Ufugaji wa kuku wa mayai kisasa
MWAKA wa 2013, Teresiah Gathii alikata kauli kwamba wanawe hawataendelea kupitia changamoto za malezi kupitia yaya.
Isemavyo, uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi, Teresiah aliamua kuacha kazi ya kuajiriwa ili azamie kulea malaika wake.
Alikuwa ameajiriwa kama mshauri wa bidhaa za kujipodoa na urembo katika kampuni moja Jijini Nairobi.
“Kupata yaya mwaminifu na atakayekulelea watoto si rahisi,” Teresiah anasema.
Hakuwa anakosa kuskia malalamishi kutoka kwa wanawe, jinsi walivyohangaishwa na ‘mlezi’ wa muda.
Shinikizo la kujilelea vitoto vyake lilichochewa na mavyaa – mama wa mumewe.
“Mavyaa ni mfugaji kuku, na alinihimiza nijilelee watoto akinihakikishia nikifuata nyayo zake kamwe zitajutia,” anaelezea.
Mwaka huohuo alioacha kazi, 2013, Teresiah aliingilia ufugaji wa kuku wa mayai.
Alianza na kuku 1, 000 pekee. “Kwa ushirikiano na baba watoto, tuliwekelea Sh250, 000, mtaji, kuanza kufuga kuku.”
Fedha hizo zilitumika kuunda vizimba ambavyo vilikuwa vya mbao.
Hata ingawa utangulizi haukuwa mteremko, Teresiah anadokeza alianza kuridhia kazi hiyo ya kujiajiri.
Miaka 12 baadaye, mama huyu ana kila sababu ya kutabasamu kutokana na hatua alizopiga mbele kimaendeleo.
Mosi, kando na kuona kuwa wanawe wanalelewa chini ya matunzo ya mama, kifedha ameimarika akilinganisha na mapeni aliyokuwa akilipwa.
Pili, historia ya waliojitolea mhanga kuhakikisha nchi ina bidhaa za kuku za kutosha ikiandikwa, Teresiah hatakosa kuwa kwenye orodha.
Kutoka kwa vizimba vya mbao, ameimarika na kuwa na vizimba vya kisasa (automated caging system).
Mama huyu anaendeleza ufugaji wa kuku wa mayai katika mtaa wa kifahari wa Thindigua, karibu na Mji wa Kiambu.
“Vizimba tunavyotumia vimepunguza upotevu wa nafasi,” anasema.
Kimoja, kinasitiri kuku 9, 000 na kingine, jumla ya 7, 500.
“Vyote huvijaza kwa kuku,” anadokeza. Ni uwekezaji wa teknolojia ya kisasa uliomgharimu mamilioni ya pesa.
Mbali na kuhakikisha nafasi iliyoko hasa maeneo ya mijini inatumika ipasavyo, automated caging system inadumisha kiwango cha usafi.
Kuku wanapoenda haja, kinyesi kinatekwa. Kinyesi hichohicho, kwa baadhi ya wakulima hutumika kama mbolea shambani.
Kigezo hicho kinasaidia kudhibiti msambao wa maradhi.
Kuku wanapotaga mayai, nayo yanakuwa salama kwani yanatekwa na vichungi cha nyaya zilizowekwa.
“Kizimba kimoja, kinatumia nguvu za umeme kusambaza chakula kwa kipimo na pia maji,” Teresiah akaambia Akilimali wakati wa mahojiano katika mradi wake Thindigua, Kiambu.
Ni teknolojia aliyotambua kupitia utafiti kuboresha ufugaji kuku.
“Isitoshe, kampuni inayonisambazia vifaranga imenifaa pakubwa kuelewa ufugaji kuku kitaalamu, kupitia mafunzo yake ya mara kwa mara. Ugonjwa unapolipuka, mavetinari wake huwa ange kuarifu wakulima,” Teresiah akaelezea.
Licha ya mama huyu kuandikisha maendeleo makubwa, anakiri utangulizi haukuwa rahisi.
Alipoanza, alikuwa mteja wa kuku wake kufariki kila wakati kwa sababu ya kutoelewa kuwatunza.
Anakumbuka mwaka 2015 ambapo alipoteza kuku zaidi ya 200, kupitia kero ya kudonana.
Kadhalika, mfumko wa bei ya chakula cha kuku hasa 2020 Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19, nusra uzime ndoto zake.
Teresiah, hata hivyo, sasa hujiundia malisho ya kuku.
Ana mashine mbili za shughuli hiyo; kusaga na kuchanganya malighafi.
“Chakula kingi cha madukani hakijaafikia ubora wa bidhaa, na kilichotimiza, bei yake haikamatiki. Hata hivyo, hatua ya kujitengenezea niliyochukua imenishushia gharama pakubwa,” anafafanua.
Kreti moja ya mayai bei yake huchezea kati ya Sh200 hadi Sh350, ambayo huuzia wanunuzi wa kijumla.
Bei hiyo, hata hivyo, inalingana na msimu, akilalamikia uwepo wa mayai kutoka nchi jirani huharibu bei ya wafugaji wa Kenya.
Kuku wanapofikisha umri wa kushusha ari ya utagaji, Teresiah huwauza Sh350 hadi Sh400, kila mmoja kwa wanunuzi wa kijumla.