UFUGAJI: Ni chakula kipi bora kwa ng'ombe wa maziwa?
Na SAMMY WAWERU
UKIZURU mashambani wakazi wengi hufuga ng’ombe.
Hata ingawa mijini kuna wachache wanaofuga, ni wenye vipande vikubwa kidogo vya ardhi ikizingatiwa kadhia mi.
Ng’ombe wanafugwa kwa minajili ya maziwa na nyama. Pia, ngozi yake hutumika katika uundaji wa bidhaa kama vile viatu, mishipi, mikoba, na zingine zinazotengenezwa kwa ngozi.
Uzalishaji wa maziwa ndiyo sababu kuu ya kuwafuga, ambapo kando na faida yake kiafya, pia yanaletea mkulima faida kimapato pamoja na ushuru kwa serikali.
Uzalishaji wa maziwa kwa wanyama hawa unategemea vigezo kadha wa kadha; lishe, maji, usafi na matibabu.
Kulingana na wataalamu wa mifugo, kinacholeta tofauti kati ya wanaopata maziwa mengi na kiduchu ni lishe wanayopewa ng’ombe.
Wanahoji ili uzalishaji uwe wa kuridhisha, mkusanyiko wa vyakula mbalimbali hasa vyenye ukwasi wa virutubisho vya kutosha unahitajika.
Wafugaji wengi wana mazoea ya kulisha mifugo majani mabichi-yenye unyevunyevu wa maji, na kulingana John Momanyi kutoka Sigma Feeds – kampuni ya kutengeneza chakula cha mifugo – hii ni mojawapo ya sababu kuu ya ng’ombe kutozalisha maziwa ya kutosha.
Anasema majani ya aina hiyo yana maji ya ndani kwa ndani, na ambayo hufanya mifugo wa maziwa kutokuwa na hamu ya kunywa maji.
Bw Momanyi, mtaalamu wa mifugo na msimamizi wa mauzo Sigma Feeds, anaendelea kueleza kwamba uundaji wa maziwa unategemea kiwango cha maji anayokunywa ng’ombe.
Ili azalishe kiwango cha maziwa ya kuridhisha, anasema hakuna njia ya mkato ila kumlisha chakula kilichokauka ili kimpe motisha ya kunywa maji mengi.
“Uundaji wa maziwa unategemea kiwango cha maji anayokunywa. Ng’ombe alishwapo chakula kilichokauka, huwa na ari ya kunywa maji mengi kwa sababu ya kuhisi kiu na ili chakula kisagige upesi. Maji yanasaidia pakubwa katika uundaji wa maziwa,” anafafanua mdau huyu.
Isitoshe, majani mabichi mbali na kupunguza kiwango cha maziwa yanatia mifugo katika hatari ya kuugua.
“Majani mabichi husambaza magonjwa upesi. Wadudu wanaoyategemea ng’ombe wakiyala ni hatari katika afya yao,” anatahadharisha mdau huyu.
Wanaokuza ndizi utawaaona wakilisha ng’ombe wao kwa migomba, na kulingana na wataalamu hii ni hatari katika afya zao mbali na kushusha kiwango cha mazao.
Iwapo hulisha mifugo wako kwa nyasi aina ya Nepia, Bracharia, Boma Rhodes., unahimizwa kuzikausha kabla ya kuwapa.
“Unaweza ukazifanya Hay au Silage, ili kuepuka changamoto ibuka,” anashauri Bi Agnes Omingo, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa kaunti ya Kajiado.
Licha ya hayo, mlo kamilifu ni suala muhimu zaidi kuzingatia katika ufugaji.
Kulingana na Agnes ambaye ana tajiriba zaidi ya miaka 20 katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, wanahitaji chakula chenye madini kamilifu.
Awali, mfugaji huyu alikuwa akizalisha kiwango kidogo cha maziwa lakini alipogundua siri ni kujitengenezea chakula uzalishaji wa zao hili kwake umenoga.
“Baadhi ya kampuni huandika kwenye mifuko ya chakula madini ambayo hawajayatia kwa minajili ya kufanya mauzo pekee. Nilipotambua hilo, hushirikiana na Sigma Feeds kujiundia chakula mwenyewe ambapo hunifadhili kwa madini yafaayo mbali na kuniuzia yaliyokamilika,” anaelezea.
Kauli yako inatiliwa mkazo na Sigma Feeds, ikieleza haja ya ng’ombe kulishwa chakula kamilifu kwa madini.
“Kufanikisha uzalishaji wa maziwa siri si nyingine ila kuzingatia madini kamili kwa chakula cha mifugo, pamoja na vigezo muhimu kwa wanyama,” anasema Bw John Momanyi.
Mlo wa mifugo wanaozalisha maziwa na nyama, unapendekezwa kuwa na zaidi ya asilimia 35 ya Protini.
Pia unapaswa kuwa na Vitamini, Wanga na Mafuta.
Madini mengine muhimu kuzingatia ni; Calcium, Chlorine, Magnesium, Phosphorus, Sodium (kwa chumvi) na Potassium.
Huu ni mkondo ambao pia unapaswa kuigwa na wafugaji wa mbuzi na kondoo.
Joseph Mathenge, mfugaji wa mbuzi wa maziwa Kiambu, maarufu kama Alphine, anasema huwalisha nyasi zilizokauka, ikiwa ni pamoja na chakula chenye madini kamili.
“Siri ya kupata maziwa ya kutosha ni kuwapa chakula kilichokauka, chenye madini kamili na maji kwa wingi,” anasisitiza Bw Mathenge.
Ni muhimu kutaja kuwa mifugo wanapaswa kukaguliwa kila wakati, na wanapoonyesha dalili za udhaifu waitiwe daktari kwa minajili ya matibabu.