• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Ukeketaji huamsha moto wa wasichana na kuwaharibu zaidi – Mwanaharakati

Ukeketaji huamsha moto wa wasichana na kuwaharibu zaidi – Mwanaharakati

NA KALUME KAZUNGU

WANAODHANI kuwa ukeketaji huongeza maadili ya kitamaduni ya mwanamke na adabu, wamenoa.

Haya ni kulingana na mwanaharakati wa kijamii ambaye pia yuko mstari wa mbele kupiga vita tohara ya wanawake, Bi Zeinabu Gobu Wako aliyefichua kuwa ukeketaji hata unaamsha ‘moto’ wa wasichana na hata kuwaharibu zaidi.

Ukeketaji au tohara ya wanawake ni tendo la kukata sehemu za nje za viungo vya uzazi vya mwanamke.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bi Gobu, ambaye pia anatoka jamii ya wafugaji eneo la Witu,kaunti ya Lamu ambako tohara ya wasichana imekithiri, alisema ukeketaji katu haumzui mwanamke kulalalala na wanaume kama inavyodhaniwa.

Bi Gobu alisema kulingana na hali halisi ilivyo eneo lake la Witu, wasichana wengi waliopitia ukeketaji wamekuwa wakiendeleza ngono kiholela.

Alizitaka jamii zinazoendeleza tohara ya wanawake kwa kigezo cha kuwapunguzia hamu ya tendo la ndoa kutupilia mbali dhana hiyo kwani sivyo kabisa.

“Tohara ya wanawake ni uharibifu unaofaa kukemewa na jamii zote, serikali na mashirika. Kuna jamii zimeshikilia dhana kwamba ukeketaji huchangia maadili bora kwa akina dada. Hizo ni stori za abunuwasi. Kikweli ni kwamba wasichana wanaotahiriwa,hasa eneo hili la Witu ndio walio mstari wa mbele kuendeleza uhawara. Hiyo ina maana kwamba ukeketaji unachangia kuharibiwa kwa maadili hata zaidi. Tukemeeni na kutokomeza ukeketaji. Hakuna maana yoyote ya tohara ya wanawake,” akasema Bi Gobu.

Baadhi ya wazee wa jamii zinazoendeleza ukeketaji kisiri waliozungumza na Taifa Leo pia walikiri kutokuwepo kwa tofauti yoyote, hasa kitabia, kwa wasichana wanaopitia kisu cha ngariba na wale wasiotahiriwa.

“Zamani tuliamini kabisa kwamba punde msichana anapokeketwa basi anakuwa safi. Pia tuliamini inaongeza urembo hata zaidi. Tulichukukulia sehemu hizo za mwili zinazofaa kuondolewa ni najisi. Ila miaka ya sasa huo utamaduni umepitwa na wakati. Hata wasichana waliokeketwa eneo hili letu utapata wamepotoka kimaadili hata zaidi,” akasema Bw Khalifa Adan.

Ikumbukwe kuwa katika jamii nyingi, ambapo ukeketaji unafanywa,inachukuliwa kuwa ni mila ya kitamaduni, ambayo mara nyingi hutumiwa kama hoja ya kuendeleza ukatili huo.

Baadhi ya sehemu za Lamu ambako maovu hayo yamekuwa yakiendelezwa kisiri ni Witu Mjini, Koreni, Pangani, Mokowe, Dide Waride, Kitumbini, Chalaluma, Moa, Nairobi Area, Vipingoni, Onido, Pandanguo, Jima, Lumshi, Bar’goni, na viunga vyake.

Maeneo hayo ni ngome kuu za jamii za wafugaji, hasa Orma, Wasomali, Waborana, Waata (Watha) na Waboni.

Bw Khamis Lule alitaja tabia hizo kuwa zilizopitwa na wakati.

Kulingana na Bw Lule, wasichana wa umri mdogo wamekuwa wakishurutishwa kutahiriwa wakijua maeneo ya Witu,hasa punde shule zinapofungwa na  likizo kuanza.

“Wajua watoto wadogo hawana nguvu ya kujitetea. Na ndio sababu jamii zimekimbilia kuwafanyia tohara ya lazima,” akasema Bw Lule.

Alishikilia kuwa itikadi hiyo ya kukeketa wasichana iimekuwa ikichangia ndoa na mimba za mapema na ongezeko la idadi ya wanaoacha shule eneo hilo.

“Si ajabu kushuhudia hapa kwetu wasichana ambao punde wanapokeketwa inamaanisha wako tayari kuolewa na kuanza maisha ya utu uzima bila kujali umri wao. Wasichana wetu wengi waliotahiriwa hapa wameacha shule punde ilhali wengine wakiishia kuolewa. Lazima tabia hii ikomeshwe,” akasema Bw Lule.

Miongoni mwa athari za ukeketaji ni wahasiriwa kukumbwa na matatizo ya kisaikolojia, ikiwemo msongo wa mawazo, wasiwasi, kupata kiwewe baada ya kujifungua na kutojiamini.

Wahasiriwa pia hupata matatizo wakati wanaposhiriki tendo la ndoa wakati wamefunga pingu za maisha, ambapo mara nyingi huhisi maumivu, kutofurahia tendo na kutoridhika, yaani kutofika kileleni.

Kuna wanaoshuhudia mshtuko na hata kifo wakati wakipitia ukeketaji.
  • Tags

You can share this post!

Bondia Tyson Fury ataka mkewe amfyatulie watoto 10 wafunge...

Hii ndio siri ya kufaulu katika biashara

T L