Makala

UFUGAJI: Usagaji wa majani unaepushia mifugo athari za wadudu na magonjwa

September 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MBALI na kuwa mkulima wa matunda, mboga, majanichai, kahawa na viazi vikuu, Apollo Maina ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Shamba lake lililoko eneo la Kigumo, kaunti ya Murang’a, ameligawanya kiasi kwamba lina sehemu kukuza nyasi maalum aina ya nepia.

“Pia hulisha ng’ombe wangu kwa majani ya sukuma wiki, kabichi na spinachi,” asema Bw Maina. Nyasi, majani ya mboga, na mihindi, ni kiini kizuri cha Vitamini kwa mifugo.

Ili kupata mazao ya kutosha na yenye hadhi, mfugaji anahimizwa kuhakikisha mlo anaowapa mifugo wake ni kamilifu, yaani una madini faafu.

Mbali na Vitamini, Protini, Wanga, Mafuta, madini kama vile Calcium na Phosphorus ni muhimu katika kuimarisha afya ya mifugo.

Mifugo wanafugwa kwa minajili ya maziwa na nyama.

Nyasi zinazoshabikiwa na ng’ombe ni Nepia, Boma Rhodes, Lucerne na Desmodium.

Wataalamu wanaonya kuwa si salama kulisha mifugo nyasi ambazo hazijasagwa. Baadhi ya wafugaji wana mazoea ya kuzivuna na kulisha ng’ombe moja kwa moja.

“Ni muhimu kuzikatakata au hata kuzisaga kwa mashine ili kuepushia mifugo wadudu wanaojiri na nyasi,” ashauri Dkt John Muchibi wa kutoka Elgon Kenya, kampuni inayotoa huduma za kilimo na ufugaji.

Kulingana na mdau huyu, haja ipo nyasi ziruhusiwe kukauka ili kuondoa wadudu na magonjwa yanayoziathiri.

“Majani mabichi yana changamoto nyingi hasa zile zitokanazo na wadudu na magonjwa,” aonya Dkt Muchibi.

Anaeleza kwamba nyasi zilizokauka huwapa ng’ombe motisha kunywa kwa wingi. Maji ni kiiungo muhimu katika uundaji wa maziwa.

Hay ni nyasi zilizokaushwa ili kutoa unyevuunyevu wa maji, ilhali Silage ni zilizohifadhiwa kwa muda fulani bila kukaushwa. Aidha, Silage huwa na uchachu unaofurahiwa na mifugo.

Kuna mashine tofauti zinazotumika kusaga nyasi au majani, mfano Chaff Cutter, mashine ya kuunda Silage, Hay Cutter na Crusher.

Amos Njane kutoka Thika Coffee Machinery Ltd, kampuni inayounda mashine hizo anasema huuzwa kulingana na matumizi yake. Pia, anasema kuna zinazotumia mafuta ya petroli na nguvu za umeme. Aidha, zinagharimu kati ya Sh30,000 hadi Sh100,000.