Ukichoka na ndoa, fanya hivi ili kupata talaka
KUTAYARISHA kesi ya talaka sio ngumu ikiwa mtu ana sababu za kutosha kufanya hivyo. Mtu huanza kwa kuandaa kesi ambayo anaambatisha na ushahidi kuhusu kwa nini anataka talaka.
Kesi inaweza kutayarishwa na wakili au mtu binafsi ikiwa anajiwakilisha. Hata hivyo, inashauriwa mtu atafute huduma za kisheria kuandaa kesi ya talaka.
Stakabadhi zinazohitajika ni na hati ya kiapo kuunga kesi, taarifa yako ya ushahidi, orodha yako ya ushahidi na orodha yako ya mashahidi. Wakili wako pia atatayarisha notisi ya kufika mahakamani.
Inachukua takriban wiki mbili kwa Hakimu kutia saini notisi hiyo. Hii ni notisi rasmi inayoelekeza mshtakiwa kuijulisha mahakama ikiwa anapinga talaka au la. Ikiwa anapinga talaka, atakuwa na siku 15 za kujibu kesi.
Pindi mshtakiwa anapopokea stakabadhi za kesi ya talaka na notisi ya kufika kortini, anapewa siku 15 za kuamua iwapo atapinga au la. Kumbuka talaka nchini Kenya haiwezi kuwa kwa makubaliano, lazima ifike kortini na kufuata mchakato uliowekwa kisheria.
Baada ya siku 15 kupita, wakili huwa anawasilisha ombi kwa mahakama ithibitishe kesi na kusikilizwa kwake.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya talaka, mlalamishi hutoa ushahidi wake. Hii ni hatua muhimu ambayo mlalamishi au wakili wake huwa anawasilisha ushahidi unaoonyesha mahakama kwamba ndoa imevunjika kiasi cha kutorekebishwa.
Ikiwa talaka itapingwa, upande wa pili pia utaita mashahidi na kuwasilisha ushahidi na Mahakama itapanga tarehe ya hukumu.
Sababu za kutosha
Siku ya hukumu, mahakama huamua ikiwa kuna sababu za kutosha za kuvunja ndoa au la. Ikiwa mahakama itapata sababu za kutosha, itatoa amri ya kwanza ya talaka.
Hii ikishatolewa, mlalamishi hupatiwa mwezi mmoja ili kufikiria na kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo anataka ndoa ivunjwe au la.
Ndani ya mwezi huu, iwapo mlalamishi atabadilisha nia na kuamua kuokoa ndoa yake, anaweza kuijulisha mahakama na mahakama huondoa amri ya awali na kukuruhusu ndoa idumu.
Mwezi mmoja ukipita bila mtu kubadilisha nia, amri ya talaka kamili inatolewa na ndoa huwa imevunjwa rasmi na cheti cha talaka kutolewa.
Ndoa huvunjika kiasi cha kutoweza kutorekebishwa mtu akimuacha mume au mkewe kwa miaka mitatu.
Misingi mingine ya kuvunjika kwa ndoa kiasi cha kutoweza kuokolewa ni mke au mume akiwa katili kwa watoto wao au kumnyima mchumba haki zake.
Ndoa huchukuliwa kuwa imevunjika kabisa mume au mke akifungwa jela miaka saba au akifungwa jela maisha.
Sheria inasema kwamba mtu akifungwa jela maisha, ndoa yake huwa inavunjika kiwango cha kutoweza kurekebishwa na huu ni mojawapo wa misingi ambayo mahakama huzingatia kuamua kesi ya talaka.