Ujenzi wa hospitali mpya mjini Ruiru waendelea
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Ruiru watapata afueni mara itakapokamilika hospitali mpya inayojengwa eneo hilo.
Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema hospitali hiyo inayojengwa kutumia teknolojia ya kisasa itakuwa na vitanda 150.
Alisema itakuwa tayari Disemba 20, 2020, na itawafaa watu wengi katika eneo hilo.
“Tunajua vyema kuwa mji wa Ruiru una idadi kubwa ya wakazi na kwa hivyo ile hospitali moja ya Ruiru Level 4, haiwezi kuhudumia wakazi wa hapa. Sasa tumeongeza hospitali nyingine kando ya hiyo ambayo itakamilika kwa muda wa miezi miwili pekee,” alisema Dkt Nyoro.
Alisema vifaa vinavyotumika kuijenga ni vya kiteknolojia na ndiyo maana itakamilika haraka.
Alisema gharama ya kujenga hospitali hiyo ni takribani Sh65 milioni.
“Kuna hospitali zingine mbili za Karatu na Lari ambazo zitafanyiwa ukarabati na kuwekwa vifaa vya kisasa ili ziweze kuhudumia wakazi vilivyo,” alisema Dkt Nyoro.
Aliyasema hayo mnamo Jumamosi alipozuru katika hospitali ya Ruiru Level 4 kujionea ujenzi wa kitengo kipya kinachokaribia kukamilika.
Alitoa mwito kwa wakazi wa Kiambu kwa jumla wawe makini na wasikubali kutembea mitaani bila barakoa.
“Homa ya corona ni mbaya na ni lazima tukabiliane nayo vilivyo. Homa hiyo imerudi na nguvu katika awamu ya pili hivyo ni lazima tuchukue tahadhari,” alisema gavana huyo.
Alisema sehemu wanakostahili kuwa makini sana ni katika masoko, vituo vya matatu, madukani na katika maeneo ya burudani.
Alipongeza maafisa wa polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kukabiliana na watu wanaokiuka sheria za kuzuia kuenea kwa Covid-19.
Alisikitika watu wengi wanachukulia jambo hilo kwa mzaha licha ya kwamba “mmeona watu wanaendelea kufariki kwa wingi.”
“Kaunti ya Kiambu inazidi kuripoti zaidi ya watu 30 wanaoambukizwa corona kwa siku jambo ambalo ni hatari kwa usalama. Ni vyema kila mmoja wetu ajaribu kufuatilia masharti yote yaliyowekwa na Wizara ya Afya,” alifafanua gavana huyo.
Alisema tayari hospitali ya Tigoni imewalaza wagonjwa wapatao 60 wa Covid-19 ambapo 30 wako kwenye mashine za oksijeni.
Alisema Kiambu itazidi kukabiliana na janga hilo hadi dakika za mwisho na kwa hivyo wananchi nao wakubali kushirikiana na kaunti hiyo kwa kukabiliana na corona.