hasa Bw Musyoka.
“Ili Rais Ruto anufaike na uungwaji mkono wa Odinga, lazima awe pamoja na Musyoka,” alisema.
Bila Ruto
Seneta wa Makueni Bw Dan Maanzo aliambia Taifa Leo kwamba ‘mnamo 2027 Bw Musyoka ataungana na vyama vingine ambavyo havijumuishi Rais Ruto’.
Alisema ‘tayari tunachangamkia ambao wamekasirishwa na utawala mbovu unaodhihirika kote, kutojali hisia za Wakenya na tabia ya kutokubali ukweli’.
Kufikia sasa, Bw Musyoka anaonekana kuwania Mlima Kenya kuelekea 2027 ingawa Mlima huo huo unawalenga Bw George Natembeya na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani Dkt Fred Matiang’i.
Bw Mwangi aliongeza kuwa “isisahaulike kwamba matokeo ya mwisho ya Bw Odinga yalikuwa na takriban asilimia 12 za kura za Mlima Kenya ambazo rais wa zamani Uhuru Kenyatta na Martha Karua walimsaidia kupata”.
Alisema hakuna uwezekano kwamba eneo la Mlima Kenya ambalo tayari limeonyesha hisia baridi kwa Rais Ruto na wafuasi wake litaruhusu mgawanyiko wowote wa maana katika uchaguzi.
Mlima Kenya hautagawanyika
Mtaalamu wa siasa Gasper Odhiambo anasema 2027 kutakuwa na miungano itakayozunguka Rais Ruto, Mlima Kenya, Odinga na Bw Musyoka.
Anasema kuwa ‘dalili zote zinaonyesha kuwa Mlima Kenya hautagawanyika licha ya Rais Ruto kumtumia Kindiki kutwaa Mlima Kenya Mashariki ambao una kaunti za Meru,Embu na Tharaka Nithi.
Ili kutimiza hilo, Bw Odhiambo anatarajia Rais Ruto kuchaguliwa tena iwapo Odinga na Musyoka watakuwa upande wake.
“Mipangilio mwingine hatari kwa Rais Ruto ni kuungana na Odinga, bila Mlima Kenya, na bila Bw Musyoka au mbaya zaidi Rais Ruto bila Odinga, na Musyoka na Mlima Kenya,” akasema.
Wadadisi wanasema ushawishi wa Dkt Ruto umepungua pakubwa miongoni mwa raia hivi kwamba itakuwa vigumu kwa muungano wowote kumsaidia kuurejesha wakitaja sera za serikali yake ambazo zimewakera raia.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA