UDAKU: Sanaipei adai kolabo nyingine na Jua Cali haitatokea
NA SINDA MATIKO
JUZI, msupa Sanaipei Tande alitupia picha akiwa anajiachia na rapa Jua Cali.
Kwa mashabiki wao wengi, wakaamini kwamba malejendari hao watakuwa wanapanga kuachia mzigo mwingine wa pamoja.
Licha ya kuwa Sanaipei na Jua Cali wana kolabo moja tu tena iliyofanywa zaidi ya miaka 12 iliyopita, kazi hiyo ‘Kwaheri’ iliyokuwa hiti kubwa enzi ilipotoka, bado haijashuka wala kuisha ladha.
Isitoshe, kwa namna mastaa hao walivyoweza kujiheshimisha na kudumu kwenye gemu kwa zaidi ya mwongo na nusu, wengi walihoji kwamba, itakuwa haki kama wakiingia studio na kuandaa fataki nyingine.
“Ndio tatizo lililopo na tasnia yetu, vichwa viwili vya mastaa vikikaa pamoja inakuwa kwamba aidha kuna kasheshe baina yao, ama ni kolabo wanapanga. Lakini yule ni mshikaji wangu, ndiye msanii wa kwanza niliyefanya naye kolabo kwa hiyo tumeishi kuwa marafiki. Najua ni vyema kurudi nyuma na kufanya kazi nyingine lakini wasanii ni wengi kwa sasa na ni poa kuwapa wengine nafasi. Kwa hiyo, watu wasikae kitako eti wakategemea kuna kolabo inakuja kati yetu, hapana haipo,” kakata kauli sanaipei Tande.
Sanaipei aliyetimiza miaka 39, mwezi uliopita (Machi 2024) anasema wawili hao huwa wanakutana mara kwa mara.
“Tulikuwa tunajienjoi tu, tukutane tupige picha, tule maisha,” anasema.
Sababu za Sanaipei kutokuwa na uhakika wa kutokea kwa kolabo nyingine na Jua Cali ni kuwa mara nyingi yeye ndiye hushirikishwa.
“Mara nyingi mimi ndiye hushirikishwa kwenye ngoma za wasanii. Mimi ninapokuwa nikiandika wimbo mara nyingi huwa siandiki nikiwa nawaza msanii mwingine atakuja atie vesi au korasi, huwa naandika nikijua ni mimi ndiye nitakayeishia kuimba,” anasema.
Na kwa wachache waliobahatika kufanya kolabo naye, Sanaipei anasema ni kwa sababu walikidhi vigezo anavyovienzi yeye.
“Mwanzo ili tufanye kolabo lazima mashairi yako yawe na mada sio kula siku wimbo za kupati. Lakini pili, lazima uwe na talanta, kwamba unaweza kupiga shoo za laivu na bendi na sio mambo ya kusafisha sauti studio na auto-tunes. Mimi napiga laivu na bendi, sasa kama wewe huwezi tutafanyaje kolabo maana ukitakiwa kupiga laivu hautaweza,” Sanaipei anasisitiza.
Kwa zaidi ya miaka 10, Sanaipei alikuwa akiandaa shoo za laivu bendi za karaoke hadi alipoamua kuachana na shughuli hiyo.