Uendeshaji kasi wa magari ya miraa waanza kukemewa familia zikipoteza wapendwa
Na GITONGA MARETE
MADEREVA wanaoendesha magari ya miraa kwa kasi ya aina yake katika Kaunti ya Meru wanaendelea kulaumiwa huku tabia hiyo ikizidi kusababisha ajali na kuangamiza maisha ya wengi.
Baadhi ya familia ambazo zimewapoteza wapendwa wao na wanasiasa wanataka madereva hao wahukumiwe vikali kisheria kwa kuwa wengi wao huwa hawazingatii sheria za trafiki.
Kinaya ni kuwa wanapopita katika baadhi ya vituo vya kibiashara kati ya Maua, Meru hadi Nairobi, makundi ya vijana huwashangilia katika kile ambacho kinalinganishwa na mbio za Safari Rally.
Kwa familia ya marehemu Joanina Kainda, hawatawahi kusahau jinsi ambavyo maisha yao yalibadilika ghafla kutokana na tabia hiyo ya waendeshaji wa magari ya miraa.
Mnamo Novemba 20, 2020 saa kumi na moja jioni, Bi Kainda alikuwa amekamilisha mchango wa pesa za kugharimia matibabu ya mumewe Jeremiah Kariithi aliyekuwa akiugua kansa ya utumbo.
Bw Kariithi alikuwa anastahili kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Kiirua, Kaunti Ndogo ya Buuri kwa gharama ya Sh40,000.
Alipoondoka mchangoni, alipanga kulipa pesa hizo keshoye ili mumewe afanyiwe upasuaji. Hata hivyo, aligongwa na gari la miraaa dakika chache baada ya kubebwa kwenye bodaboda ya Jackson Kobia katika kituo cha kibiashara cha Ngundune, Tigania Magharibi.
Bw Kobia aliaga papo hapo huku Bi Kainda akifa katika Hospitali ya Meru siku tatu baadaye. Katika mahojiano mnamo Februari 15, 2021 Bw Kariithi alimwomboleza mkewe kama mtu aliyekuwa akimtakia uhai kwa kupambana kuona amepata matibabu yaliyohitajika.
“Alikusanya watu na kuandaa mchango wa kunisaidia kufanyiwa upasuaji. Wakati wa ajali hiyo, alilia mtu aliyechukuwa pesa alizokuwa nazo akisema zilikuwa za matibabu yangu,” akasema Bw Kariithi wakati huo.
Wiki mbili zilizopita, bintiye Emily Makena alisema Bw Kariithi aliaga dunia mnamo Machi 2022 kutokana na kansa ya utumbo na msongo wa mawazo.
“Mamangu alipoaga dunia, babangu alikuwa ameathirika sana na akaomboleza kwa miezi kadhaa. Pengine mamangu angekuwa hai, babangu angeishi kwa miaka mingi. Kwa sasa sisi ni mayatima na tunapambana na maisha,” akasema Makena, 22, ambaye hana ajira.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Idara ya Trafiki Ukanda wa Mashariki, kumekuwa na ajali 16 ambapo watu hugongwa na magari ya miraa kati ya Maua na Embu.
Watu 11 wameaga dunia katika ajali saba kati ya idadi hiyo. Mbunge wa Tigania Magharibi, Dkt John Mutunga, amesema kama kiongozi, hataketi na kutazama tu watu wakiaga dunia kwa kugongwa katika ajali za magari ya miraa.
“Haya ni mauaji kwa sababu madereva hao hawafuati sheria za trafiki. Maderava hao wanastahili kujibu mashtaka ya mauaji,” akasema Bw Mutunga. Msukumo wa kuwaadhibu madereva hao umechochewa tena na mauti ya Isaiah Mwega, mwalimu wa shule ya msingi ambaye aligongwa na gari la miraa katika kituo cha kibiashara cha Kianjai miezi mitano iliyopita.
Ajali hiyo ilikuwa mbaya kiasi familia yake iliathirika kisaikolojia baada ya kukusanya mwili wake ambao ulikuwa umegawanyika vipande vipande.
Kinaya ni kuwa vijana wa Kianjai husifia madereva hao wa miraa wakisema kuwa wana uzoefu katika uendeshaji magari na ajali hutokea tu kimakosa.