Ugumu wa kupambana na wezi wa mananasi Del Monte
NA MWANGI MUIRURI
WADAU wa vitengo vya usalama Kaunti ya Murang’a wamefichua kwamba kibarua cha kupambana na wezi wa mananasi katika shamba la kampuni ya Del Monte si rahisi kama inavyodhaniwa.
Wamefichua kwamba genge la uovu huo ni kama “serikali kivyake”.
Linafananishwa na kundi haramu la Mungiki.
Inadaiwa wanachama wa genge hilo wana machungu na hudai shamba hilo la Del Monte ni la mababu wao na kwa msingi huo, wanafaa kupata riziki kutokana na harakati za kampuni hiyo ambayo ni ya Kimarekani.
Tayari, kuna kesi mahakamani ya kuitaka kampuni hiyo kutoa ekari zisizopungua 8,000 kwa majirani wake wa maeneobunge ya Gatanga, Kandara na Ithanga.
Walalamishi wanadai wao ndio walipokonywa mashamba ndipo kampuni hiyo ikapata nafasi ya kufanya biashara Murang’a.
Magenge hayo pia huendeleza madai kwamba uwepo wa kampuni hiyo ni urejeo wa ukoloni uliotimuliwa mwaka wa 1963 wakati Kenya ilijipa uhuru.
Aidha magenge hayo hujifananisha na vuguvugu la Maumau lililopambana na wabeberu.
Siku za nyuma, Del Monte ilikuwa ikiajiri walinzi kutoka mitaa ya karibu.
Lakini madai yaliibuka walinzi walikuwa wakiua magenge hayo ya wizi katika vita kamili na hivyo basi kuzua visa vya miili kupatikana katika mito, vichaka na mabwawa ya eneo hilo.
Miili hiyo ilikuwa ikitambulika kama ya vijana wa eneo hilo na mingine ikiwa ni ya walinzi wa Del Monte kuashiria yalikuwa ni makabiliano makali.
Kufuatia mauti hayo, serikali ya Kenya imeshtakiwa katika Mahakama Kuu ya Thika ikitakiwa kutoa ratiba ya kumaliza visa vya ukiukaji wa haki za binadamu huku nayo Del Monte ikijipata katika marufuku ya soko la bidhaa zake kimataifa, ikishinikizwa kuimarisha uhusiano na utu.
“Hao si wezi wa kawaida mtaani. Ni wezi ambao huwa wamejipanga na huwa na usaidizi wa hata maafisa wafisadi katika vitengo vya usalama. Isitoshe, baadhi ya wafanyabiashara ambao hununua mananasi hayo hufadhili genge hilo,” yasema ripoti ya ukadiriaji hali ya usalama iliyoandaliwa na kamati ya usalama eneo hilo mnamo Machi 3, 2024.
Ilifichua kuna makateli ndani ya Del Monte ambayo hufanikisha wizi huo.
Ripoti hiyo inasema kwamba hali ni mbaya katika wizi huo kwa kuwa ukadiriaji wa pato la genge hilo kwa mwezi huwa ni Sh10 milioni.
“Wezi huuza mananasi hayo pindi baada ya kuyaiba ambapo wafanyabiashara huwa wamewategemea magari yao kandokando ya barabara ya kutoka Thika kuwenda Murang’a na Nyeri,” ripoti hiyo yasema.
Kamati ya usalama Kaunti ndogo ya Gatanga iliandaa ripoti mwaka 2022 kwamba “hao wezi ni genge ambalo limekita mizizi na husaidiwa na washirika wengi”.
Iliandaliwa na aliyekuwa kamanda wa polisi na mwenzake wa uchunguzi wa jinai, Peter Muchai na John Kanda mtawalia.
Ripoti yao ilisema kwamba walinzi wa Del Monte huvamiwa usiku wa manane na zaidi ya vijana kama 100 wakiwa wamejihami kwa silaha butu kama mapanga, shoka na mishale pamoja na mikuki.
“Mijibwa ya walinzi inapoachiliwa, vita kamili huzuka ambapo huishia mauti na majeruhi,” ripoti yao ikasema.
Ripoti hiyo ilisema Del Monte nayo huchochea wizi huo kwa kukataa kuweka ua kukinga mananasi hayo ambayo kwingine hata huwa kando mwa barabara za umma ndani ya shamba hilo.
Huku Del Monte ikiwa kwa sasa imefuta walinzi wake wote 270 kama hali ya kutii shinikizo la soko kwamba ilinde haki za binadamu, imekabidhi jukumu hilo kwa maafisa wa usalama wa kampuni ya G4S.
Lakini wengi wanahofia kwamba changamoto ya ujambazi huo haitarajiwi kuisha kwa wepesi.
“Tunaongea kuhusu vijana ambao hujipa riziki kupitia wizi wa mananasi hayo ya Del Monte. Kuwaambia vijana hao wakome haitakuwa rahisi. Ni vijana ambao huwa wameamua kwamba heri wafe wakijaribu kujipa riziki hiyo ya kiharamu,” akasema mwanamume mmoja wa eneo hilo aliyekataa kutajwa jina kwa sababu za kiusalama.
Alidai kuwa inakadiriwa kijana mmoja katika genge hilo huingiza Sh3,500 ambapo akitoa gharama za mafuta ya pikipiki, hongo kwa baadhi ya polisi na baadhi ya walinzi wa Del Monte, pato lake la haramu halipungui Sh2,000.
Alisema kwamba mikutano ya maafisa wa usalama ilibaini kwamba wakati magenge hayo yamesakamwa na polisi na kuzimwa kuiba mananasi, huwa yanajigeuza kuwa magenge ya kuvamia magari ya uchukuzi na ya kibinafsi katika barabara ya Thika-Kenol.
Kamanda wa Polisi Murang’a Kainga Mathiu alisema wameunda kamati za kukabili wizi huo baada ya kung’amuliwa kwamba shida hiyo ni hatari hata kwa uchumi wa taifa.
Del Monte hutoa ajira ya watu 2,800 moja kwa moja na kwa wengine zaidi ya 30,000 kupitia ushirika wa kibiashara kando na kutumia zaidi ya Sh4 bilioni kwa mwaka kupitia ununuzi wa bidhaa za kutumika katika harakati zake.
“Tumeamua kwamba magenge hayo yote ya wizi wa manasi lazima yatokomezwe ili Del Monte iendelee kuwa kiungo thabiti cha uchumi wa nchi na wa kaunti. Tutadhibiti genge hilo lisiibe mali ya Del Monte na pia lisitatize watu barabarani au mitaani,” akasema Bw Mathiu.
Bw Mathiu aliwataka wanasiasa wakome kutoa matamshi ambayo yanaashiria kuunga mkono genge hilo.