Ufugaji nyuki wazima mioto ya Aberdares na kuleta riziki tamu
SHUGHULI za ufugaji nyuki katika maeneo ya kimkakati karibu na Msitu wa Aberdare zimepunguza kwa kiasi kikubwa mioto katika misitu na kuchangia uhifadhi wa mazingira huku zikitoa mapato ya kutosha kwa wakulima wa maeneo hayo.
Mpango huu umebadilisha uhusiano kati ya jamii na msitu, na kugeuza mienendo iliyotia wasiwasi hapo awali kuwa ushirikiano endelevu na wenye manufaa.
Kwa miaka mingi iliyopita, mioto ilikuwa tishio la mara kwa mara katika Aberdares, ikiharibu sehemu kubwa ya msitu na kuwaathiri wanyamapori.
Moja ya matukio mabaya zaidi yalitokea mwaka wa 2019 katika eneo la Kinangop, ambapo zaidi ya hekta 100 za msitu wa mianzi ziliharibiwa.
Moto mwingine mkubwa uliripotiwa Geta, eneobunge la Kipipiri mwaka huo huo, na kusababisha uharibifu sawa na huo.
Visa zaidi vya mioto viliripotiwa katika misitu ya maeneo ya Shamata, Ndaragua mnamo 2020 na 2021.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hakuna matukio makubwa ya moto ambayo yameripotiwa katika eneo la Aberdares, Kaunti ya Nyandarua, kutokana na kukumbatiwa kwa ufugaji nyuki.
Kuanzishwa kwa kilimo cha ufugaji wa nyuki katika msitu pia kumeongeza uzalishaji wa asali katika Kaunti ya Nyandarua.
Pato la kila mwaka limepanda kutoka kilo 500 hadi zaidi ya tani 20, na hivyo kusababisha serikali ya Kaunti ya Nyandarua kujenga kiwanda cha kuchakata asali katika soko la Ndunyu Njeru, Kinangop.John Gichuki, mkurugenzi msaidizi anayehusika na maendeleo ya mifugo Nyandarua, alihusisha ukuaji huu na uhusiano wa manufaa kati ya ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira.
“Ili ufugaji wa nyuki ustawi, uhifadhi ni muhimu. Kulingana na ongezeko la mahitaji ya mizinga ya nyuki, tunakadiria kuwa uzalishaji wa asali unaweza kufikia tani 50 ndani ya miaka mitano. Huu ni ushindi kwa wakulima kwani kuimarika kwake kunakuza uzalishaji wa chakula,” alisema.
Serikali ya kaunti hiyo imewahimiza wakulima kuunda vikundi, kuwezesha upatikanaji rahisi wa mafunzo, rasilimali na usaidizi.Katika kijiji cha Umoja Mbuyu, Ndaragua, mpakani na Kaunti ya Laikipia, kikundi cha Somar ni miongoni mwa vinavyokumbatia ufugaji wa nyuki.
Kikundi kilipokea mizinga 20 mnamo 2021 lakini hapo awali kilikabiliwa na changamoto ya kutoroka kwa nyuki kwa sababu ya uhaba wa maua.
“Hali iliimarika baada ya kuanzisha mazao ya malisho kama miti ya Sesbania, lupine na lucerne. Upanzi wa miti unaimarika taratibu, mashirika ya uhifadhi yametusaidia kwa miche ya kiasili na miparachichi. Mwaka jana, tulipanda zaidi ya miche 10,000 ya miti katika mashamba ya watu binafsi na maeneo ya umma kwa usaidizi kutoka kwa washirika kama Mpango wa Mazingira wa Kiangure Springs, Wakfu wa Dedan Kimathi na Huduma ya Misitu ya Kenya,” alisema Mwenyekiti wa Kikundi cha Somar Self-Help, Bw John Ndiritu.
Kikundi hicho ni miongoni mwa vinavyopangiwa kupokea vifaa vya kuvuna na kusindika asali kutoka kwa serikali ya kaunti hii, na hivyo kuwaongezea kipato. Chifu Msaidizi wa Muthiga, Bw Anthony Wamai alisema kuanzishwa kwa ufugaji nyuki kumerahisisha juhudi zake za kuhimiza utunzaji wa mazingira.
“Ufugaji wa nyuki umehamasisha jamii kulinda msitu, ambao sasa wanauona kuwa rasilimali muhimu. Sio tu kuhusu kuhifadhi mazingira tu bali pia kuunda maisha endelevu,” alisema.
Ufugaji wa nyuki pia umekumbatiwa na wamiliki wa ardhi ambao hawatumii mashamba yao. John Ndaire, ambaye anasimamia mizinga 300 ya nyuki karibu na Msitu wa Aberdare, alisema mradi huo umegeuza wavunaji asali haramu na wachoma mkaa kuwa wakulima halali.
“Ninasimamia mizinga ya nyuki ya wamiliki saba wasioishi hapa. Kwa kuwa msitu wa Aberdare huwa na majani mwaka mzima, wakulima huvuna asali mara tatu kila mwaka. Wale ambao hapo awali walivamia msitu huo kutafuta asali au kujihusisha na uchomaji makaa sasa wanaona ufugaji wa nyuki kuwa salama na wa kuaminika zaidi,” akasema Bw Ndaire.
Ushiriki wa jamii ya eneo hilo pia umeshughulikia moja ya sababu kuu za moto msituni. Mkuu wa Huduma ya Misitu, Kaunti Nyandarua John Njoroge alibainisha kuwa mioto mingi ilianzishwa na wavunaji asali haramu ambao mbinu yao mara nyingi ilihusisha kuchoma ili kuvuna asali.
“Kwa kushirikisha jamii katika ufugaji nyuki halali na endelevu, tumepunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya moto,” alisema.
Ili kuimarisha zaidi ufugaji wa nyuki, serikali ya Kaunti ya Nyandarua imezindua mpango wa upanzi wa tufaha wa Sh26 milioni.
Tufaha, ambazo huchanua maua mara mbili hadi tatu kila mwaka, hukamilisha juhudi za upanzi miti za eneo hilo na kutoa lishe ya ziada kwa nyuki.
“Wataalamu wetu waligundua kuwa tufaha ni bora kwa kusaidia ufugaji nyuki huku tukifikia malengo yetu ya kupanda miti. Ingawa hatuwezi kukidhi mahitaji makubwa ya mizinga ya nyuki, tumetoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo kutengeneza mizinga ya kibiashara, kuwezesha wakulima kununua kibinafsi. Hii ni kuunda fursa za biashara na kukuza uhifadhi,” alisema Gavana Kiarie Badilisha.
Mpango wa ufugaji nyuki sio tu wa kupunguza uchomaji moto misitu lakini pia kubadilisha mazingira ya kijamii na kiuchumi ya kaunti.
Jamii ambazo hapo awali ziliuona msitu kama rasilimali ya kufyonza sasa zinauona kama mshirika katika ustawi endelevu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA