• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Ufisadi: Hofu mabilionea wa mafuriko waja ilivyokuwa wakati wa Covid-19

Ufisadi: Hofu mabilionea wa mafuriko waja ilivyokuwa wakati wa Covid-19

NA MWANGI MUIRURI 

TAIFA la Kenya huwa na sifa mbovu ya kuzalisha mitandao ya ufisadi na makateli wasiojali ambapo wao hujizolea mabilioni hata katika hazina za dharura za kushughulikia mikasa ya mauti kama mafuriko na magonjwa.

Ni katika hata hali za mauti na mahangaiko ambapo mafisadi hukimbia kunyakua misaada ya dharura kwa waathiriwa, wakiigeuza kuwa ukwasi wao wa kibinafsi.

Mara nyingi msumeno wa sheria huishia kuwa butu usioweza kumkata mfisadi yeyote.

Kumbukumbu za taifa zimejaa ushahidi tosha hata kwa wasio na ujuzi wa ukachero na ujasusi kwamba mafisadi wa kutajirika kutokana na majanga kama kansa, Ukimwi, malaria, na vita vya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 na 2008 wamejaa tele.

Kuna walionyonya hazina za kutuza mashujaa wa vita vya ukombozi wan chi vya Maumau na waliofyonza pesa za kuwafaa waliougua Covid-19 au kupoteza kazi shughuli nyingi ziliposimamishwa kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Lakini pia wengine wananenepa kutokana na mbolea ya ruzuku ambapo ama waliibadilisha wakaiuza au waliwauzia wakulima mbolea feki huku wakitembea huru bila kuwajibishwa kisheria.

Mafuriko sasa yakiwa ndio janga lililoko nchini tangu Aprili hadi mwezi huu wa Mei, hofu ni kwamba kutazuka kashfa ya uhepeshaji wa rasilimali za hazina za dharura zilizotengwa kuokoa hali.

Kufikia sasa mafuriko yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 200 na kufurusha zaidi ya 190,000 kutoka makwao na kuwa wakimbizi wa ndani.

Tangazo la Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti na Uadilifu wa Matumizi Bw Ndindi Nyoro linazua hofu hiyo ya ufisadi kutandazwa.

Mnamo Aprili 30, 2024, akiwa katika kambi ya wakimbizi wa mafuriko ya Ngutu iliyoko katika eneobunge la Mathioya ambapo wahasiriwa 54 walionusurika mauti kufuatia maporomoko ya ardhi yalipokumba kijiji cha Kiganjo na kusababisha vifo vya watu saba, Bw Nyoro alitoa idhini ya kipekee.

“Natangaza ya kwamba idara zote za serikali zitumie pesa kuokoa hali pasipo kujali bajeti. Zile pesa zote ambazo mmepewa za kushughulikia hali hii ya dharura mzitumie zote na ikiwa hazitoshi, basi mzidishe matumizi hata yasiyo kwa bajeti. Mtatafuta idhini ya bunge baada ya matumizi,” akasema Bw Nyoro.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro (kulia) ambaye kauli yake ina utata. PICHA | MWANGI MUIRURI

Bw Nyoro hata hakutoa ilani yoyote kwamba mwanya huo usitumike na walafi kupora rasilimali, akisema tu kwamba “mkileta maombi yenu Bungeni kuhalalisha matumizi, tutawasaidia kupiga muhuri gharama hizo”.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah ametaja idhini hiyo kama hatari na iliyo na uwezo wa kuunda mabilionea wa mafuriko.

“Kuna kanuni na utaratibu wa matumizi ya pesa zote za umma. Msingi ni uadilifu na nidhamu katika kuwajibikia utawala bora kuratibu rasilimali,” akasema Bw Omtatah.

Bw Omtatah alisema taifa hili liko na historia mbovu ya maafisa wa serikali kutekeleza bajeti kwa njia za kujinufaisha na badala ya kuwapa waathiriwa afueni, wanashibisha matumbo yao.

Aliyekuwa mwaniaji wa urais wa mwaka wa 2013 Bw Peter Kenneth ameteta kwamba “yale tumeshuhudia katika taifa hili ni makubwa kiasi kwamba tangazo la Bw Nyoro linazua kiwewe”.

“Shida kuu ni kwamba, hata wakati imebainika waziwazi kwamba kashfa imetandazwa, vitengo vyetu vya kisheria huzidisha usingizi wa pono,” akasema Bw Kenneth.

Akiongea na Taifa Jumapili kwa njia ya simu, Bw Kenneth alisema kwamba “hata hadi sasa hatujaondoka kwa kashfa ya mbolea feki ambapo tunangojea tendo la haki halafu tunapisha mwanya wa mabilionea wa mafuriko”.

Alisema bajeti ya dharura huwa ni asilimia mbili hadi tano ya bajeti za idara na hizo sio pesa kidogo kwa kuwa ni kati ya Sh70 bilioni na Sh150 bilioni ambazo ukiongeza idhini ya kutumia pasipo kuzingatia uhalali wa wakati kuhusu bajeti, hazina hiyo inaweza hata ikawa Sh1 trilioni.

“Huko ni kuchezea shilingi katika shimo la choo… ni sawa na kusinzia ukichunga minofu karibu na himaya ya fisi na katika hali zote mbili, tunachuuza rasilimali kwa wezi,” akasema Bw Kenneth.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kukusanya maji ya mvua yatumike wakati wa kiangazi

Safisha nywele: Wigi si za kuficha nywele chafu, upara

T L