Akili MaliMakala

Udongo wa Kenya kupigwa msasa kuboresha kilimo

Na SAMMY WAWERU May 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI inaendeleza zoezi la kuchukua sampuli za udongo kote nchini kwa lengo la kuboresha afya ya udongo wa Kenya, ili kunogesha kilimo.

Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO) linaendesha zoezi hilo, na linasema kuwa hatua hiyo itawawezesha wakulima kupata ushauri nasaha sahihi kuhusu pembejeo za kilimo, hasa fatalaiza.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo ya Kiserikali, Dkt Eliud Kireger, katika mahojiano na waandishi wa habari jijini Nairobi, alisema kuwa mpango huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.

Alielezea kusikitishwa kwake na suala la afya ya udongo kupuuzwa kwa muda mrefu, hata wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kushuhudiwa.

Sampuli za udongo kwenye maabara. Picha|Sammy Waweru

“Suala la afya ya udongo limepuuzwa kwa muda mrefu sana, na kwa sasa, KALRO inaendelea kukusanya sampuli za udongo kote nchini ili kupigwa msasa,” Dkt Kireger alifichua.

Ingawa hakudokeza bajeti ya mradi huo, alisema kuwa zoezi hilo linafadhiliwa na Benki ya Dunia, ndiyo World Bank. Aidha, shughuli hiyo inaendeshwa katika kaunti zote 47.

“Tunakusudia kukusanya karibu sampuli 77,000 kutoka kaunti zote 47,” Dkt Kireger alisema. Wataalamu wamekuwa wakitoa ushauri nasaha jinsi ya kuboresha shughuli za kilimo, ila kulingana mkuu huyo wa taasisi ya utafiti nchini, ukosefu wa maarifa kuhusu afya ya udongo unatishia jitihada za uzalishaji chakula.

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), Dkt Eliud Kireger. Picha|Sammy Waweru

Dkt Kireger anasema mbinu inayotumika kukusanya udongo, ni ya kidijitali. Ni mfumo ambao utawezesha wataalamu kujua pembejeo faafu, hasa mbolea, katika eneo lengwa.

“Kupitia mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa udongo, tutaweza kubaini aina ya fatalaiza au mbolea ambayo mkulima anapaswa kutumia, pamoja na mimea inayofaa kulimwa shambani mwake,” alifafanua.

Hatua ya kubaini afya ya udongo, itasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula nchini – hasa wakati huu ambapo serikali inaendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na uhaba wa chakula na njaa.

Shamba lenye maharagwe asilia aina ya minji. Picha|Sammy Waweru

Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 60 ya udongo wa Kenya umeharibika, kutokana na matumizi ya kupindukia ya pembejeo zenye kemikali za kilimo, haswa fatalaiza na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa ya mimea.

Pembejeo zenye kemikali hufanya udongo kuwa na asidi kupita kiasi. Kwa sasa, serikali inasambaza fatalaiza kwa bei nafuu kwa wakulima kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea, ulioanzishwa mapema 2023.

KALRO inaripoti kuwa, kufuatia mvua nyingi na mpango wa ruzuku ya mbolea, uzalishaji wa mahindi mwaka jana, 2024, ulifikia magunia milioni 60 ya kilo 90 kila moja, kutoka wastani wa magunia milioni 41 yaliyokuwa yakivunwa katika miaka ya awali. Kuongezeka kwa uzalishaji huo pia kumechangiwa na juhudi za serikali kupambana na usambazaji wa mbegu ghushi.

Shamba lenye mahindi. Picha|Sammy Waweru