Uchomaji makaa Boni ungali tishio kwa uhifadhi wa mazingira
Na KALUME KAZUNGU
UCHOMAJI wa makaa ndani ya msitu mkuu wa Boni, Kaunti ya Lamu bado ni tishio kwa uhifadhi wa mazingira eneo hilo.
Imebainika kuwa licha ya kuwepo kwa doria nyingi za walinda usalama wanaohakikisha marufuku ya kukata miti na usalama vinadhibitiwa eneo hilo, biashara ya makaa bado imetia for a na kukita mizizi kwenye sehemu nyingi za msitu wa Boni.
Utafiti uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa sehemu ambazo biashara ya magendo ya makaa inaendelezwa ni pamoja na Ziwa la Kengo, Ziwa la Taa, Maisha Masha, Jima, Poromoko, Mavuno, Bar’goni, Ingini na sehemu zingine ambazo zote zinapatikana kwenye msitu wa Boni.
Baadhi ya waliohojiwa walikiri kushirikiana na maafisa wa usalama, ikiwemo wale wa Shirika la Huduma za Misitu (KFS) na wale wa wanyamapori (KWS) katika kuendeleza biashara haramu ya makaa.
Rama Karisa ambaye ni mchomaji maarufu wa makaa alisema hajakamatwa na polisi yeyote licha ya kuendeleza biashara hiyo kila kukicha kwani yeye pamoja na wenzake huwahonga fedha au magunia ya makaa walinda usalama hao ili kuwaruhuru kupita vizuizi vyao badala ya kuwakamata.
“Najua marufuku ya kukata misitu ipo. Hata hivyo bado tunaendeleza biashara ya uchomaji makaa kwani ndicho kitega uchumi chetu cha kipekee. Inabidi tunakula na hawa walinda usalama ili wasitushike,” akasema Bw Karisa.
Kuondolewa kwa marufuku ya kukata mikoko eneo la Lamu mwaka jana pia kumetajwa kuchangia kuendelezwa kwa biashara ya kuchoma makaa na kuvuna mbao msituni Boni.
Hassan Bole ambaye ni mnunuzi maarufu wa makaa eneo la Lamui alisema baadhi ya wachomaji makaa wamekuwa wakitumia mwanya huo wa kuondolewa kwa marufuku ya mikoko kuendeleza biashara ya makaa.
“Mtu anajidai yeye ni mkataji mikoko aliyeruhusiwa kuendeleza biashara hiyo. Anapoingia msituni anaendeleza mambo yake, ikiwemo kuchoma makaa,” akasema Bw Bole.
Kwa upande wake aidha, Afisa wa Kuhifadhi Misitu, tawi la Lamu, Evans Maneno alitoa onyo kali kwa wanaokiuka marufuku yaliyoko ya kukata miti kiholela na kuharibu misitu nchini.
Bw Maneno alisema kuendeleza uchomaji wa makaa usioruhusiwa kwenye misitu ya serikali ni hatia na kwamba watakaopatikana wakifanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Lamu iko na misitu mitano mikuu ya serikali, ikiwemo Boni, Pandanguo, Boni-Lungi huko Mangai, Witu na ule mkubwa zaidi wa kisiwa cha Lamu.
“Tumeweka mikakati kabambe , ikiwemo kuongeza doria za walinda usalama msituni ili kuona kwamba biashara ya uchomaji makaa isiyoruhusiwa haiendelei. Ninashuku wale wanaoendeleza biashjara hiyo wanaifanya kisiri kwenye mashamba yao ya kibinafsi. Tushirikiane ili kutunza mazingira yetu,” akasema Bw Maneno.