Makala

Ufugaji nyuni unavyompa kijana riziki

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER CHANGTOEK

TITUS Kiptoo, 27, alijitosa katika ufugaji wa mabatamzinga kama uraibu, lakini baada ya kuona faida ambayo ndege hao wanayo, akaamua kujitosa kikamilifu na kama njia ya kujipa riziki.

“Nimekuwa nikiwafuga mabatamzinga kwa muda sasa. Nilipata hamu ya kuwafuga mabatamzinga baada ya kumtembelea rafiki yangu katika mtaa wa Elgon View mjini Eldoret. Alinijuza kuhusu faida zao na punde, nikaanza kuwapenda. Niliwanunua mabatamzinga wawili wa kike kwa Sh3,000 kila mmoja, na nikamwazima mmoja wa kiume, ambaye aliniuzia baadaye,’’ afichua Kiptoo, ambaye mbali na ufugaji wa mabatamzinga, huwafuga mabatabukini na kanga pia.

Mkulima yuyo huyo anaongeza kwamba mnamo mwaka uliopita, alipokuwa amekuja jijini Nairobi kwa ajili ya masomo zaidi, akaishi na amu yake aliyekuwa akiishi karibu na jirani ambaye alikuwa akiwafuga ndege mbalimbali kama vile mabatamzinga, mabatabukini na kanga.

Punde si punde, akawa na hamu na ghamu ya kuwafuga kanga. “Mnamo Desemba mwaka 2018, akanipa vifaranga wanne wa kanga, ambao walikuwa na umri wa wiki moja. Kwa sadfa, mmojawapo wa mabatamzinga wangu alikuwa ameangua vifaranga, na nikampa na alikubali kuwachukua na kuwafuga pamoja na vifaranga wake,’’ adokeza mkulima huyo.

Kiptoo anaongeza kuwa alijitosa katika ufugaji wa mabatabukini majuma mawili yaliyopita. Kwa wakati huu ana mabatabukini watatu wa kike na mmoja wa kiume. Anaongeza kuwa hivi karibuni wataanza kuyataga mayai na kuangua vifaranga.

“Mwanzoni, nilianza kuwafuga kama uraibu, lakini baadaye wakati kuhitajika kwao kulipozidi, ndugu yangu mdogo, aitwaye Mark, pamoja nami tukaamua kuwa huo ni uga tungejipatia riziki kutokana nao. Tukaamua kuongeza idadi yao, na muda si muda, tukawa na mabatamzinga thelathini,’’ asema, akiongeza kuwa kwa wakati huu, wao wana mabatamzinga ishirini wa kike na watatu wa kiume.

Aidha, mkulima huyo, ambaye ana shahada katika masuala ya Usimamizi wa Wanyamapori, kutoka katika Chuo Kikuu cha Eldoret, na ambaye pia anasomea stashahada ya Usimamizi wa Ushuru katika chuo cha Kenya School of Revenue Administration, anasema kuwa yeye pia ana kanga wanne waliokomaa, na vifaranga thelethini na wanne wa kanga.

Kiptoo, ambaye alihitimu na kukabidhiwa shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori Chuoni Eldoret mnamo mwaka 2016, anafichua kuwa bei ya batamzinga aliyekomaa ni kati ya Sh3,000 na Sh4,500. Hata hivyo, bei hizo hutegemea jinsia za ndege hao na umri wao.

“Lakini sisi huwauza vifaranga wa mabatamzinga wenye umri wa siku moja kwa bei ya Sh300 kila mmoja. Vifaranga wa kanga wenye umri wa siku moja pia huuzwa kwa Sh300 kila mmoja,’’ aongeza Kiptoo.

Mkulima huyo anasema kwamba, kwa sababu ya bei za juu za lishe za ndege, wao hijitengenezea lishe za ndege wao. Wao huchanganya mahindi, ngano na samaki waliosagwa. Huwalisha asubuhi na kuwafungulia kutembeatembea wakijitafutia lishe nyinginezo.

Yeye anafichua kwamba kanga na mabatabukini hustahimili magonjwa mengi, ilhali mabatamzinga aghalabu huathiriwa na maradhi kama vile Fowl pox na blackhead.

Kwa mujibu wa mkulima huyo, batamzinga mmoja huyataga jumla ya mayai kati ya 10 na 20 kabla hajaanza kuatamia mayai hayo, na wao ni bora kwa shughuli ya kuyaatamia mayai.

Titus Kiptoo akiwa na kaka yake. Picha/ Peter Changtoek

“Mimi huwatumia (mabatamzinga) kuyatotoa mayai ya kanga. Kwa upande mwingine, kanga huyataga mayai mengi, kabla hawajaanza kuatamia mayai. Wangu walianza kutaga mayai kuanzia mwezi Juni, walipokuwa na umri wa miezi sita, na hawajaacha kutaga hadi sasa,’’ afichua Kiptoo, ambaye hukiendesha kilimo hicho katika kitongoji cha Merewet, umbali wa kilomita 20 kutoka mjii Eldoret, katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Mkulima yuyo huyo, anasema kwamba wateja wake hutoka sehemu tofauti tofauti nchini, mathalani maeneo ya Narok, Kisumu na Nairobi.

Mojawapo ya changamoto ambazo mkulima huyo amepitia ni mbwakoko ambao huwavizia na kuwala ndege wake.

“Mabatamzinga na kanga hupenda sana kutembeatembea, na mbwakoko huwavamia. Kuna wakati ambapo niliwapoteza mabatamzinga kumi kwa siku moja, walioliwa na mbwakoko,’’ asema.

Anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika shughuli ya ufugaji wa mabatamzinga, mabatabukini na kanga kujua kuwa ni sharti kuwe na subira ili wawe na fanaka.

Huku akishikilia kikiki kwamba kilimo hicho kina faida, mkulima huyo anafichua kuwa anaazimia kuongeza idadi ya ndege wake ili achume zaidi kutoka kwao.